Tuesday, February 19, 2013

MAHAKAMA KUU KANDA YA MWANZA YAPIGA STOP UCHAGUZI WA TFF.

Jaji wa Mahakama kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Jaji Mruma hivi punde amepiga stop uchaguzi wa TFF usifanyike mpaka pale kesi ya msingi iliyofungukiwa na Bwana Richard Julius Rukambura dhidi ya Tanzania football federation, shauri namba 1 ya mwaka 2013.

Katika shauri hilo Mlalamikaji Richard Julius Rukambura alijiwakilisha yeye mwenyewe na Mlalamikiwa yaan TFF, aliwakilishwa na Wakili Maaarufu Bwana Mgongolwa.  Aidha Mheshimiwa jaji aliwaamu

Wednesday, February 6, 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAJI MFAWIDHI(KANDA YA MWANZA) KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI (LAW DAY), 2013
Mhe. Mkuu wa Mkoa,

Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu,
Mheshimiwa Jaji Mstaafu, Jaji Nchalla,
Mhe. Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu, Mwanza,
Mhe. Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara,
Mhe. Wakili wa Serikali Mfawidhi, Mwanza,
Mhe. Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tawi la Mwanza,
Wah. Wastahiki Meya – Nyamagana/Ilemela,
Wah. Wakuu wa Wilaya – Nyamagana/Ilemela,
Wah. Mahakimu wa ngazi zote na Wasaidizi wote wa Sheria wa Majaji,
Wah. Mawakili wote wa Serikali na Kujitegemea,
Wah. Makamanda wa vyombo vya Ulinzi, Magereza na Usalama wa Mkoa,
Wah. Viongozi  wa Dini na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali mliopo,
Wah. Viongozi wote wa Vyama vya Siasa,
Watumishi wote wa Mahakama wa ngazi zote,
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Itifaki imezingatiwa.

Wageni waalikwa mabibi na mabwana, awali ya yote napenda kuwatakia wote heri ya mwaka mpya wa 2013. Aidha nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa kujumuika nasi katika sherehe hizi za Siku ya Sheria ambayo ndio kiashiria cha kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama mwaka huu. Najua mmeacha shughuli zenu za kawaida ili kujumuika nasi kufanikisha sherehe hii. Nasema asanteni sana na karibuni sana.                            

Wageni waalikwa mabibi na mabwana Maudhui ya Siku ya Sheria ya mwaka huu ni “Utawala wa sheria; Umuhimu na uimarishaji wake nchini”.


1.0       DHANA YA UTAWALA WA SHERIA
Hakuna tafsiri ya moja kwa moja ya maana ya utawala wa sheria, kwani kihistoria  dhana ya utawala wa sheria ilianza zamani sana, na imepata tafsiri tofauti kulingana na maendeleo katika Jamii. Wanazuoni na wanafalsafa maarufu duniani, kama Aristotle, Dicey na John Locke na wengineo wengi wamejaribu kutoa tafsiri tofauti tofauti juu ya utawala wa sheria, lakini  tafsiri isiyo rasmi ya dhana nzima ya utawala wa sheria yaani “Rule of law “-  ni ule utawala wenye kuheshimu usawa, uhuru wa watu, haki za binadamu pamoja na usawa mbele ya sheria.    

1.1        MISINGI YA UTAWALA WA SHERIA
Wageni waalikwa mabibi na mabwana,
Ipo misingi mbalimbali ya utawala wa sheria, ambayo jamii yoyote iliyostaarabika duniani sharti iifuate, misingi hii ndio chimbuko la maendeleo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni  katika jamii. Misingi hii ni kama ifuatayo:-
(i)   Usawa mbele ya Sheria yaani “Equality before the Law”, Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
(ii)  Haki za binadamu, jamii itahesabika kufuata utawala wa sheria pale ambapo itazingatia na kuheshimu haki za binadamu. Haki hizi ni pamoja na haki ya kuishi, haki ya kuabudu, haki ya kusikilizwa, haki ya faragha na usalama wa mtu na nyinginezo nyingi kama zilivyoainishwa katika sehemu ya Tatu ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
(iii)Uhuru wa Mahakama- dhana ya utawala  wa sheria haiwezi kuwa timilifu kama Mahakama zetu nchini hazitakuwa huru.  Dhana ya uhuru wa Mahakama imebainishwa wazi katika Ibara ya 107B ya Katiba yetu ya 1977 tuliyonayo hivi sasa. Ibara hii inasema kuwa katika
kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi”.

Ibara hii ndio chimbuko la uhuru wa mahakama Tanzania. Ni vema nikagusia walau kwa muhtasari, sana kuhusu dhana hii ya uhuru wa Mahakama.
Moja, mahakama ni mhimili wa dola kati ya mihimili mitatu iliyopo. Mhimili huu unatakiwa uwe huru na mihimili mingine yaani Serikali na Bunge haipaswi kuingilia uhuru huu kwa hali yoyote. Na siyo mihimili hii tu hata asasi za kitaifa wala mtu yeyote hapaswi kuingilia uhuru huu. Uhuru huu wa mahakama, kama papa avumavyo baharini, ndio unaovuma sana na pengine unakera pia. Imejitokeza mara nyingi watendaji wa serikali kuingilia maofisa wa mahakama katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Ipo mifano mingi sana,
mfano mojawapo ni ule wa kesi ya Jamhuri dhidi ya Iddi Mtegule iliyotokea huko Dodoma. Katika kesi hii vita ilikuwa kati ya Hakimu  Mahakama ya Mwanzo na Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma. Hakimu katika kutekeleza   kazi yake alimwachia huru mshtakiwa ambaye alikuwa ameshitakiwa kwa kuuza maandazi. 

Mkuu wa Wilaya alikasirika kwa mtu huyo kuachiwa huru kwa kuwa alikuwa amepiga marufuku uuzaji wa vyakula ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu kilichokuwa kimejitokeza wakati huo, hivyo aliamua  kuandika barua kali kwa Hakimu akimuonya kwamba ametoa  maamuzi ya upendeleo na majaribio ya makusudi kwa kuzuia juhudi za mamlaka kuondokana na kipindupindu. Alikwenda mbali zaidi ya hapo kwa kumtaka hakimu kueleza kwa nini alimwachia huru mshitakiwa na kutishia kuchukua hatua kali dhidi yake. Hakimu huyu aliyekuwa anaielewa vizuri misingi ya kazi yake  alijibu mara moja barua ya  Mkuu wa wilaya na kumueleza  kwamba alikuwa anaingilia huru wa mahakama. Alimweleza zaidi kwamba si kila mshitakiwa anatakiwa kuwa na hatia mpaka pale itakapothibitika vinginevyo.

Pili, mahakama inatakiwa iwe huru na wale wenye kesi mbele yake. Kila mwenye kesi asimwingilie  Jaji au Hakimu anayesikiliza shauri lake.

Tatu, mahakama inapaswa iwe huru na umma au sehemu ya umma. Hitaji hili nalo pia ni muhimu sana. Wananchi wanaweza wakaamini kuwa mshitakiwa ni mhalifu kumbe mahakama ikamwona siyo. Sasa mahakama isishinikizwe kumtia hatiani mtu ambaye hana hatia. Uhuru huu ni muhimu sana katika nyakati kama hizi za tuhuma zilizo kithiri za ufisadi ambapo baadhi ya wananchi tayari wamekwisha watia hatiani baadhi ya watuhumiwa hata kabla ya      kufikishwa mahakamani.

Nne, Majaji na Mahakimu wanatakiwa wawe na kinga katika kutekeleza majukumu yao. Katiba ya sasa haiwapi maofisa hawa wa Mahakama kinga katika maamuzi wanayofanya ya kusikiliza mashauri mbalimbali. Huu  ni mwiba mkali sana katika tasnia nzima ya upatikanaji wa haki nchini.

Tano, kuna uhuru binafsi wa kila Jaji au Hakimu. Uhuru huu hupatikana kwa kumthibitishia kila jaji na kila hakimu uhakika wa ajira yake. Jaji au hakimu ambaye ana wasiwasi na ajira yake na anahofu kuwa ajira inaweza kukatishwa wakati wowote na kwa sababu yoyote, hawezi kuwa thabiti katika kutekeleza majukumu yake ya utoaji haki chini ya Katiba. Hii ni pamoja na uhakika wa kupata mshahara na maslahi yake kila mwezi na kwa ukamilifu.

Pengine ni wakati muafaka niseme kwamba dhana ya uhuru wa mahakama haimaanishi mahakama kujitenga na taasisi nyingine za umma katika kulijenga taifa letu. Kumekuwepo mtazamo na uelewa tofauti kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wananchi walio wengi kwamba tunapozungumzia uhuru wa mahakama tunazungumzia utengano. Hii ni uelewa potofu. Uhuru wa mahakama kimsingi ni uhuru anaopaswa kuwa nao Jaji au Hakimu anapotekeleza majukumu yake ya utoaji haki na sii vinginevyo. Hivyo basi inatosha kusema dhana ya uhuru wa mahakama ni ndugu pacha na jukumu la mahakama la kikatiba la utoaji wa haki.  Mahakama huru ndio tegemeo kuu la Utawala wa Sheria.  Bila mahakama huru, Utawala wa Sheria utakuwa kama ndoto za alinacha.  Hata hivyo nitoe wito kwa Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kwamba, uhuru wa Mahakama unatudai tuwajibike kwa jamii, kwa kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati.  Tukifanya hivyo tutakuwa kichocheo cha amani, udugu na uhuru.  Lakini pia heshima ya Mahakama itapanda na imani ya Umma kwa Mahakama itaongezeka.

Wageni waalikwa mabibi na mabwana, msingi mwingine muhimu wa dhana ya utawala wa sheria ni Mgawanyiko wa Mihimili ya Dola, yaani separation of powers. Ibara ya 4 (1),(2),(3) na (4) ya Katiba yetu inaelezea mihimili mikuu mitatu ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Ili kulinda na kuenzi dhana nzima ya utawala wa sheria kama nilivyotangulia kusema, sharti mihimili hii isiingiliane katika kutekeleza majukumu ya ujenzi wa taifa letu.
1.2       UMUHIMU WA UTAWALA WA SHERIA NCHINI
Utawala wa sheria una umuhimu mkubwa sana nchini. Umuhimu wake kwa uchache ni kama ifuatavyo:-
1.    Ukuzaji wa demokrasia:- Iwapo dhana ya utawala wa sheria nchini utapewa umuhimu wake yamkini  kutaimarisha demokrasia iliyopo nchini, kutaimarisha na kudumisha amani na usalama kwa kila mwananchi. Kuheshimu utawala wa sheria kutawawezesha wananchi kujikita kwenye shughuli za maendeleo ya nchi.
Si vibaya nikasema wazi kuwa matukio mbalimbali tunayoyaona na kusikia hivi sasa kama migongano ya vyama vya siasa, migongano ya itikadi za kidini na maandamano yasiyoisha yanatokana na kutokutii utawala wa sheria na kutoitumia demokrasia tuliyonayo kwa ustaarabu.
2.   Uimarishaji wa Utawala bora:- Utawala wa sheria ni muhimu kwa kuwa hupelekea utawala bora. Kwa kufuata misingi ya utawala wa sheria Taasisi mbalimbali za kiserikali na idara zake zitachochea misingi iliyotukuka ya utawala bora.
3.   Upatikanaji wa haki:- Iwapo misingi ya utawala wa sheria itaheshimiwa na kuimarishwa ipasavyo jamii itapata haki inayostahili.  Watu wengi wamepoteza haki zao na wengine kukumbwa na mauti kutokana na wanajamii kutokutii utawala wa sheria.
4.  Utawala wa sheria kama kichocheo cha maendeleo:- Maendeleo yoyote katika jamii  yawe ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni hayawezi kupatikana kama utawala wa sheria utawekwa kapuni. Iwapo jamii itaheshimu dhana ya utawala wa sheria maendeleo yatapatikana kwa kasi kubwa.
2.0       HALI HALISI YA UTEKELEZAJI WA UTAWALA WA SHERIA NCHINI
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana, utekelezaji wa dhana ya utawala wa sheria nchini unakabiliwa na matatizo lukuki na changamoto mbalimbali. Baadhi ya matatizo na changamoto hizi ni kama zifuatavyo:-
1.   Jamii kujichukulia sheria Mikononi,yaani “Mob Justice”, baadhi ya wananchi kwa kushindwa kuheshimu misingi ya utawala wa sheria, wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi, pale wanapokamata mtuhumiwa wa uhalifu. Hii kwa kiasi kikubwa hukinzana na misingi ya utawala wa sheria iliyobainishwa katika Katiba yetu. Kwa mfano Ripoti ya Mwaka 2011 ya Kituo cha Haki za binadamu, inaonesha ya kwamba mnamo mwaka 2011 idadi ya watu 673 waliuawa nchini kote kwa aidha kuchomwa moto na au kupigwa kwa kutuhumiwa kutenda makosa mbalimbali. Takwimu zinaonesha ya kwamba mikoa mitatu iliyoongoza kwa mauaji hayo ni Dar- watu 157, Mbeya watu 89 na Mwanza watu 84 pia mikoa mitatu iliyokuwa na mauaji kiasi ni mikoa ya Singida watu 5, Arusha watu 4 na Dodoma watu 3.
Ni wito wangu kwa wananchi na hasa vijana ambao ndio taifa na viongozi wa kesho kuacha kabisa kujichukulia sheria mkononi. Tudumishe amani, upendo na utulivu kwa kuheshimu utawala wa sheria.
2.   Rushwa:- Rushwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa utawala wa sheria nchini. Hayati baba wa Taifa wakati akilihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 12 Oktoba, 1965 alisema “rushwa huzuia haki, na kama ikiruhusiwa kuenea itaangamiza taifa letu.  Haki inapouzwa na kununuliwa, matumaini ya jamii yanapotea.  Nitoe wito na kuwakumbusha Majaji na Mahakimu kwamba huwezi ukapokea rushwa ukabaki kuwa mwaminifu kwa kiapo cha Ujaji/Uhakimu. Yeyote anayepokea rushwa hupoteza uhuru wake na anabakia kuwa mtumwa wa kudumu.  Hata hivyo kuna wimbi la watumishi wa Mahakama wengine kuacha Majaji na Mahakimu kudai rushwa tena kwa kutumia majina ya Majaji na Mahakimu visivyo.  Hili ni baya zaidi na linahatarisha usalama wa Majaji na Mahakimu.  Nichukue fursa hii kulikemea kwa nguvu na niwatake wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
3.   Kuingiliwa kwa uhuru wa Mahakama:- Kama nilivyoeleza hapo awali serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikiingilia uhuru wa Mahakama. Vyombo vya habari halikadhalika mara nyingi vimekuwa vikiingilia uhuru wa Mahakama kwa kutoa taarifa za mashauri ambayo hayajamalizika mahakamani. Kumekuwepo uhaba wa rasilimali watu na fedha. Vyote hivi vinapelekea kuingiliwa kwa uhuru wa mahakama kwa njia moja au nyingine.  Iwapo Mahakama haitakua huru haki haitaonekana kutendeka.  Katika shauri maarufu la Ally Juuyawatu dhidi ya Loserian Mollel & Mwenzake [1979] L.R.T. 6. Mhe. Jaji Edward Mwesiumo (kama alivyokuwa) alivamiwa ofisini kwake kutokana na maelekezo ya “bwana mkubwa”,  na faili la kesi aliyokuwa akisikiliza kuchukuliwa kwa nguvu. Lakini siku chache baadae faili hilo lilirudishwa na alipewa barua. Hata hivyo kutokana na kuingiliwa  na watendaji wa serikali Mheshimiwa Jaji aliamua kujitoa kusikiliza shauri hilo.
Lakini pia wakati mwingine hata Katiba yetu yenyewe, inazuia mahakama isifanye kazi yake kwa ufasaha, kwa mfano Ibara ya 7(2) inasema kwamba, nanukuhu “Masharti ya Sehemu hii ya Sura hii hayatatiliwa nguvu ya kisheria na Mahakama yoyote. Mahakama yoyote nchini haitakuwa na uwezo wa kuamua juu ya suala kama kutenda au kukosa kutenda jambo kwa mtu au mahakama yoyote, au kama sheria, au hukumu yoyote, inaambatana na masharti ya Sehemu hii ya Sura hii’’.  Sehemu hii inahusu “malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali”. Hili  ni hatari kubwa sana kwa dhana ya utawala wa sheria nchini hususani katika msingi wa Uhuru wa Mahakama.
Wageni waalikwa mabibi na mabwana, ili kuondokana na changamoto hizi ni rai yangu kwamba yafuatayo yafanyike:-
a.     Elimu juu ya utawala wa sheria itolewe:- Napenda kutumia fursa hii kulipongeza jeshi la polisi kwa kujitahidi kuelimisha umma juu ya utii wa utawala wa sheria katika vipindi mbalimbali vya Radio na Televisheni chini ya kauli mbiu yao “ utii wa sheria bila shurti”. Hizi ni jitihada nzuri zinazotakiwa kuungwa mkono na taasisi nyingine za serikali.
b.      Mabadiliko ya Katiba:- Naelewa kwamba hivi sasa tuko kwenye mchakato kabambe wa kuwa na Katiba mpya. Ni rai yangu kwa wananchi wote kuhakikisha wanachangia maoni yao kwani mabadiliko haya yataleta mageuzi makubwa katika misingi mbalimbali juu ya suala zima la utawala wa sheria nchini.
c.      Uboreshwaji wa Mhimili wa Mahakama, kimiundombinu na stahili za wafanyakazi:-  Miundo mbinu ya Mahakama zetu sio rafiki na wahitaji wote wa haki na hata kwa watoaji haki wenyewe.  Maslahi duni pia hufifisha hamu ya kufanya kazi kwa bidii.
d.    Kurekebishwa kwa sheria kandamizi:- Sheria kandamizi zinaondoa dhana ya kuleta haki kwa watanzania wote mbele ya sheria. Sambamba na uwepo wa Katiba mpya ni dhahiri kwamba sheria kandamizi zinapaswa kufanyiwa marekebisho, kama siyo kufutwa kabisa.  
e.      Uzingatiaji wa dhana ya mgawanyo wa madaraka katika utekelezaji wa shughuli za serikali nchini, nk.
f.     Kutoa kipaumbele kwa makundi yaliyo pembezoni, ili makundi hayo nayo yaweze kufaidi keki ya taifa” national cake” kama yalivyo makundi mengine.
3.0       MWISHO
Wageni waalikwa mabibi na mabwana napenda kuhitimisha kwa kusema kwamba hakikisho la kuwepo haki sawa kwa wote  katika nchi yetu ni uwepo wa Utawala wa Sheria.  Kama nilivyojitahidi kuonyesha hapo juu, msingi mkuu wa Utawala wa Sheria ni uwepo wa Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wake bila woga, chuki wala upendeleo.  Kwa hiyo basi sote tudumishe Utawala wa Sheria.  Aidha nichukue fursa hii kuwaasa watanzania wenzangu kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, ili tupate Katiba nzuri tuitakayo kwa maendeleo ya nchi yetu nzuri na vizazi vijavyo.
Asanteni kwa kunisikiliza!!
Mungu ibariki Mahakama, Mungu ibariki Tanzania.

Wednesday, January 30, 2013

MCHUNGAJI EAGT APANDISHWA KIZIMBANIMchungaji wa kanisa la Evangelical Assemblies of God nchini EAGT Daniel Mwasumbi amefikishwa katika mahakama ya mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari jijini Mbeya.

Mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Mheshimiwa Gilbert Ndeuluwo, mchungaji Mwasumbi mwenye umri wa miaka 57 alisomewa mashitaka na kukana kutenda makosa hayo.

Akisoma maelezo Mwanasheria wa serikali Achilaus Mulisa alisema kati ya mwaka 2008 hadi 2011 mshitakiwa huyo alimbaka mwanafunzi Neema Benson mwenye umri wa miaka 17 kinyume  cha sheria za kanuni ya adhabu 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili E  pamoja na kanuni ya adhabu ya 131 iliyorekebishwa mwaka 2002.

Katika shitaka la pili mshitakiwa huyo anatuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi huyo katika kipindi hicho kinyume cha sheria ya elimu namba 25 ya mwaka 1978.Hata hivyo mshitakiwa alikana makosa yote yanayomkabili.Na kwa mujibu wa mwanasheria wa serikali upelelezi juu ya kesi hiyo umekamilika kwa ajili ya kuwaleta mbele ya mahakama mashahidi watatu.

Mshitakiwa aliachiwa huru kwa dhamana baada ya kudhaminiwa na mtu mmoja kwa thamani ya fedha taslimu shilingi milioni 2 na kesi hiyo imeahirishwa hadi jumatano ijayo Januari 30 mwaka huu ambapo itaanza kusikilizwa. Chanzo Sahara Media.