Powered By Blogger

Friday, November 18, 2011

Mwekezaji Akamatwa siku ya Harusi kwa kuoa Mwanafunzi na Kushitakiwa.

RAIA wa Oman ambaye inadaiwa kuwa ni mwekezaji wa Kampuni ya Madini ya Katavi Gold Mine, Seif Khalid Abdallah (41), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda akikabiliwa na mashitaka ya kumuoa mwanafunzi kwa niaba ya mdogo wake.

Katika kesi hiyo, mwekezaji huyo ameunganishwa na baba wa mwanafunzi huyo, Salum Esri (35) ambao kwa pamoja walifikishwa juzi katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu, Richard Kasele .


Kwa Mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Phinias Majula, mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Esri, mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Madukani mjini Mpanda ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi aliyeolewa.


Esri anakabiliwa na mashitaka ya kumwozesha binti yake huyo ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza.


Aidha mtuhumiwa wa pili Seif ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Singililwa eneo ambalo kampuni ya Katavi ya Gold Mine inachimba madini anashitakiwa kwa kosa la kusaidia na kuwezesha ndoa kwa mdogo wake aitwaye Ally Khalid Abdallah ambaye hajapatikana.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Seif alifunga ndoa na mwanafunzi huyo wa Kidato cha Kwanza kwa niaba ya mdogo wake ambaye kwa sasa hajulikani mahali alipo.


Watuhumiwa wote walikana mashtaka hayo na wako nje baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ambapo kesi yao hiyo itatajwa tena Desemba 5, mwaka huu.


Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kati ya Mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu ambapo walipanga mipango ya kumwozesha mwanafunzi huyo.


Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Seif alikamatwa Jumapili saa 2.30 usiku katika sherehe hiyo ya harusi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Huria mjini humo.


Mwendesha Mashtaka Majula alidai mahakamani hapo kuwa baada ya’ maharusi" kuingia ukumbini na ratiba kufuatwa kwa muda, timu hiyo ya askari iliwaweka chini ya ulinzi Seif na bibi harusi (mwanafunzi) na kuwachukua hadi Kituo cha Polisi mjini Mpanda kwa mahojiano.
chanzo Habari leo.

No comments: