Powered By Blogger

Sunday, November 27, 2011

Babu '67' afungwa kwa Kunyofoa kidole cha Mkewe.

MZEE Juma Iboma (67) wa kijiji cha Msisi tarafa ya Mtinko huko Singida, amehukumiwa kutumikia adhabu ya miezi mitatu jela, baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh 70,000 kwa kosa la kumng’ata mkewe kidole cha mkono na kukinyofoa.

Mzee huyo, alipewa adhabu hiyo majuzi na Mahakama ya Mwanzo Utemini mjini hapa. Awali ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa Iboma alitenda kosa hilo baada ya kuchukizwa na kitendo cha mkewe, Hawa Wawa (63), kumpa paka makande bila ruhusa yake.


Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Ferdinard Njau, alisema upande wa mashitaka ulithibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alifanya kitendo hicho na hivyo kumwona ana hatia.


"Baada ya Mahakama hii kukutia hatiani, unapewa adhabu ya kulipa faini ya Sh 20,000 na fidia kwa mlalamikaji ya Sh 50,000.


“Ni lazima uanze kulipa fidia kwanza, ukishindwa kulipa faini na fidia, utakwenda jela miezi mitatu," alisema Hakimu Njau. Mshitakiwa hakuweza kulipa faini wala fidia, hivyo kulazimika kwenda jela miezi mitatu ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wanaonyanyasa wake zao.


Hakimu Njau alipomwuliza Hawa, kama yuko tayari kurudiana na mumewe, alikataa kata kata akidai kuwa amechoka kung’atwa mara kwa mara na mumewe huyo. Chanz Habari leo.

Mh. JAJI SUMARI AZINDUA"SAUT LAW JOURNAL".

 Mh. Jaji sumari akionesha Jarida hilo la sheria

Wadau Mbalimbali waliohudhulio Uzinduzi huo



Mh.Jaji Sumari(Aliyashika Mkasi )akiwa na Sister Hellen mkurugenzi wa Utafiti na uchapishaji wakati wa uzinduzi huo.







Mh. Jaji mfawidhi Aishieli Sumari wa Mahakama Kuu Mwanza, alizindua jarida la sheria" Saint Augustine University Law Journal". linalotolewa na chuo kikuu cha Mtakatifu Sauti jijini Mwanza. Uzinduzi huo ulifanyika siku moja kabla ya Chuo hicho kuadhimisha na kuzalisha wahitimu wa kwanza wa shahada ya  kwanza na ya pili za sheria.

Akielezea umati wa wanazuoni na wanafunzi waliokusanyika katika uzinduzi huo Mh, Sumari alisema kwamba, jarida hilo la sheria lina umuhimu mkubwa sana kwa heshima na hadhi ya chuo husika, kwani ndio kielelezo cha ufanisi wa chuo hicho. Mh. huyo alizidi kusisitiza kwamba nae pia atakua tayari wakati wowote kuandika mambo mbalimbali ya kisheria, kwa manufaa za wasomaji wa jarida hilo.

Aidha, aliwataka waaadhiri wa Chuo hicho katika kitivo cha sheria na waandishi wa jarida hilo kutumia fursa walionayo katika uandishi wa habari mbalimabali za kisheria juu ya mabadiliko yanayoendelea katika jamii yetu hususani  mchakato mzima wa Katiba unaoendelea wakati watanzania wanakaribia kusheherekea miaka 50 ya uhuru. 

Hafla hiyo iliudhuriwa na wanafunzi pamoja na jopo la waadhiri wa chuo hicho na Mapema kabla ya  uzinduzi huo Mkuu wa Chuo hicho Fr. Kitima, Mkuu wa kitivo cha sheria ndugu, Kilangi pamoja na professa Mhalu, walimshukuru kwa nyakati tofauti Mh. sumari kwa kuacha majukumu yake na kuja katika tukio hilo la kihistoria katika Chuo hicho. Walisema Kwamba jarida hio ndilo kielelezo cha ukuaji wa chuo cha Sauti katika kitivo cha sheria.

kwa upande wake Mhadhiri wa chuo hicho, ndugu Innocent Ndanga alionesha kufurahishwa na uamuzi huo wa chuo wa kuchapicha jarida hilo la sheria, na alitoa changamoto kwamba jarida hilo litumike katika kuakisi matatizo mbalimbali ya kisheria yanayowakabili wananchi na jamii kwa ujumla.










Thursday, November 24, 2011

ENZI HIZO; MAHAKAMA NA MIAKA 50 YA UHURU

  
Mwaka 1977 Mwl. Julius Kambarage Nyerere alimuapisha Jaji Francis Lucas Nyalali kuwa Jaji Mkuu wa pili mzalendo baada ya Jaji Augostino . Jaji Nyalali alishika wadhifa huo hadi mwaka 2000   
Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipomuapisha Jaji Augostino Saidi kuwa Jaji Mkuu wa kwanza mzalendo mwaka 1971 kazi aliyoifanya hadi mwaka 1977. Kabla ya Mhe. Jaji Augostino Saidi kuwa Jaji Mkuu, wadhifa huo ulishikwa na Mhe. Jaji Philip T. Georges aliyekuwa raia kwa Jamaica.     

Wednesday, November 23, 2011

Anusurika kifungo kwa Kumuua Hawara aliyejaribu kumbaka bintiye.


 
Mama lucia Mayunga (umri haukuweza kufahamika mara moja)ameponeakwenda jela baada ya kumuua harawa yake Sadau Elikali  aliyetaka kumbaka binti wa mama huyo.  Mtuhumiwa huyo alipandishwa kizimbani  katika Mahakama kuu kanda ya Mwanza katika kesi no 31 ya Mwaka 2009 na kushtakiwa kwa kosa la kuuwa bila ya kukusidia kinyume cha kifungu cha 195 sura ya 16, kanuni ya adhabu.

Akiongoza upande wa mashtaka  Mahakamani hapo, wakili wa serikali bi, Zaituni mseti aliieleza mahakama hiyo kwamba mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo mnamo tarehe 27.02.2009 majira ya saa nne usiku huko wilayani sengerema.  Alieleza kwamba marehemu na mtuhumiwa walikua na mahusiano ya kimapenzi  kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya tukio hilo kutokea, na kwamba siku hiyo majira ya usiku marehemu aliingia nyumbani kwa  Mtuhumiwa bila taarifa ya mama huyo, aliyekua anaishi na watoto wawili wa mdogo wake mmoja wapo akiwa binti wa miaka 15 , kwa jina Magesa Mathias.

Wakili huyo msomi wa serikali, alizidi kueleza Mahakama hapo  , kwamba mara baada ya marehemu kuingia nyumbani kwa mshitakiwa bila ridhaa yake ,alienda  kwenye chumba cha watoto hao waliokua wamelala kisha kuanza kumnyanyua miguu  ya binti huyo mwanafunzi, ndipo binti huyo aliposhtuka na kuanza kupiga kelele. Hali hiyo iliwapelekea watoto hao kukimbia kwa balozi na kutoa taarifa ya tukio hilo.

Ilielezwa na upande wa mashtaka kwamba, baada ya mabinti hao kuondoka, Mtuhumiwa  aliyakua kwenye chumba kingine aliamka baada ya kusilia kelele hizo kisha alichukua fimbo na kuanza kumpiga marehemu  sehemu mbalimbali za mwili kiasi ambacho marehemu alipata majeraha makubwa kichani, yaliyopelekea kifo chake siku moja baadaye.

Akiongoza upande wa utetesi wakili wa Mtuhumiwa ndugu Rutaindurwa aliiomba Mahakama hiyo tukufu  imwachie mama huyo kwani  amekiri mahakamani hapo, na kujutia kutenda kosa hilo, vilevile  marehemu alijitakia kifo chake yeye mwenyewe kwani japokua alikua na mahusiano ya mtuhumiwa bado hakuridhika na kutaka kumbaka binti huyo ambaye ni mtoto wa mdogo wake mtuhumiwa, aliyekua akiishi nyumbani hapo.

Akitoa hukumu hiyo Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu, Mh. Sumari aisema  kwamba kwa kiasi kikubwa marehemu alisababisha kifo chake kwa tendo lake alilotaka kulifanya, pia alihatarisha maisha ya watoto hao waliolazimika kutemba usiku usiku kwenda kwa balozi. Hivyo, kwa busara ya Mahakama mama huyo aliachiliwa huru kwani aliua pasi kukusudia.

Mattaka kizimbani kwa matumizi mabaya ya fedha.

Aliyekua Mkurugenzi wa ATCL akiwa Chini ya ulinzi wa Askari polisi.
Aliyekua  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kuweka kumbukumbu za ununuzi wa magari chakavu yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Mbali ya Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa shirika hilo, Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, William Haji.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincon alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo kati ya Juni na Julai, 2007.

Katika shtaka la kwanza ambalo linawahusu wote watatu, ilidaiwa kuwa kati ya Juni na Julai, 2007 Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam washtakiwa kwa nafasi zao walishindwa kutunza kumbukumbu za taarifa za kukubali zabuni ya ununuzi wa magari chakavu 26.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa katika shtaka la pili ambalo pia linawahusu washtakiwa wote, kati ya Julai 2 na Agosti 23, 2007 kwa pamoja, walishindwa kufuata taratibu za ununuzi wa umma katika magari chakavu 26 yenye thamani ya Dola za Marekani 809,300,000 kutoka katika Kampuni ya Bin Dalmouk Morots Co. Ltd ya Dubai.

Katika shtaka la tatu linalomuhusu Mattaka, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23, 2007 akiwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, alitumia madaraka yake vibaya katika ununuzi wa magari hayo bila kuwepo kwa mkataba wa zabuni uliosainiwa na pande zote mbili na kuhakikiwa na bodi ya zabuni ya shirika hilo suala ambalo ni kinyume cha sheria.

Baada ya kusomwa mashtaka hayo, upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wa Serikali Oswald Tibabyekomya ulisema kuwa haupingi dhamana kwa washtakiwa lakini ukaitaka mahakama kuzingatia kifungu namba 148 (5) (e) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kwa mujibu wa kifungu hicho, mshtakiwa wa kosa linalozidi Sh10 milioni anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha alizoshtakiwa nazo kama dhamana.

Hata hivyo, upande wa utetezi uliokuwa unaongozwa na Mawakili, Peter Swai na Alex Mgongolwa ulipinga kifungu hicho kwa madai kuwa hakiendani na mashtaka yanayowakabili wateja wao.

“Tunapinga hoja za upande wa mashtaka kwa sababu katika mashtaka yanayowakabili wateja wetu hakuna mahala palipotajwa kwamba wamesababisha hasara ama wizi,” alisema Swai.

Mshtakiwa wa pili ambaye hakuwa na wakili, aliiomba mahakama impe dhamana kwa madai kuwa yeye ni mfanyakazi mwaminifu wa Serikali kwani ni mwanataaluma ambaye amesajiliwa na Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), anayekagua hesabu za Serikali na taasisi mbalimbali.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Mkazi, Rita Tarimo alikubaliana na hoja za upande wa utetezi kwamba mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hayahusiani na kusababisha hasara au wizi hivyo akatoa masharti ya dhamana.

Katika masharti hayo, kila mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini dhamana ya maneno ya Sh10 milioni.

Washtakiwa wote walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Desemba 5, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.Mattaka alistaafu utumishi wa umma Mei mwaka huu baada ya kuitumikia ATCL kwa miaka mitano. chanzo gazeti la Mwananchi.

Mahakama Kuu yatupilia Mbali kesi ya Ubunge, Mwibala.

Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi ya pingamizi uchaguzi wa ubunge Jimbo la Mwibara mkoani Mara, iliyofunguliwa na mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mahakama hiyo imemtangaza rasmi mgombea wa CCM, kwamba alishinda kihalali katika uchaguzi huo.

Aliyekua mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mwibara Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Chiriko Aron David, amepinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, juu ya kesi yake ya kupinga matokeo dhidi ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Kangi Lugola (CCM), na anatarajia kukata Rufaa katika Mahakama Kuu ya Rufaa.

Katika madai yake mgombea wa Chadema, alidai kuwa taratibu za uchaguzi zilikiukwa, ikiwa ni pamoja na mgombea wa CCM, kuanza kampeni mapema, vitendo vya rushwa, kutumia gari la ubalozi, kutishia wananchi kwa kuwafyatulia risasi na msimamizi wa uchaguzi hakufuata taratibu za uchaguzi huo.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa nne, Jaji Chocha alisema hakuna ushahidi wowote unaojitosheleza wa kutengua matokeo ya uchaguzi jimbo hilo, kwani mgombea wa CCM alishinda kihalali.

Alisema katika hoja zote zilizotolewa na upande wa mashitaka, ikiwemo hoja ya rushwa, mashahidi wote walioletwa hawakuziunga mkono moja kwa moja hoja hizo, na pia ushahidi wao ulipingana, ikiwa ni pamoja na wengine kutokujiamini, hali iliyoashilia kuwa huenda ulikuwa wa kupangwa.

Alisema kwa jinsi hiyo anaamini kuwa wananchi wa Jimbo la Mwibara, walitumia demokrasia yao vizuri kwa kuchagua mbunge waliyemuona kwamba anawafaa kuwaletea maendeleo na hivyo kuifungua kesi mahakamani ni kuwacheleweshea maendeleo yao.

Alisema katika maelezo ya mashahidi wote akiwemo shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji, hakuona kama gari la ubalozi lilikuwa na makosa kwani picha zilizopigwa kama kielelezo zilionesha gari hilo likiwa limesimama, hivyo haamini kama gari hilo lilikuwa kwenye kampeni ya mgombea wa CCM, kama ilivyodaiwa.

Kuhusu rushwa, Jaji Chocha wakati wa kesi inaendelea, hakuna shahidi ye yote aliyethibitisha moja kwa moja rushwa hiyo, aliipokea nani na hata waliopewa hawakufika mahakamani kuthibitisha hilo.
 
Hatima pekee iliyobaki kwa mgombea huyo wa Chadema ni kukuata rufaa Mahakama ya rufaa  au kuomba marejeo ya kesi hio.

Friday, November 18, 2011

Mwekezaji Akamatwa siku ya Harusi kwa kuoa Mwanafunzi na Kushitakiwa.

RAIA wa Oman ambaye inadaiwa kuwa ni mwekezaji wa Kampuni ya Madini ya Katavi Gold Mine, Seif Khalid Abdallah (41), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda akikabiliwa na mashitaka ya kumuoa mwanafunzi kwa niaba ya mdogo wake.

Katika kesi hiyo, mwekezaji huyo ameunganishwa na baba wa mwanafunzi huyo, Salum Esri (35) ambao kwa pamoja walifikishwa juzi katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu, Richard Kasele .


Kwa Mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Phinias Majula, mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Esri, mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Madukani mjini Mpanda ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi aliyeolewa.


Esri anakabiliwa na mashitaka ya kumwozesha binti yake huyo ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza.


Aidha mtuhumiwa wa pili Seif ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Singililwa eneo ambalo kampuni ya Katavi ya Gold Mine inachimba madini anashitakiwa kwa kosa la kusaidia na kuwezesha ndoa kwa mdogo wake aitwaye Ally Khalid Abdallah ambaye hajapatikana.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Seif alifunga ndoa na mwanafunzi huyo wa Kidato cha Kwanza kwa niaba ya mdogo wake ambaye kwa sasa hajulikani mahali alipo.


Watuhumiwa wote walikana mashtaka hayo na wako nje baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ambapo kesi yao hiyo itatajwa tena Desemba 5, mwaka huu.


Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kati ya Mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu ambapo walipanga mipango ya kumwozesha mwanafunzi huyo.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Seif alikamatwa Jumapili saa 2.30 usiku katika sherehe hiyo ya harusi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Huria mjini humo.


Mwendesha Mashtaka Majula alidai mahakamani hapo kuwa baada ya’ maharusi" kuingia ukumbini na ratiba kufuatwa kwa muda, timu hiyo ya askari iliwaweka chini ya ulinzi Seif na bibi harusi (mwanafunzi) na kuwachukua hadi Kituo cha Polisi mjini Mpanda kwa mahojiano.
chanzo Habari leo.

Bunge lapitisha Muswada wa katiba Mpya.

Mh. Makinda
BUNGE limeupitisha kwa hoihoi, nderemo na vifijo, Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, huku Serikali ikisisitiza kuwa mchakato wa Muswada huo ulifuata taratibu zote bila kukiuka Katiba.

Pia Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, amesisitiza kuwa mtu atakayekwamisha utekelezaji wake, atakabiliwa na adhabu kali na kubainisha kuwa adhabu katika Muswada huo imeongezwa kutokana na hali halisi ya matukio ya kisiasa yanayoendelea.


Wakati akihitimisha jana hoja ya Muswada huo bungeni, Spika Anne Makinda, alisema hajui sababu halisi ya wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi, kususa mjadala wa Muswada huo, na hata alipomwuliza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, kuhusu suala hilo hakuwa na majibu.


Jana katika mkutano wa tano, kikao cha tisa saa saba mchana, wabunge wa CCM na wa CUF kwa pamoja waliboresha vifungu vya Muswada huo kwa kuongeza vingine vitatu na kuupitisha.


Awali wakati akijibu hoja za michango ya wabunge iliyotolewa wakati wa mjadala kuhusu Muswada huo, Kombani alisema kuwasilishwa kwa Muswada huo bungeni ni halali na kwamba haukupaswa kusomwa kwa mara ya kwanza kama inavyodaiwa.


Alisema Muswada huo hauna tofauti na wa awali na ushahidi uko kwenye kipengele cha maudhui ambacho hakijabadilishwa na katika Muswada wa sasa kilichofanyika ni kuuboresha kutokana na maoni ya wadau.


Aidha, alisisitiza kuwa madai ya Kambi ya Upinzani kutaka Rais asiteue Tume hayawezekani kubadilishwa, kwa kuwa ukweli unabaki kwamba Rais ni Mkuu wa Nchi na ndiye mwenye mamlaka ya masuala yote makubwa yanayotokea nchini.


Kuhusu hoja ya vyama vya siasa kushiriki kuteua Tume, alisema haiwezekani kwa kuwa kila chama kina ilani yake, hivyo iwapo itatokea kutofautiana, hakuna kitakachofanyika zaidi ya vurugu na kutukanana.


Tundu Lissu apotosha “Naomba hapa nihadharishe Kambi Rasmi ya Upinzani iwe makini na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na kupitia matamko yake, kabla ya kuwasilishwa kwani, maoni aliyotoa katika mjadala huu sina uhakika kama amehusisha chama, mengi ni yake,” alisema Kombani.


Aidha, alisema mambo mengi yamepotoshwa na Msemaji huyo, kutokana na ukweli kuwa amekuwa hauhudhurii vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambamo ni mjumbe, matokeo yake amekuwa akipotosha kuhusu utendaji wa Kamati.


Alisema asilimia kubwa ya maoni yaliyotolewa dhidi ya Muswada huo yamepotoshwa na kuwataka Watanzania wasikubali kuchonganishwa na kuvunjiwa amani na umoja wao.


Mwanasheria Mkuu Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema anashangazwa na hoja ya Muswada huo kusomwa mara ya kwanza wakati ulishasomwa mara ya kwanza, na kilichofanyika ni kuuboresha kutokana na maoni ya wadau.


“Inashangaza Muswada huu ndio umeng’ang’aniwa usomwe eti kwa mara ya kwanza, mbona Muswada wa Ununuzi wa Umma uliletwa hapa mwaka jana, juzi ukasomwa kwa mara ya pili na haukulalamikiwa, hata Muswada wa Uchaguzi vivyo hivyo,” alisema.


Alisisitiza kuwa kutokana na hali halisi ilivyo, adhabu iliyokuwapo kwenye kifungu cha adhabu kwa atakayekwamisha utekelezaji wa Muswada huo, imeongezwa kutoka kifungo cha miaka mitatu hadi saba na faini ya Sh milioni tano hadi Sh milioni 15.


Akihitimisha mjadala huo, Makinda alisema Muswada huo ulipita kihalali kwa kufuata taratibu zote na kanuni za Bunge ikiwamo Katiba pamoja na wananchi kushirikishwa kupitia mikutano ya hadhara.


Alisema kitendo cha Chadema na NCCR-Mageuzi kutoshiriki kimewanyima wananchi wao haki ya kusikiliza michango yao iwe ya kukosoa au kuboresha ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kuzingatiwa na kusikilizwa.


“Jana (juzi) nilikutana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani (Mbowe) nilimwuliza sababu za kutoka ili nijue kama nimekosea sehemu basi nijisahihishe, ingawa tayari nilishajichunguza na kuuliza wataalamu wangu na kukuta sijakosea chochote.


“Kusema ukweli Mbowe hakuniambia chochote kuhusu sababu halisi za wao kutoka, ndiyo maana nasema hawa wamewakosesha haki wananchi wao, kama wanapinga wangebaki ndani wawasilishe mawazo yao na kwa uchache wao yangesikilizwa,” alisisitiza. Chanzo Habari leo.

Profesa Maina: Achaguliwa kuwa Mjumbe Kanisheni ya Sheria UN.

MHADHIRI Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina Peter, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Sheria za Kimataifa (ILC).

Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika mkutano uliofanyika juzi katika makao makuu yake, walipiga kura ya siri kuchagua wajumbe 34 kati ya 49 waliotakiwa kuingia katika Kamisheni hiyo.


Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Balozi Nassir Abdulaziz Al - Nasser alimtangaza Profesa Peter wa Tanzania, kuwa ni mmoja wa wagombea tisa kati ya 13 kutoka Afrika ambao walishinda na kuingia katika Kamisheni hiyo.


Profesa Peter alishinda uchaguzi huo, uliokuwa na ushindani mkubwa akichuana na wagombea wengine 13 wakiwamo mabalozi na watu mashuhuri kama aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Amos Wako.


Wagombea wengine mbali ya tisa wa Afrika, walikuwa ni wanane wa kundi la nchi za Asia, watatu kundi la Ulaya Mashariki, sita kundi la Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean na wanane wa Ulaya ya Magharibi na nchi zingine.


Profesa Peter, atakuwa mjumbe wa Kamisheni hiyo kwa miaka mitano kuanzia Januari 2012. Mbali ya Tanzania, wengine kutoka kundi la Afrika walioshinda ni wa Afrika Kusini, Misri, Msumbiji, Nigeria, Algeria, Kenya, Libya na Cameroon


Ushindi wa Profesa Peter ulitokana uthubutu, wasifu na weledi wake binafsi, uratibu na ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa Tanzania katika UN ambako, maofisa wake wakiongozwa na Balozi Ombeni Sefue, walifanya kazi kubwa na maandalizi mazuri ya kufanikisha uchaguzi huo.


Profesa Peter akiongozwa na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania katika UN anayehusika na Kamati ya Sita ya Masuala ya Sheria na Uchanguzi, alifanya kampeni kwa takribani wiki nzima akikutana na mabalozi na maofisa mbalimbali wa UN.

Tuesday, November 8, 2011

Msajili azitaka nchi za EAC ziiamini mahakama

MSAJILI wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Dk. John Ruhangisa ametoa mwito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujenga imani kwa mahakama hiyo ili kuiwezesha kushughulikia ukiukwaji wa haki kikamilifu.

“Kutokana na uchunguzi unaofanywa ni wazi kwamba baadhi ya wadau hawatambui nafasi muhimu iliyopewa mahakama hii na Mkataba uliounda Jumuiya hii,’’ alisema Jaji Ruhangisa.

Msajili huyo wa EACJ alikuwa akizungumza na wajumbe wa warsha ya kwanza juu ya majukumu ya EACJ katika kuukuza mtangamano wa nchi wanachama, mjini Kampala nchini Uganda juzi.

Warsha hiyo, yenye kauli mbiu ‘Jukumu na nafasi ya Mahakama katika ajenda ya mtangamanao wa EAC’, ilihudhuriwa na majaji wakuu kutoka nchi wanachama, wabunge wa Bunge la EAC, wasajili wa mahakama za kitaifa, wakuu wa taasisi za EAC na wajumbe wa asasi za kiraia.

Ruhangisa alihadharisha kwamba mahakama hiyo isionekana kama ni wapinzani kila inapotoa uamuzi usiowafurahisha watunga sera.

“Mahakama inatoa tafsiri na kutumia vifungu vya sheria kutoka katika Mkataba ili kufikia malengo ya EAC na siyo kwa lengo la kumfurahisha mdau anayeguswa na uamuzi wa mahakama,” alifafanua.

Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda, Eriya Kategaya, alisema katika warsha hiyo kwamba kadiri Itifaki ya EACJ inavyokaribia kukamilishwa, nchi wanachama hazina budi pia kuwa tayari kuachia sehemu ya mamlaka za mahakama zao za kitaifa kwa ajili ya mahakama hiyo ya Kanda.

“Ni dhahiri kwamba nchi wanachama zitachambua sheria zake za kitaifa zinazohusiana na uongozi wa mahakama na kuzioanisha na za EACJ pindi Itifaki ya mahakama hiyo ya Kanda itakapokamilika,’’ alifafanua Kategaya. Chanzo Habari leo.