Powered By Blogger

Tuesday, January 31, 2012

TANZANIA KUJENGA MAHAKAMA YA HAKI ZA BINADAMU

Rais Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania itagharamia ujenzi wa Makao Makuu ya kudumu ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika – African Court on Human and Peoples Rights (ACHPR) mjini Arusha.

Aidha, Rais Kikwete amesema Tanzania inaunga mkono mageuzi yanayokusudiwa kufanywa kwenye muundo wa Mahakama hiyo ili kuiwezesha kuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuzitolewa maamuzi kesi za makosa ya jinai sawa na mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ya mjini The Hague, Uholanzi.


Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Majaji wa Mahakama hiyo ya ACHPR wakiongozwa na Rais wake, Jaji Gerald Niyungeko kwenye Hoteli ya Sheraton, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Rais Kikwete alikuwa Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika Jumatatu usiku.


Majaji wengine walioambana na Jaji Niyungeko kukutana na Rais Kikwete ni Jaji Sophia Akuffo ambaye ni Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Elsie Nwanuri na Msajili wa Mahakama hiyo, Dk. Robert Eno.


Rais Kikwete amewaambia majaji hao kuwa ni vyema wakati wanafanya maandalizi ya michoro ya jengo la Makao Mkuu ya Mahakama hiyo wakumbuke kuwa hiyo itakuwa ni Mahakama ya Bara zima na wala siyo ya Tanzania na hivyo wafikirie jengo zuri na lenye hadhi inayostahili Mahakama ya Bara la Afrika.


“Kwa kweli tunataka kujenga jengo kubwa na zuri la kuwa Makao Makuu ya Mahakama yetu hii. Tunataka kujenga Mahakama ya Afrika. Kwa hiyo katika michoro yenu zingatieni jambo hilo kwa sababu tunataka jengo la hadhi,” Rais Kikwete aliwaambia majaji hao.


Ameongeza: “Nyie hangaikeni na michoro mizuri kwa ajili ya jengo lenye hadhi. Habari za fedha za kujenga jengo hilo tuachieni sisi katika Serikali kuona tutafanya vipi.”


Rais pia ameahidi kuwa Serikali itaongeza kasi ya kutafuta ardhi za ujenzi wa mahakama hiyo. Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa AU uliomalizika juzi umebariki makao makuu ya Mahakama hiyo kuwa mjini Arusha.


Jaji Niyungeko alitumia fursa hiyo kumweleza Rais kuhusu shughuli za Mahakama hiyo na kuishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuunga mkono shughuli za Mahakama hiyo.


Alimueleza Rais Kikwete kuwa Mahakama hiyo sasa imeanza kupokea kesi nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Alisema mwaka jana peke yake, ilipokea kesi 14, ikiwemo moja kutoka Tanzania, na maombi mawili ya kuitaka kutoa ushauri wa kisheria. Alisema kati ya kesi hizo, tayari kesi saba zilikwishakuamuliwa.
Chanzo Habari leo.