Powered By Blogger

Sunday, November 27, 2011

Babu '67' afungwa kwa Kunyofoa kidole cha Mkewe.

MZEE Juma Iboma (67) wa kijiji cha Msisi tarafa ya Mtinko huko Singida, amehukumiwa kutumikia adhabu ya miezi mitatu jela, baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh 70,000 kwa kosa la kumng’ata mkewe kidole cha mkono na kukinyofoa.

Mzee huyo, alipewa adhabu hiyo majuzi na Mahakama ya Mwanzo Utemini mjini hapa. Awali ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa Iboma alitenda kosa hilo baada ya kuchukizwa na kitendo cha mkewe, Hawa Wawa (63), kumpa paka makande bila ruhusa yake.


Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Ferdinard Njau, alisema upande wa mashitaka ulithibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alifanya kitendo hicho na hivyo kumwona ana hatia.


"Baada ya Mahakama hii kukutia hatiani, unapewa adhabu ya kulipa faini ya Sh 20,000 na fidia kwa mlalamikaji ya Sh 50,000.


“Ni lazima uanze kulipa fidia kwanza, ukishindwa kulipa faini na fidia, utakwenda jela miezi mitatu," alisema Hakimu Njau. Mshitakiwa hakuweza kulipa faini wala fidia, hivyo kulazimika kwenda jela miezi mitatu ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wanaonyanyasa wake zao.


Hakimu Njau alipomwuliza Hawa, kama yuko tayari kurudiana na mumewe, alikataa kata kata akidai kuwa amechoka kung’atwa mara kwa mara na mumewe huyo. Chanz Habari leo.

No comments: