Powered By Blogger

Thursday, July 28, 2011

TUNDU LISSU,LEMA NA BABA MCHUNGAJI WATIMULIA BUNGENI.

Mh.Job Ndugai( Naibu Spika)

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwatimua kikaoni wabunge watatu wa Chadema. Wabunge hao waliofukuzwa bungeni jana asubuhi ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Tundu Lissu (Singida Mashariki).Walifukuzwa kutokana na kile Naibu Spika Ndugai alichoeleza kuwa ni kukiuka Kanuni za Bunge zinazowataka kutozungumza chochote ndani ya bunge bila idhini ya kiti cha spika. 

 Tukio la kufukuzwa kwa wabunge hao limekuja siku moja baada ya mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba, kumfukuza bungeni Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema),  baada ya kukaidi amri iliyomtaka akae chini wakati akiomba mwongozo.Wakati tukio hilo la juzi likiwa limeonyesha taswira mbaya kwa mhimili huo wa dola wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali,  jana Lissu, Lema na Msigwa kwa pamoja walipewa adhabu hiyo baada ya kubishana na Ndugai bila utaratibu.

Katika tukio hilo, wabunge hao walipinga kile walichokiita  muda mrefu aliokuwa amepewa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kueleza kukiukwa kwa kanuni za Bunge.Lukuvi aliomba kupewa mwongozo wa Naibu Spika mara baada ya Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kusoma hotuba ya maoni ya kambi ya upinzani kuhusu wizara hiyo ambayo ilikuwa na shutuma nyingi dhidi ya Serikali, hasa Jeshi la Polisi

 "Mwongozo wa Spika, mwongozo wa Spika........Mheshimiwa Naibu Spika sasa......," alisikika sauti ya Lissu wakati Lukuvi akiendelea kuzungumza, hali iliyosababisha Naibu Spika kusimama na kumuonya. 

 "Nimesema hairuhusiwi kuwasha mic (kinasa sauti) yako bila ruhusa yangu...waziri endelea...." alisema Ndugai Baada ya kauli hiyo, ndipo vipaza sauti ambavyo haikuwa rahisi kufahamu idadi yake viliwashwa na sauti kuanza kusikika zikimkosoa Ndugai kwamba anapendelea, kwani Lukuvi alipewa muda mrefu wa kuomba utaratibu tofauti na msimamo wa awali aliokuwa ameutoa Naibu Spika huyo

 "Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ..." ilisikika sauti ya Msigwa huku sauti nyingine kadha wa kadha zikisikika bila mpangilio hali iliyosababisha taharuki na kuathiri shughuli za Bunge. Sauti hizo zilisababisha mzozo na kukosekana kwa utulivu na usikivu bungeni hivyo Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM) akaamua kutumia rungu lake kuwafukuza wabunge hao watatu kutoka ndani ya Ukumbi wa Bunge.

 "Nilishasema tangu asubuhi na nimewakumbusha kwamba hakuna mbunge anayeruhusiwa kuwasha microphone (kinasa sauti) na kuzungumza bila idhini ya kiti, sasa naanza kutumia kanuni, nimewaona wabunge watatu, Mheshimiwa Lissu, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa na Mheshimiwa Lema, tokeni nje," aliamuru Ndugai na kuongeza:

"Tena nitafuatilia kuhakikisha kwamba mnaondolewa kabisa nje ya geti (lango kuu) la kuingilia bungeni, muondoke kabisa katika eneo hili."

Kufuatia kauli hiyo, wabunge hao walitoka nje huku wakisindikizwa na askari (wapambe) wa Bunge hadi nje ya ukumbi na baadaye kuondolewa kabisa katika eneo hilo, hivyo kutokuwa na fursa hata ya kuzungumza na waandishi wa habari

 Tafrani hiyo ilishuhudiwa na IGP Mwema pamoja na wakuu wa taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo jana iliwasilisha hotuba yake kwa mwaka 2011/2012.

 Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, wabunge hao jana hawakuruhusiwa kurejea tena bungeni siku hiyo, badala yake watarejea leo kwani adhabu yao ni kukosa kikao kwa siku moja tu.

Mahakama yamwachia mtuhumiwa wa Richmond.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mfanyabiashara Naeem Gire aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kughushi na kutoa taarifa za uongo kuhusu kampuni ya Richmond. Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Wariyalwande Lema aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo. Hakimu Lema alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi ya mashtaka waliyomshtaki nayo Gire. 

Alisema ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa ni dhahifu na kwamba usingeweza kumfanya mshtakiwa huyo ajitetee. “Naiondoa kesi hii chini ya kifungu namba 230 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwasababu upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa,”alisema Hakimu Lema.

 Hakimu Lema alisema hakuna sehemu yoyote ambayo mshtakiwa huyo aligushi na kwamba vitu vyote vilifanywa na Mohamed Gire ambaye ni kaka wa mfanyabiashara huyo.

 Baada ya uamuzi huo, upande wa mashtaka kupitia kwa Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro ulisema utakata rufaa kupinga hukumu hiyo. “Tunaomba tupewe nakala ya mwenendo wa kesi na nakala ya hukumu kwa ajili ya kwenda ngazi za juu zaidi,”alisema Kimaro.Gire alikuwa akidaiwa kuwa, Juni, 2006 jijini Dar es Salaam alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya Serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme ili apewe zabuni.

Mfanyabiashara huyo pia alikuwa akidaiwa  kuwasilisha hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, 2006 ikimuonesha kuwa aliruhusiwa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Hemed Gire ambaye ni kaka yake kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.Source Mwananchi

Wednesday, July 27, 2011

WENJE ATOLEWA KWA NGUVU, MBUNGE CCM ANUSRIKA KUPIGWA

Wabunge katika zogo
MBUNGE wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, jana alijikuta akitolewa bungeni na askari (wapambe) wa Bunge waliotii amri ya Mwenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba, aliyeongoza kikao siku hiyo.Katika tukio ambalo ni la kwanza kutokea tangu kuanza kwa Bunge la Kumi linaloongozwa na Spika Anne Makinda, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alinusurika kupigwa na wabunge wa kambi ya upinzani baada ya kuwakejeli Chadena akisema waache mambo ya kitoto.

Mabumba alitoa amri ya Wenje kutolewa nje baada kukaidi amri ya Mabumba kumtaka akae chini mbunge huyo wa Nyamagana alipokuwa akiomba mwongozo, katikati ya mabishano yaliyokuwa yakiwajumuisha wabunge wengine wakati huo.Wakati Wenje akisisitiza kuomba mwongozo kwa maelezo kwamba jambo analotaka kusema "lina maslahi ya nchi", Mabumba ghafla aliwaita askari (wapambe) wa Bunge na kuwaamuru wamtoe nje kwa kukiuka kanuni za Bunge.

Kabla ya kuwaita askari hao, Mabumba ambaye ni Mbunge wa Dole alikuwa amemwamuru mara tatu Wenje akae chini, lakini hakutii akisema: "Nina jambo la dharura ambalo ni kwa maslahi ya Taifa"."Sargent Ant Arms, mtoe nje mheshimiwa Wenje," alisema Mabumba na hapo askari watatu waliingia na kumtoa nje Wenje, tukio ambalo liliacha kukiwa hakuna utulivu bungeni.

Pamoja na kusindikizwa na askari wa Bunge, baadhi ya wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi walitoka nje wakimsindikiza Wenje.Walipofika nje ya ukumbi wa Bunge walianza kumlalamika kwamba, Mabumba ameshindwa kuongoza Bunge na kudai kuwa anaonyesha upendeleo wa wazi katika uendeshaji wa vikao vya chombo hicho.

Nje ya Ukumbi wa Bunge
Nje ya Ukumbi wa Bunge ilizuka tafrani nyingine iliyosababisha Mbunge Filikunjombe (CCM), kunusurika kupokea kichapo kutoka kwa wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi baada ya kuingilia mazungumzo yao wakati wanajadili suala la Wenje kutimuliwa ukumbini.

“Tatizo lenu ninyi wabunge wa Chadema mnaishia kuwa wabishi kila wakati, jambo ambalo linawapotezea heshima kwa wananchi,’’ alisema Filikunjombe na kuongeza: “Acheni mambo ya kitoto rudini ndani kuendelea na Bunge. Sio kila siku ninyi Chadema tu, watu wamewachoka.’’

Kauli ya ilikuwa kama kumwaga petroli kwenye moto, kwani kundi la wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi ambao kwa wakati huo wakiongozwa na Moses Machali (Kasulu Mjini NCCR), walimvaa kama nyuki mbunge huyo na kuanza kurushiana maneno makali.

“We mjinga kweli, hapa sio wabunge wa Chadema hata sisi wa NCCR-Mageuzi tupo tunachojadili ni maslahi ya nchi sio ushabiki wa vyama, toka hapa mshamba wewe,’’ alisema Machali.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Kiwanga, alimwambia Filikunjombe aache hadithi za kijinga kwani wananchi wa eneo lake wanaporwa chuma, lakini yeye (Filikunjombe) anashindwa kuwatetea badala yake anarukia mambo yasiyomuhusu.“Tuondolee ujinga wako hapa, wananchi wako katika maeneo ya Liganga wanaporwa mali usiku na mchana unashindwa kuwatetea leo unapotuambia tuna akili ya kitoto, hivi unataka Watanzania wafe ili ninyi mshangailie,’’alisema Kiwanga.
Wabunge wengine waliomwandama zaidi Mbunge huyo ni, Machali (NCCR-Mageuzi), Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), Mariam Msabaha na Susan Kiwanga wote wa Viti Maalum (Chadema) ambao walimzingira mbunge huyo na kuanza kumrushia maneno ya kejeli.Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya wabunge wengine wa Chadema, Godbles Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Vicent Nyerere (Musoma Mjini) walipoingilia ugomvi huo na kutaka Filikunjombe awaombe radhi, lakini alikataa.Kama si busara iliyotumiwa na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM) hali ingekuwa mbaya kwani idadi ya wabunge wa Chadema ilipozidi yalisika maneno kuwa mbunge huyo apigwe, ndipo Nkamia alipofika na kuokoa jahazi akimtaka Filikunjombe aondoke katika eneo hilo.Chanzo Gazeti la Mwananchi.

Tuesday, July 26, 2011

Cocain ya mil. 700 yabambwa Tanga

POLISI Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya, kimekamata dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye thamani ya sh. milioni 700 ndani ya basi Raha leo na Tawaqal.Dawa hizo zilikamatwa katika matukio mawili tofauti baada ya Kikosi cha Kupamba na Dawa za Kulenya kuwatilia shaka watuhumiwa hao.

Kwa mujibu wa Mkuu Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Bw. Jafary Mohamed, watu saba wanashikiliwa katika matikio hayo.Alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea Jumamosi ndani ya basi la Raha Leo katika eneo la Kabuku ambapo polisi iliwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na kilo 12 za Cocain.

Kukamatwa kwa dawa hizo kutokana na mtego uliowekwa na kikosi hicho kwa kuwatilia shaka baadhi ya watu akiwemo mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam.Mkuu huyo wa upelelezi alisema mfanyabiashara huyo alikamatwa Jumamosi saa 5:30 asubuhi, katika kizuizi cha Polisi Tanga baada ya kupekuliwa na kukutwa na baadhi ya dawa kwenye mfuko.

Alisema kuwa kikosi hicho, kilifuatilia nyendo za mfanyabiashara huyo ambaye alionekana katika Kituo Kikuu cha cha Mabasi Tanga na akimkabidhi mkazi mmoja wa Pongwe begi lililokuwa na dawa na kupanda basi la Raha Leo lililokuwa likitoka Mombasa kwenda Dar es Salaam.

Mfanyabiashara huyo alianza safari akiwa nyuma ya basi hilo akiwa kwenye gari ndogo aina ya Baloon.

Hata hivyo, basi hilo lilikamatwa baada ya kufika kwenye mizani ya Tanga na katika upekuzi walibaini kuwepo kwa dawa hizo kwenye begi.Alisema mfanyabiashara huyo alikamatwa akiwa na mifuko mikubwa 12 ya dawa za kulevya.

"Ni mapema kuwataja majina yao kwa kuwa bado kuna watuhumiwa wengine tunaendelea kuwatafuta kutokana na kushiriki kwenye uuzaji na usambazaji wa dawa hizo," alisema Bw. Mohamed.Alisema katika tukio la pili, jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wanne wakisafirisha dawa za kulevya kwenye basi la Tawaqal kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa na kilo tatu na mara baada ya kukamilika kwa upelelezi watafikishwa mahakamani.

Thursday, July 14, 2011

Anusuriki kifungo kwa kumuua mumewe kwa kipigo

Mshtakiwa Letisia Kasabuka amenusurika kwenda jela kwa kumuua mumewe bila ya kukusudia kinyume na  kifungu cha 195 na 198 Cha sheria ya makosa ya Jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akiieleza Mahakama wakili wa Serikali Ndugu Kamala, alisema kwamba mnamo  tarehe 28.12.2008 majira ya usiku mtuhumiwa na marehemu mumewe walikua nyumbani kwao huko Geita. Wakiwa nyumbani hapo ugomvi ulizuka baina yao ivyo kupelekea kuumizana.

Wakili huyo, aliendelea kukiambia Kikao hicho cha Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kwamba hali ya mume wa mshtakiwa ilidhoofu kesho yake kutokana na kipigo kilichotolewa na mama huyo hali iliyolazimu kupelekwa Hospitalini, kabla ya kuhamishwa kwa mganga wa kienyeji.

Mshtakiwa alikiri mbele ya Mh.Jaji G.K.Mwakipesile hivyo wakili wake wa utetezi, kuiomba mahakama hiyo tukufu imuonee huruma mtuhumiwa huyo kwani ni mama wa watoto wanne na alifanya kosa hilo bila ya kukusudia pia ana motto mdogo aliyemuacha na mwaka mmoja . Kwa upande wake ndugu kamala aliiomba Mahakama  itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa akina mama wenye tabia ya kupiga waume zao.


Hata hivyo Mh.Jaji G.K Mwakipesile aliamuru mtuhumiwa kuachiwa huru, kwa kuua bila ya kukusudia. Chini ya kifungu cha 326(1)b cha Sheria ya mwenendo wa Mashtaka Sura ya 20, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Sunday, July 10, 2011

Mabinti wa familia moja wabakwa, mmoja auawa.

WASICHANA wawili wa familia moja, wakazi wa Kitongoji cha Nyabirongo, Kijiji cha Gibaso, Kata ya Nyarukoba, wilayani Tarime, wamebakwa na watu wanaosakiwa kuwa majambazi, kisha kuwashambulia kwa kuwakatakata mapanga na kusababisha kifo cha binti mmoja.Majambazi hao waliwavamia mabinti hao kwenye nyumba walikokuwa wamelala, waliwabaka kasha kuwakatakata mapanga na kupora Sh58,000.

Kutokana na majeraha ya mapanga waliyopata, wasichana hao walikimbizwa Hospitali ya Masanga na mmoja alifariki akipatiwa matibabu.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Deus Kato, alisema tukio hilo lilitokea Julai 7, mwaka huu saa 5:00 usiku.Wakizungumza nyumbani kwa Mwera Wantae jana, mmoja wa mashuhuda Daniel Nyandege, alisema walisikia sauti ya yowe nyumbani hapo hatua iliyowalazimu kukimbilia eneo hilo.

“Ilikuwa muda wa saa 5:00 usiku nikasikia sauti ya yowe, ilinibidi nikimbie hadi eneo la tukio nilipofika ndani nilimkuta mama wa familia akiwa analia, huku akiwa amefungwa mikono yote miwili, nilipomuuliza aliniambia niingie ndani walikolala mabinti wake, nilipoingia nilikuta wakiwa wamejeruhiwa kwa kukatwakatwa mapanga huku nguo zao za ndani zikiwa zimetupwa chini na magauni yakiwa yamesogezwa hadi juu ya kifua, sehemu za siri zikiwa wazi,” alisema Nyandege.

Shuhuda mwingine, Mjumbe wa kitongoji hicho, Simion Chacha, alisema alipofika alishangaa kuona damu ikimiminika na kwamba, alimuona mmoja wa mabinti hao akiwa na majeraha matatu ya kukatwakatwa panga.
Hata hivyo, mabinti hao wakiwa Hospitali ya Masanga wakipatiwa matibabu, mdogo alipoteza maisha na mwingine anaendelea na matibabu.

Kamanda Kato alisema hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba, polisi kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kuwasaka wahusika.Source gazeti la Mwananchi.

Saturday, July 9, 2011

Afande akiwa na mtuhumiwa wake.

Askari wa Usalama barabarani akiwa na dereva wa daladala ambaye alifanya kosa na kukimbia kwa kushani askari huyo hakumuona na ndipo alipomfuata katika kituo alichokua  amepaki daladala lake kisha kumkamata ma kumpeleka kituoni.Source michuzi Blog.


                                                                       

Mh.Joseph Mbilinyi akamatwa, aachiwa huru, atoa Tamko Rasmi!

Mh.Sugu Mara baada ya ya kuachiwa kwa Dhamana kituo cha polisi Mbeya


Jana tarehe 8 Julai 2011 Polisi walinikamata kwa kile walichokiita kuwa ni kufanya mkutano bila kibali.Hata hivyo, mtiririko wa matukio unaonyesha kwamba polisi walisukumwa na sababu nyingine kwa kuwa suala la taarifa kupelekwa polisi kama sheria zinavyohitaji lilishashughulikiwa na viongozi wa CHADEMA mkoa na wilaya ya Mbeya Mjini.

Leo tarehe 9 Julai 2011 pamoja na kutolewa kwa dhamana polisi wameonyesha nia ya kutaka kuzuia tamasha la wazi la bure ( ‘Burudani Nyumbani’) ambalo wasanii mbalimbali walikuwa walifanye kwa mwito wangu kwa ajili ya kutoa burudani na kuhamasisha maendeleo. Polisi wameonyesha vitendo vya kutaka leo kufanyike tamasha la fiesta pekee wakati ambapo matamasha haya yote mawili yameandaliwa na wadau tofauti katika maeneo tofauti.


Mpaka wakati huu ninapotoa taarifa hii wananchi wengi wamejikusanya katika uwanja wa Ruanda Nzovwe ambao ni maarufu kama Uwanja wa Dr Slaa wakisubiri tamasha hilo lakini polisi wameonyesha dhamira ya kutaka kuwatawanya.Maneno na vitendo vya Jeshi la Polisi vinaelekea kuwa na uhusiano na kauli ambayo niliitoa hivi karibuni kupitia mtandao wa Facebook ya kutohitaji tamasha la Fiesta kufanyika Mbeya.Katika mazingira haya ni muhimu nikaeleza tu kuwa kauli yangu kuhusu Fiesta ilikuwa na madhumuni ya kuanzisha mjadala kuhusiana na suala zima la wizi na unyonyaji uliopo kwenye Sanaa, ambao sio tu unawanyima haki Wasanii, bali pia kukosesha mapato kwa Serikali ambayo yangetokana na kodi kupitia Sanaa ikiwemo muziki.

Nilifanya hivyo baada ya tamasha hilo kutangazwa kufanyika katika eneo ambalo wananchi wamenipa wajibu wa uongozi wa kuwatumikia na kuwawakilisha. Hivyo kwa niaba ya wananchi wa Mbeya Mjini wanaokosa mapato katika sanaa na wasanii wa Mbeya wanaokosa fursa kutokana na vikwazo nilichukua uamuzi wa kuwakilisha kupaza sauti kama ambavyo nimekuwa nikipaza sauti katika masuala mengine yanayogusa umma kama viwanda, kilimo, barabara za Mbeya Mjini na Haki za wanafunzi wa Elimu ya Juu pamoja na makundi mengine katika jamii.

Niliamua kupaza sauti katika hili kupitia Fiesta, kwa kuwa waandaji wake kimsingi ni sehemu ya vyanzo vya maovu kwenye maendeleo ya muziki hapa nchini. Fiesta ikiwa kitovu cha uonezi kwani hata Wasanii wanaoshiriki halipwi ipasavyo au hawalipwi kabisa. Na hii ni kutokana na wao kutumia njia haramu kuhodhi (monopolise)biashara ya muziki hapa nchini, huku wakiwanyima nafasi watanzania wengi kutumia vipaji na ubunifu wao kwenye biashara ya muziki.Waandaji wa Fiesta ndio wenye redio ya Clouds, Kampuni ya promotion ya Primetime, na pia wanahusika na N.G.O ya THT, waandaji wa matamasha ya injili, ikiwemo kuwa na ushirika katika Tamasha la Pasaka.Huku wakiwa na ushawishi wa hila kwenye Kili Music Awards (One Call Promotion) na mambo mengine yote muhimu yanayohusu Sanaa. Ikiwemo ujumbe wa bodi kwenye Tamasha la majahazi, Zanzibar. Lisingekuwa jambo baya kama wangetumia nafasi hizo kwa haki na maendeleo ya sanaa.

Kutokana na haya, kwa miaka mingi himaya (“empire”) hii imetumia nafasi yake dhalimu kukandamiza watu wengine hasa Wasanii. Kwa mfano kama Msanii hayupo kwenye hiyo “himaya” yao basi hana nafasi ya kutimiza ndoto yake. Na iwapo Msanii hakubaliani na taratibu zao au malipo finyu wanayowalipa Wasanii, basi watahakikisha wanampiga vita na hatimaye kuhujumu usanii wake ili atoweke, kwa kuwa tu hakubaliani nao. Msanii hana haki ya kufanya majadiliano ya kibiashara mbele yao. “Empire” hii imehodhi mpaka makampuni ya udhamini hapa nchini, ambapo makampuni haya yamekuwa magumu kutoa udhamini kwa wadau wengine kwa kuwa tu wao ni washirika wa “Empire” hii.

Walifikia hatua ya kuhodhi mpaka biashara ya usambazaji kwa “Wadosi” ambapo bila ya wao kuruhusu basi Msanii yeyote kazi yake haipewi nafasi ya kusambazwa wala kusikika. Hata kama nyimbo au album yake ni nzuri kwa kiasi gani.Kibaya zaidi wamehodhi mpaka nia njema ya Rais Kikwete katika kusaidia Sanaa na Wasanii. Mfano ni Studio ambayo Rais kupitia Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano alitangaza kuwa amewapa Wasanii wa Tanzania, lakini baadaye tukashangaa kusikia ipo mkononi! Pia Rais aliahidi na kutoa nyumba ya Serikali kwa Wasanii ambayo ingetumika kuendeshea Studio husika, lakini nyumba hiyo ya Serikali iliyotolewa na Rais sasa iko chini yao na ndio makao ya THT! Wamefanikiwa kumhadaa Rais kuwa wao ndio “Care takers” wa Sanaa ya Tanzania akawaamini na wao wanaitumia vibaya imani njema ya Rais kwao kufanya dhuluma.

Yote niliyoyataja juu, japokuwa hayo ni kwa uchache tu! Yanalalamikiwa sana na wasanii wengi na wadau hapa nchini, japokuwa wengi wameshindwa kujitokeza waziwazi kutoka na vitisho vya watu hawa. Vitendo hivyo wanavyofanya vimeleta madhara katika tasnia ya sanaa na matokeo yake ni kudumaa kwa maendeleo ya muziki hapa nchini. Vijana wengi wanaojihusisha na sanaa wamepoteza matumaini. Wengi walipata tegemeo la ajira kupitia muziki, lakini hali haipo hivyo tena. Vijana wengi wasanii wamekata tamaa kwa ajili ya ukandamizaji wa “empire” hii.

Na sio tu wasanii na wadau wengine wanawapoteza katika hili. Kwa watu hawa kuhodhi na kuvuruga kabisa biashara ya muziki, hata Serikali inapoteza fedha nyingi kupitia kodi. Kwa mujibu wa utafiti wa Dr. Jehovaness Aikaeli ambaye ni mchumi wa UDSM, hata katika hali hii mbaya ya biashara ya muziki, Serikali imepoteza Tsh. Milioni 18, kwa kutokusanya kodi kupitia muziki tu, ukiachilia mbali filamu na sanaa nyingine. Na iwapo hali itaboreshwa basi kodi hiyo itapanda mpaka wastani wa Tshs. Bilioni 50 kwa mwaka! Hizi sio pesa kidogo kwaserikali, hasa ukizingatia bajeti ya Wizara inayohusika na Utamadnuni ni Tsh bilioni 14, kwa mwaka, fedha ambazo mara nyingi hawapewi zote kutokana na Serikali kutokuwa na fedha ya kutosha! Lakini hapa utaona kukwa kodi ya mwaka peke yake ingetosha kwa bajeti ya Wizara na ziada kubwa ingebaki kwa miradi ya maendeleo kama kujenga Art Theatres n.k.

Napenda ieleweke wazi kwamba mimi binafsi ni “Mhanga” au “victim” wa uharamia wa “himaya” hii kwa miaka mingi, tukupitia migogoro kadhaa ya kibiashara lakini kilichonisikuma kuchukua hatua hii; sio nafsi yangu pekee bali wajibu nilionao hivi sasa kama mwakilishi umma.Izingatiwe kuwa baada ya mimi kuchaguliwa kuwa Mbunge na wananchi wa Mbeya tena kwa kishindo, Serikali kupitia Wizara inayohusika na utamaduni na pia Baraza la Sanaa (BASATA), walinipongeza kwa barua huku wakinitaka niendelee na harakati za kupigania sanaa na wasanii kwa kutumia nafsi au jukwaa langu jipya Bungeni na nje ya Bunge. Jukumu ambalo nililikubali kwa mikono miwili kwani harakati za muziki huu si kitu kipya kwangu, ulianza kabla ya Ubunge na ndio ninachokifanya na hasa ukizingatia mimi pia sasa ni Waziri Kivuli (Shadow Minister) wa Wizara ya Habari, Vijana na Michezo.

Kwa lugha nyingine ujumbe nilioutoa wa kukataa Fiesta ni ishara ya mgomo wenye nia ya kutuma ujumbe wa madai ya msingi. Na historia inaonyesha kuwa, Wasanii wa Nigeria walianza kulipwa vizuri kama wanavyolipwa sasa baada ya kuanzisha migomo dhidi ya mapromota wanyonyaji wa nchini kwao.Na kama ni suala la kukuza uchumi na ajira, Ni nini mchango wa Fiesta na matamasha mengine kwa halmashauri za mji na majiji wanayopita na kuvuna mamilioni ya fedha kila siku?
Wenu katika kutaka haki,
Joseph Mbilinyi (Mb)
9/7/2011-Mbeya Mjini

Thursday, July 7, 2011

DPP aomba ushahidi wa Dr.Slaa Dhidi ya Chenge.

Dr.wilbord slaa
Imeripotiwa katika gazeti la Mwananchikwamba; MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amemtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, kuwasilisha nyaraka zenye ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa rada  serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi.Feleshi aliliambia gazeti hili jana kuwa ofisi yake inayo sehemu ya ushahidi wa suala hilo, lakini hautoshi kumtia Chenge hatiani kama atafikishwa mahakamani."Kama Chadema wanao (ushahidi), kama alivyoeleza Dk Slaa, walete tutaulinganisha na ushahidi tulionao ili tuone kama unatosha kuitetea kesi hiyo mahakamani," alisema Feleshi.

Kwa mujibu wa Feleshi kuna uwezekano wa nyaraka alizonazo Dk Slaa kuwa na ushahidi unaotofautiana na ushahidi uliopo serikalini hivyo kuwasilisha nyaraka hizo, kutasaidia kufanikisha jambo hilo.

“Sheria zetu zina utaratibu mzuri wa kupokea ushahidi. Sheria ya Mwenendo wa Kesi na Makosa ya Jinai, kifungu cha Saba na ile ya kupambana na rushwa, kifungu cha 39, zinaeleza bayana kuwa mtu mwenye ushahidi anaweza kuuwasilisha kwenye vyombo vinavyohusika,” alisema Feleshi.

Feleshi alitoa kauli hiyo jana alipokua akihojiwa na gazeti hilo kuzungumzia kauli ya Dk Slaa aliyoitoa juzi kuwa Serikali ina ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa rada ila imeamua kuwalinda.“Waupeleke serikalini ushahidi huo kama wanao ili ukalinganishwe, inawezekana ukawa tofauti na uliopo, hivyo kufanikisha kuwachukuliwa hatua watuhumiwa, hakuna mtu anayefurahia suala hilo,” alisema Feleshi.

Hata hivyo, Feleshi alibainisha kuwa ushahidi pekee hauwezi kumtia mtu hatiani isipokuwa ushahidi unaoweza kuithibitishia mahakama kuwa mshtakiwa ametenda kosa.Alisema ni vema Chadema na watu wengine wanaodai kuwa wana ushahidi wa kutosha kuhusu ushiriki wa Chenge kwenye ufisadi wa rada wauwasilisha serikalini ili ufanyiwe kazi badala ya kulalamika nje ya utaratibu.

Kauli ya Mwanasheria Mkuu
Kauli hiyo ya DPP imeungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema, aliyesema kuwa nyaraka alizo nazo Dk Slaa kuhusu watuhumiwa wa rada zipo pia ofisini kwake, lakini hazina ushahidi wa kutosha kumtia Chenge hatiani.

Hata hivyo akinukuu Katiba ya nchi, Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali alisema ofisi yake siyo ya mwendesha mashtaka, hivyo haina mamlaka kuwashtaki watuhumiwa.

“Kuna mtu anayehusika na kazi hiyo, mimi siyo prosecutor (mwendesha mashtaka). Lakini uchunguzi ulifanyika na kuonekana kuwa ushahidi hautoshi kumtia Chenge hatiani,” alisema Werema na kuongeza:

“Ungekuwa karibu tungeangalia Katiba na tungesoma Ibara ya 59 Sehemu ya Kwanza, Tano hadi 60. Yupo mtu wa kufanya kazi hiyo ya uchunguzi.”Ibara ya 59 ya Katiba, Sehemu ya Tatu inaeleza kazi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni kuishauri serikali juu ya mambo ya sheria na kwamba, yeye ndiye atakayeshughulikia mambo yote yahusuyo sheria yatakayopelekwa kwake au kazi atakazoagizwa na Rais na nyingine zinazokabidhiwa kwake kwa mujibu wa katiba.

Katiba imeeleza kuwa mwenye mamlaka ya kuendesha mashtaka ni Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na anafanya kazi hiyo akiwa huru bila kuingiliwa na mtu ama mamlaka yoyote.

Katiba inamtaja Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai katika Ibara ya 59(b), Sehemu ya Nne kuwa katika kazi zake hataingiliwa na mtu yeyote wala mamlaka yoyote na atafanya kazi kwa kuzingiatia nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.Kazi zake ni kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini.

Juzi ikiwa ni siku moja baada ya Serikali kumkingia kifua Mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge, ili asishtakiwe kwa rushwa katika mchakato wa ununuzi ya rada, Chadema imeweka hadharani kurasa 11 za ushahidi inaodai kuwa unaweza kumtia hatiani Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani kama atashtakiwa.

Ushahidi huo uliotolewa na Dk Slaa, ni ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Shirika la Upelelezi la Makosa Makubwa ya  Jinai la Nchini Uingereza (SFO).

Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa amefikia hatua hiyo baada ya kusikitishwa na majibu ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, kuhusu suala hilo alipokuwa akijibu hoja za wabunge.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, ukurasa wa tano wa ripoti hiyo, unaeleza jinsi Chenge alivyoshinikiza utekelezwaji wa mkataba huo na jinsi alivyofaidika kwa malipo ya kitita cha Dolaza Marekani 1.5 milioni kupitia akaunti ya Benki ya Barclays iliyoko katika kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.

"Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kati ya mwaka 1995 na 2006. Katika kipindi hicho, BAE na SPS walikuwa wakifanya majadiliano ya ununuzi wa rada kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na Chenge alihusika moja kwa moja katika mchakato huo hasa kushinikiza ununuzi huo," alisema Dk Slaa akinukuu waraka huo alioutoa pia kwa waandishi wa habari.

Aliendelea,"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitakiwa kutoa maoni na kuthibitisha malipo hayo na bila Chenge kukubali, kusingeweza kufanyika chochote."

Kwa mujibu wa Dk Slaa, kauli ya Waziri Chikawe kuwa Serikali haina ushahidi unaowataja watuhumiwa wa kashfa ya rada moja kwa moja na kutaka mwenye ushahidi wauwasilishe kwake, ni hatari kwa kuwa inaonyesha kuwa haina dhamira ya kweli ya kushughulikia rushwa na ufisadi huo.

Alisema ripoti hiyo ya SFO, ambayo anaamini Serikali inayo, ni ushahidi tosha unaoweza kumtia hatiani Chenge ambaye pia angeweza kusaidia kutaja wahusika wengine katika sakata hilo.

Kauli ya Dk Hoseah
Katika katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hosea, alisema taratibu za kuwasilisha ushahidi ofisini kwake ziko wazi, hivyo kumtaka Dk Slaa kuuwasilisha kwake ili akaufanyie kazi.

 
Dk Hosea alisema Ofisi yake inafanya kazi saa 24, lakini inahitaji ushahidi na ndio sababu Kifungu cha 39 cha Sheria ya kupambana na rushwa Takukuru kinamtaka mtu yeyote mwenye ushahidi juu ya masuala ya rushwa kuwasilisha hapo.

Kuhusu hatua ambazo ofisi yake inafanya kuhusu tuhuma za rada ambazo juzi Dk Slaa alidai ana ushahidi, alisema swali hilo aulizwe waziri (Chikawe).“Kwanini usimuulize waziri , yeye ndiye aliyetoa kauli hiyo (Statement) muulize huyo ndiye anaweza kuwa na majibu kuhusiana na hilo,” alisema Dk Hosea.

Alisema wao ni watendaji na si wanasiasa na kwamba, ofisi yake inafanya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria zilizopo.Alisema kama kunamtu mwenye ushahidi auwasilishe kwao nao wataufanyia kazi mara moja  kwa sababu  hiyo ndiyo kazi yao.Source Mwananchi magazine.

Wednesday, July 6, 2011

Wazuia maiti asizikwe, risasi zawatawanya

POLISI jijini Dar es Salaam jana ililazimika kutumia risasi kutawanya kundi la vijana lililovamia msikiti kuzuia mwili wa Bakari Hamisi aliyefariki juzi baada ya kuanguka wakati akicheza mpira katika viwanja vya Faru, Manzese, usizikwe.

Saa 7 mchana, mwili wa Hamis anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 25, ulishaandaliwa na kupelekwa msikitini kuswaliwa kabla ya kwenda kuuzikwa, lakini kundi la watu, wengi wao wakiwa vijana liliingilia kati na kwenda kufukia kaburi kushinikiza usizikwe.

Taarifa kutoka msibani zinasema, vijana hao wanadai kuwa kifo cha kijana huyo ni cha kutatanisha kutokana na madai kwamba, baadhi ya watu walimuona akitembea nje. “Wakati tukijiandaa kuswalia maiti hiyo, ndipo zikaanza tetesi kwamba marehemu ameonekana nje akitembea. Kauli hiyo ilianza kuenea miongoni mwa watu waliokuwa msibani, na hatimaye kujaa kila upande wa msikiti,” alisema ndugu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Baada ya kuibuka mzozo baina ya pande mbili zinazounga mkono azikwe na wengine wakipinga, polisi walifika msikitini hapo kutuliza vurugu.

Wakati baba wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Hamisi kutangaza kuwa mwili ukazikwe, kundi lingine lililokuwa likitaka asizikwe, lilikwenda moja kwa moja hadi makaburi ya Msikiti wa Jumuiya Manzese kwa Mfuga Mbwa na kufukia kaburi.

Polisi ilibidi wapige risasi hewani kwa ajili ya kutuliza vurugu katika eneo ulipo msikiti huo. Hata hivyo, waombolezaji hao walianza kuwarushia polisi chupa, mawe na vipande vya miti. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kuwepo tukio hilo. “Sasa hivi natoka safarini ila nitaelekea kwenye tukio,” alisema na kuongeza kwamba amewatuma polisi kwenda kuchunguza chanzo.

Alisema, ingawa amesikia, lakini chanzo hakijajulikana kama ni imani za kishirikina au ipo sababu nyingine. Polisi waliamua kuuchukua mwili na kuupakia kwenye gari na kuupeleka kwenye Hospitali ya Mwananyamala. Kijana huyo ambaye alianguka katika viwanja vya mpira vya Faru, vilivyopo karibu na Kituo cha Polisi Mpakani Manzese, alichukuliwa hadi nyumbani alikofia kabla ya kumpeleka hospitali.Chanzo Habari leo.

Diwani, wengine 5 wauawa.

Imeripotiwa katika gazeti la Habari leo, kwamba watu sita akiwamo Diwani wa Lagangabilili wilayani Bariadi mkoani Shinyanga, kupitia chama cha United Democratic (UDP), wameuawa kikatili katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea saa 2.30 usiku katika kijiji cha Ng’esha wilayani hapo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema ofisini kwake jana kuwa, watu sita wakiwa na pikipiki tatu na bunduki moja ya kienyeji inayotumia risasi za shotgun waliwashambulia diwani Simba Sita (45) na Nyebu Kadundu (60) ambaye alikufa papo hapo.

Sita baada ya kupigwa risasi alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza, lakini akiwa njiani alipoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi. Inadaiwa majambazi hao walifyatua risasi ovyo kutawanya wananchi waliokuwa wakipiga kelele za kuomba msaada.

Katika tukio hilo, baada ya majambazi hao kufyatua risasi kadhaa walipora Sh milioni moja za Mduhu Sita (35) alizopata baada ya kuuza ng’ombe mnadani siku hiyo, Sh 55,000 na simu ya mkononi aina ya Nokia.

Kwenye duka la Mongo Maduhu kijijini hapo, walipora bidhaa za dukani zikiwamo betri za tochi na bidhaa nyingine ambazo idadi na thamani yao halisi bado haijafahamika na kuondoka kwa pikipiki tatu walizokuwa nazo na moja waliyopora kwa Diwani Sita aina ya Lifan namba T 693 BCN.

Kwa mauaji hayo ya kikatili, wananchi walikusanyika na kupiga kelele za kuomba msaada huku wakiwafuatilia majambazi hao kwenye vijiji jirani vya Lagangabilili, Gambasingu, Ipilililo, Kisesa na Giriku.

Baada ya msako na ufuatiliaji wa haraka, wananchi kwa kushirikiana na Sungusungu waliwaona wakiwa na pikipiki nne katika kijiji cha Kisesa, Meatu umbali wa kilometa saba kutoka eneo la tukio na wananchi kuwashambulia kwa mawe na marungu.

Kamanda Kamugisha alisema katika purukushani hiyo majambazi waliwaponyoka wananchi na kutelekeza pikipiki nne; namba T 664 BEQ, T 530 BDQ, T833 BFV zote aina ya Sunlag na namba T 693 BCN ya marehemu Diwani.

“Wananchi waliendelea kuwafuatilia majambazi hao huku wakiwashambulia kwa silaha za jadi na kusababisha vifo vya wanne na kufanya idadi ya waliouawa katika tukio hilo, kuwa sita hadi leo (jana),’’ alisema Kamugisha.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Nzungu Cherehani (50) mkulima wa kijiji cha Bukundi, Meatu; Sospeter James (40) wa mtaa wa Sima, Bariadi; Manjale Ngimba (40) mkulima wa kijiji cha Inalo, Bariadi na Jeremia Ntembe (35), mkazi wa kijiji cha Budalabujiga na Ng’esha, Bariadi, aliyeuawa jana na mwili wake kuteketezwa kwa moto. Kamugisha alisema, polisi wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.

Breaking newzzz......Hali ya hewa yachafuka mwanza!Risasi za moto zatumika.


Hali ya jiji la mwanza leo hii imechafuka baada ya polisi kupambana na machinga waliotakiwa kutolewa katika maeneo kadha wa kadha katikati ya jiji. Habari zilizoifikia blog hii ni kwamba takriban watu watatu wameuawa katika sakata hilo, maduka kuvamiwa na vibaya na mali kuporwa ikiwemo magari yaliyo katika maeneo ya karibu kuharibiwa vibaya.
Jamaa akijiandaa kurusha jiwe

Umati katikati ya hekaheka

Vibanda vimevunjwa, Baadhi ya bidhaa zilizopangwa nje zimeibiwa nayo matairi yamechomwa katikati ya njia panda kuingia mtaa wa Makoroboi kuelekea Soko kuu na kiunganishi cha barabara ya Lumumba Mwanza huku baadhi ya wamachinga hao wakirusha maboksi yaliyoshika moto kwenye majengo yaliyo karibu na eneo hilo.kamanda wa Polisi hakuweza kupatikana kuelezea vurumai izo.



Tuesday, July 5, 2011

Msaada kizimbani: Nyumba yetu imepata mbia, Tufanyaje??

Habari yako, mimi nilikua nataka kukuuliza suala moja kuhusu mirathi, mimi na family members wenzangu tulikua na mzee wetu ambaye aliingia mkataba na kampuni za ujanja ujanja ili kujengewa nyumba kwa mgao wa asiliamia 30 kwa 70. kwa bahati mbaya Mzee wetu amefariki na sisi baada ya kufungua mirathi tulivyofika kwenye hatua hizo za mirathi ndipo tulipogundua marehemu mzee wetu aliingia kwenye Mkataba huo usiokua na maslahi kwetu. Katika huo Mkataba na masuala yote hayo marehemu mzee wetu hakuwahi kumshirikisha mtoto wake yeyote na pia baada ya Mzee kufariki hatukuwahi kuona karatasi zozote juu ya suala hilo.

Tulipokua kwenye harakati za mirsthi ndipo tulipopewa hati ya ubia baina ya marehemu mzee wetu na kampuni hiyo.Kwamba nyumba yetu ya kawaida itajengwa ghorofa na kwa makubaiano ya asilimia 70 kwa 30.Je sisi tunayohaki ya kuanza nae upya mazungumzo kuhusu mkataba maana bado ipo vile vile huyo mshirika hajaongeza chochote kwenye nyumba mpaka sasa hivi, asante nategemea ushauri wako. Mr.B

Monday, July 4, 2011

Ujambazi waitikisa Zanzibar.

Watu wawili wameuawa kwa kucharangwa mapanga na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi baada ya kuvamia hoteli ya kitalii ya Mbweni Ruins, iliyoko nje kidogo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi majira ya alfajiri na kuwataja waliouawa kuwa ni dereva wa hoteli hiyo, Pius Paulo na mlinzi, Abdalla Simba.

Kamanda Juma alisema dereva huyo alikufa papo hapo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kucharangwa kwa mapanga kichwani na Mlinzi huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambako alikimbizwa kwa matibabu.Alisema mlinzi mwingine wa hoteli hiyo, Said Abdalla, anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo kutokana na majeraha aliyoyapata kwa kucharangwa kwa mapanga na majambazi hayo.

Alisema majambazi hayo ambayo yalikuwa na silaha za kienyeji baada ya kuvamia hoteli hiyo na kufanya mauaji hayo yaliiba kompyuta tatu ikiwemo moja ndogo (laptop) na kubwa mbili na fedha taslim zinazokadiriwa kufikia sh. 104,000 Alisema baada ya majambazi hayo kufanya uvamizi huo, walinzi walijaribu kupambana nao, lakini walizidiwa. Katika tukio hilo hakuna mgeni aliyejeruhiwa.Kamanda huyo alisisitiza kuwa polisi wanaendelea kuyasaka majambazi hayo na kuwaomba wananchi kulisaidia jeshi hilo kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaowatilia mashaka katika maeneo yao.

Habazi zaidi zinadai kuwa dereva huyo amezikwa kijijini kwao Kizimbani katika Wilaya ya Magharibi Unguja na mlinzi makaburi ya Mwanakwerekwe. Habari zinaeleza kuwa baada ya majambazi hao kumcharanga mapanga Pius kichwani pia walimvua nguo zote alizokuwa amevaa na kumchoma na vitu vyenye ncha kali katika baadhi ya maeneo ya mwili wake.

Kwa upande wao wafanyakazi wa hoteli hiyo, walisema dereva huyo alilala hotelini hapo ili kuwahi kuwapeleka uwanja wa ndege watalii kwa ajili ya kurudi nchini kwao." Tukio hili ni la pili kwa hoteli yetu kuvamiwa na majambazi. Kwa mara ya kwanza tukio kama hili lilitokea mwaka 2001, lakini hakuuawa mtu,” alisema mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo.

Mfanyakazi huyo ambaye alikataa kutaja jina lake alidai wamesikitishwa na huduma duni katika chumba cha wagonjwa mahatuti cha Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.Hospitali hiyo inakabiliwa na hali mbaya baada ya mashine zote tano za kusaidia wagonjwa mahatuti kuharibika kwa zaidi ya mwaka mmoja na kusababisha madaktari kutumia mitungi ya oxygen.Wafanyakazi wengi wa hoteli za kitalii Zanzibar wameshauri vyombo vya dola kuimarisha ulinzi katika miradi ya kitalii hasa wakati huu wa msimu wa utalii unaoendelea Zanzibar. source IPP.