Powered By Blogger

Friday, November 18, 2011

Profesa Maina: Achaguliwa kuwa Mjumbe Kanisheni ya Sheria UN.

MHADHIRI Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina Peter, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Sheria za Kimataifa (ILC).

Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika mkutano uliofanyika juzi katika makao makuu yake, walipiga kura ya siri kuchagua wajumbe 34 kati ya 49 waliotakiwa kuingia katika Kamisheni hiyo.


Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Balozi Nassir Abdulaziz Al - Nasser alimtangaza Profesa Peter wa Tanzania, kuwa ni mmoja wa wagombea tisa kati ya 13 kutoka Afrika ambao walishinda na kuingia katika Kamisheni hiyo.


Profesa Peter alishinda uchaguzi huo, uliokuwa na ushindani mkubwa akichuana na wagombea wengine 13 wakiwamo mabalozi na watu mashuhuri kama aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Amos Wako.


Wagombea wengine mbali ya tisa wa Afrika, walikuwa ni wanane wa kundi la nchi za Asia, watatu kundi la Ulaya Mashariki, sita kundi la Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean na wanane wa Ulaya ya Magharibi na nchi zingine.


Profesa Peter, atakuwa mjumbe wa Kamisheni hiyo kwa miaka mitano kuanzia Januari 2012. Mbali ya Tanzania, wengine kutoka kundi la Afrika walioshinda ni wa Afrika Kusini, Misri, Msumbiji, Nigeria, Algeria, Kenya, Libya na Cameroon


Ushindi wa Profesa Peter ulitokana uthubutu, wasifu na weledi wake binafsi, uratibu na ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa Tanzania katika UN ambako, maofisa wake wakiongozwa na Balozi Ombeni Sefue, walifanya kazi kubwa na maandalizi mazuri ya kufanikisha uchaguzi huo.


Profesa Peter akiongozwa na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania katika UN anayehusika na Kamati ya Sita ya Masuala ya Sheria na Uchanguzi, alifanya kampeni kwa takribani wiki nzima akikutana na mabalozi na maofisa mbalimbali wa UN.

No comments: