Nimenunua nakala kutoka Gazeti la JAMHURI ambalo limeamua kutoa utetezi wa Lissu
neno kwa neno ili wasomaji waweze kujua kilichomo ndani ya Mhimili wa
Mahakama. Ninanukuu kilichoandikwa katika gazeti hilo.
Mbunge wa Singida Mashariki ambaye ni Msemaji wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, ametoa
ushahidi mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kuthibitisha
kile alichokisema bungeni Julai 13, mwaka huu kuhusu uteuzi wa majaji na sifa
zao. Katika ushahidi wake ameweza kuonyesha ni kwa namna gani - kwa nyakati
tofauti - marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekuwa wakivunja Katiba
kwa kuwaongeza muda na kuwateua majaji waliofikisha muda wa kustaafu kwa mujibu
wa sheria.
Kwenye orodha hiyo amewataja baadhi ya majaji wasiokuwa na
sifa ya kuwa majaji katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa akiwamo mmoja
aliyelazimisha kuingia darasani katika Chuo Kikuu Huria, ili aweze kupata
shahada ya sheria kama kwa mujibu wa Katiba. Wamo majaji wengine walioteuliwa
kushika nafasi hizo nyeti ilhali wakiwa wanakabiliwa na tuhuma nzito za rushwa
na ukiukaji wa maadili ya kazi wakiwa mahakimu na wanasheria.
Aidha, kuna
majaji amewataja wasiokuwa na uwezo wa kuandika hukumu, akitoa mfano wa jaji
mmoja aliyeshindwa kuifanya kazi hiyo kwa miaka minne, akanyang’anywa.
Aliyekabidhiwa baada yake aliifanya kazi hiyo ndani ya wiki tatu tu. Lissu
amewataja majaji wengine wagonjwa ambao tangu wateuliwe hawajawahi kusikiliza
kesi na kuzitolea hukumu.
UTANGULIZI
Julai 13, 2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha
Maoni yake kuhusu Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria
kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na mambo mengine, Maoni ya Kambi yalihusu
utaratibu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya
Tanzania.
Maoni ya Kambi yalizua mjadala mkubwa
ndani na nje ya Bunge huku wachangiaji wengi wakimtuhumu Msemaji wa Kambi kwa
“kuidhalilisha” Mahakama na/au “kuwadhalilisha majaji” (Gosbert Blandes-Karagwe
CCM); “kuwavunjia heshima majaji” (Naibu Spika Job Ndugai); kuwatukana na
kuwadhalilisha majaji (Murtaza Mangungu-Kilwa Kaskazini); “kuwa-offend,
kuwadhalilisha na kuwanyanyasa majaji” (Assumpter Mshama-Nkenge CCM);
“kufedhehesha Mahakama na majaji” (Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick
Werema).
Aidha, Msemaji wa Kambi alishambuliwa
kwa kudaiwa kuwa mfitini na asiye na akili timamu (Muhammad Chomboh- Magomeni
CCM)); na “kujiamini kwamba yeye anajua zaidi kuliko watu wengine wote”
(Mangungu). Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
alilihakikishia Bunge kwamba “... haijatokea hata siku moja katika nchi hii Rais
akamteua Jaji wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo yaliyopelekwa kwake na
hii Tume ya Uajiri wa Mahakama.” Zaidi ya hayo, “... labda Mheshimiwa Lissu
anamjua Jaji angalau mmoja na anaweza akamtaja aseme Jaji huyu ametolewa tu
mitaani na Mheshimiwa Rais, yupi hakuna… hawa majaji wote walioteuliwa wamepitia
mchakato huu wa kikao kizito sana cha watu ambao ndiyo wenye sheria ya nchi
hii.”
Baadaye Msemaji wa Kambi alitakiwa kufuta
kauli yake kuhusu uteuzi wa majaji usiofuata utaratibu uliowekwa na Katiba.
Msemaji wa Kambi alikataa kufuta kauli hiyo ambako Mwenyekiti wa Kikao
alielekeza Msemaji wa Kambi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge kwa hatua zaidi. Alichukua uamuzi huo ili masuala hayo yapatiwe
ufafanuzi ili wananchi wapate picha kamili na ya kweli kuhusu jambo hili muhimu.
Maelezo haya yana lengo la kutoa ufafanuzi
huo.
Katika maelezo yake kwa Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya BUnge, Lissu alisema, “Nitajitahidi kwa kadri
inavyowezekana kutoa ushahidi unaothibitisha kwamba siyo tu kwamba utaratibu wa
kikatiba katika uteuzi wa majaji umekiukwa mara nyingi, bali pia majaji wengi
walioteuliwa kwa utaratibu wa nje ya Katiba wamekuwa hawana ‘uwezo, ujuzi na kwa
kila hali hawakufaa kukabidhiwa Madaraka ya Jaji wa Mahakama
Kuu.”
TATIZO LA MUDA
MREFU
Kuna ushahidi mkubwa kuthibitisha kwamba
kuna watu wameteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu “... wakiwa wamekaribia muda
wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi’ ya
ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana
katika miaka ya karibuni.” Ni muhimu kuweka wazi hapa kwamba utamaduni huu
haukuanza baada ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa kuwa Rais, bali ni tatizo la
muda mrefu. Kwa mfano, marehemu Jaji Kulwa Masaba na Jaji Madina Muro na majaji
Stephen Ihema, Juxton Mlay, Augustine Shayo na Vincent Lyimo waliteuliwa majaji
wa Mahakama Kuu baada ya utumishi wa muda mrefu kwingineko katika utumishi wa
umma.
Majaji Masaba na Muro waliteuliwa huku
wakiwa wagonjwa mahututi na – kwa kadri ninavyofahamu - hawakuwahi kuandika
hukumu hata moja kabla ya mauti kuwafika! Jaji Lyimo aliteuliwa Machi 28, 2007
mwaka mmoja kabla ya muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo,
ilipofika Oktoba 26, 2007 Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo Phillemon Luhanjo
alimtaarifu Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete “... ameamua kusogeza mbele muda wa
kustaafu wa Mheshimiwa Jaji Vincent Kitubio Damian Lyimo kwa miaka mitatu
kuanzia Machi 28, 2008 siku ambayo angestaafu kwa
lazima”!
Kwa upande wao, Majaji Ihema, Mlay na
Shayo walijizolea umaarufu kwa kuwa majaji wasioandika hukumu na hivyo kuwa
wacheleweshaji wakubwa wa kesi katika Mahakama Kuu. Jaji Ihema alitia fora
kwenye jambo hili kiasi kwamba Juni 16, 2003 Mwenyekiti wa sasa wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Mzee Joram Allute, alilazimika kumwandikia Rais
Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania “kwa uzembe na kukosa maadili.”
Mzee
Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia’ uamuzi kwa
zaidi ya miaka minne hadi aliponyang’anywa faili la kesi hiyo na kukabidhiwa
Jaji mwingine aliyeandika uamuzi ndani ya wiki tatu! Mwezi mmoja kabla ya barua
ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu
Barnabas Samatta kulalamikia ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao
walidai: “Hadhi na heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi
ya miaka mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama maombi
ya pingamizi.” Licha ya malalamiko haya dhidi yake, Jaji Ihema alipatiwa mkataba
wa ajira wa miaka miwili mara baada ya kustaafu mwaka
2005.
MAJAJI WA
MIKATABA
Agosti 2, 2005 Jaji Kiongozi
Hamisi Msumi alitoa taarifa kwa majaji wote wa Mahakama Kuu kwamba Jaji Ihema
alikuwa amepewa mkataba mpya baada ya kustaafu kama Jaji wa Mahakama Kuu.
Taarifa hiyo ilimfanya Jaji Bernard Luanda, wakati huo Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Bukoba, kuhoji ‘Uhalali Kikatiba kwa Majaji Kufanya Kazi kwa
Mkataba Baada ya Kustaafu.’ Katika taarifa yake kwa Jaji Kiongozi Msumi, Jaji
Luanda alisema kwamba “... suala la majaji kupewa mikataba ... linaenda kinyume
na Katiba.” Jaji Luanda alifafanua: “Kwa kuwa Jaji amestaafu, basi kiapo chake
nacho kimeondoka. Kwa bahati mbaya hawaapishwi ili washike kazi hizo za
ujaji.... Ni hoja yangu kwamba Majaji waliostaafu na kupewa mikataba si Majaji
kwa mujibu wa Katiba.”
Msimamo wa Jaji Luanda
uliungwa mkono mwaka mmoja baadaye na Jaji wa Rufaa, Augustino Ramadhani wakati
huo akiwa Kaimu Jaji Mkuu. Katika ‘Mawazo Kuhusu Vifungu Vinavyohusu Mahakama na
Majaji’ aliyomwandikia Jaji Mkuu Samatta na kunakiliwa kwa Majaji wa Rufaa wote,
Jaji Ramadhani alisema kwamba “... sio sahihi kwa Jaji Mkuu kustaafu na kupewa
mkataba wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia umri wa miaka 65 (ambao ndio umri
wa kustaafu kwa lazima kwa Jaji wa Rufaa na Jaji Mkuu).” Baadaye Jaji Luanda
aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wakati Jaji Ramadhani alikuja kuwa Jaji Mkuu wa
Tanzania.
Kauli ya Kambi kwamba kuna ukiukaji
mkubwa wa Katiba kuhusiana na uteuzi wa majaji inaungwa mkono na nyaraka za
ndani ya Serikali na hasa Ofisi ya Rais, Ikulu yenyewe. Desemba 6, 2007, mkutano
kuhusu ajira ya majaji waliostaafu ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam chini ya
uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi Luhanjo. Wajumbe wengine walikuwa pamoja na
Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika na Naibu wake Sazi Salula, Katibu Mkuu
Utumishi George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sophia Wambura na Susan
Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la
Mawaziri.
Kwa mujibu wa Kumbukumbu za Mkutano
huo, “kwa utaratibu unaotumika sasa, baadhi ya Majaji wanaofikisha umri wa
kustaafu kwa mujibu wa Ibara ya 110(1) kwa Majaji wa Mahakama Kuu na Ibara ya
120(1) ya Katiba wanaongezewa muda wa kuendelea na utumishi wao kwa mkataba
baada ya wao kuwasilisha maombi rasmi.” Baada ya mjadala juu ya jambo hili,
wajumbe wa mkutano walikubaliana kwamba “utaratibu wa kuongeza muda kwa njia ya
mkataba unakiuka masharti ya Katiba na kuleta mkanganyiko kama Majaji hao
wanastahili kulipwa mshahara au pensheni au vyote kwa
pamoja.”
Matokeo ya mkutano wa Ikulu ilikuwa ni
kuundwa kwa ‘Kikundi Kazi kwa Ajili ya Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya
Majaji Baada ya Kustaafu’ chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma. Kikundi Kazi kiliwasilisha Taarifa yake Machi 7, 2008. Katika Taarifa yake
Kikundi Kazi kinakubaliana na msimamo wa kikatiba kwamba “kwa kuzingatia Ibara
za 110 na 120 za Katiba inaonekana wazi kuwa suala la ajira za mikataba kwa
Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya kufikia umri wa kustaafu
ni kinyume cha Katiba.” Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, hadi mwezi Machi 2008, “...
walikuwepo Majaji wawili ... wa Mahakama ya Rufani na Majaji tisa ... wa
Mahakama Kuu, ambao wapo katika ajira za mkataba, na Jaji mmoja ... wa Mahakama
Kuu aliyeongezewa muda wa ajira kwa mujibu wa masharti ya
Katiba....”
Hii ina maana kwamba, kulikuwa na
Majaji kumi na moja ambao walikuwa wanafanya kazi kinyume cha Katiba na – kwa
maneno ya Jaji wa Rufaa Luanda – hawakuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba! Aidha,
kwa mujibu wa ushahidi wa nyaraka hizi, kulikuwa na Jaji mmoja tu ambaye alikuwa
ameongezewa muda wa ajira ya ujaji kwa mujibu wa Katiba. Katika mapendekezo
yake, Kikundi Kazi hakikumung’unya
maneno:
“Mikataba iliyopo hivi sasa iko kinyume
cha Katiba.... Hii ina maana kwamba Majaji hao wanafanya kazi ya Jaji kinyume
cha Katiba, hivyo kazi zote ambazo wamezifanya na wanaendelea kuzifanya wakiwa
chini ya ajira mpya za mikataba hazina uhalali wowote kisheria. Kazi hizo ni
sawa kama vile zimefanywa na mtumishi mwingine yeyote asiye na madaraka ya Jaji.
Hivyo basi, Rais ashauriwe kuifuta mikataba hiyo mara moja kwa vile ina madhara
makubwa kwa jamii na katika uteuzi wa Majaji wapya kuchukua nafasi zao. Majaji
waliofutiwa mikataba waendelee na pensheni zao kama
kawaida.”
Miaka minne imepita tangu Kikundi
Kazi kiwasilishe mapendekezo yake Ikulu lakini hakuna hatua zilizochukuliwa
kutekeleza mapendekezo hayo. Aidha, licha ya msimamo wa majaji Luanda na
Ramadhani kuwa na umri wa takriban miaka saba, utaratibu wa uteuzi wa majaji
wastaafu haujaachwa na mamlaka husika ya uteuzi. Ajira ya sasa ya Jaji Kiongozi
Fakih Jundu iko katika kundi hili la watu wasiokuwa Majaji kwa mujibu wa
Katiba.
JAJI KIONGOZI FAKIH
JUNDU
Jaji Kiongozi Fakih Jundu
aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Rais Mkapa mwaka 2003. Julai 29, 2009,
Jaji Jundu wakati huo akiwa Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Iringa, alitoa taarifa ya
kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, mara baada ya kutoa taarifa hiyo,
Jaji Jundu siyo tu alipewa mkataba wa ujaji kwa miaka mitatu, bali pia
alipandishwa cheo na kufanywa Jaji
Kiongozi.
Kama hiyo haitoshi, inasemekana sasa
kwamba Jaji Kiongozi Jundu ameongezewa mkataba mwingine tena wa miaka miwili
kuendelea kuwa Jaji Kiongozi kuanzia Julai 29, 2012! Huu ni ukiukaji wa Katiba.
Kwanza, kwa mujibu wa Taarifa ya Kikundi Kazi, “... umri wa kustaafu wa Jaji
Kiongozi ni miaka sitini.... Hivyo, iwapo Rais atamuongezea Jaji Kiongozi muda
wa kufanya kazi, hatamuongezea kama Jaji
Kiongozi.”
Kwa maana nyingine, kama ilikuwa
makosa kikatiba kumpa Jaji Jundu mkataba wa ajira kama Jaji wa kawaida, ilikuwa
makosa makubwa zaidi kikatiba kumpandisha cheo na kumfanya Jaji Kiongozi wakati
alikwishafikisha umri wa kustaafu wa Jaji Kiongozi! Pili, kwa utamaduni
uliozoeleka Tanzania, majaji wamekuwa wanaongezewa kipindi kimoja cha miaka
miwili ili wamalizie kesi walizokuwa nazo hadi muda wao wa kustaafu unawadia.
Kwa msimamo wa kikatiba ulioelezwa na Jaji wa Rufaa Luanda, Jaji Mkuu Ramadhani
na Kikundi Kazi, siyo sahihi kwa Jaji Kiongozi Jundu kustaafu na kupewa mkataba
wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa
Katiba!
Nyongeza hii ya pili ya mkataba wa Jaji
Kiongozi Jundu imewafanya watu wanaojiita ‘Watumishi wa Mhimili wa Mahakama’
kumwandikia Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kulalamikia jambo hilo.
Kwa mujibu wa barua yao, ambayo pia ilinakiliwa kwa Mwanasheria Mkuu na Jaji
Mkuu, watu hao wamesema yafuatayo kuhusu Jaji Kiongozi Jundu: “Sisi watumishi wa
Mahakama tunafahamu udhaifu mkubwa kiutendaji alionao Jaji Kiongozi wetu wa
sasa. Kimsingi hamudu madaraka haya. Ipo mifano mingi ya udhaifu wa Jaji Jundu.
Mfano alimhamisha hakimu kutoka kituo chake cha kazi kama adhabu kwa vile hakimu
huyo alitoa maamuzi ambayo yeye hakuyafurahiya kwenye ile kesi maarufu ya
kibaragashia. Ni busara za Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, ndizo zilizomsaidia
hakimu huyo.”
JAJI THOMAS
MIHAYO
Thomas Bashite Mihayo
aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Oktoba 8, 2003. Januari 16, 2006
Jaji Mihayo alitoa notisi ya kustaafu kwa mujibu wa Katiba kuanzia Juni 8, 2006
atakapokuwa ametimiza umri wa miaka sitini. Hata hivyo, Machi 8 ya mwaka huo,
Jaji Mihayo alitaarifiwa na Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete alikuwa amempa “...
mkataba wa miaka miwili kuanzia Juni 9, 2006.” Mkataba huo ulifikia mwisho wake
Juni 8, 2008. Hata hivyo, Jaji Mihayo alipatiwa mkataba mwingine tena wa mwaka
mmoja ulioanzia Juni 9, 2008 hadi Juni 8, 2009 na baada ya hapo hakupatiwa
mkataba mwingine.
Inaelekea Jaji Mkuu Ramadhani
alisahau msimamo wake wa awali kuhusu ajira za mikataba kwani ndiye
aliyependekeza Jaji Mihayo “... apewe mkataba mwingine wa mwaka mmoja...” Na
wala si Jaji Mihayo pekee aliyepatiwa au kuongozewa mkataba katika mazingira
tatanishi kama haya. Kwa mujibu wa nyaraka za Idara Kuu ya Utumishi, Jaji
Donasian Mwita alipatiwa mkataba wa ujaji Juni 28, 2004. Mkataba huo wa miaka
miwili ulianza kutumika Julai 1, 2004. Vile vile, Jaji Joseph Masanche alisaini
mkataba wa aina hiyo hiyo na Idara Kuu ya Utumishi ulioanza kutumika kuanzia
Machi 7, 2006.
MAADILI YENYE
SHAKA
Msemaji wa Kambi hakuzungumzia
masuala yanayohusu maadili ya majaji. Hata hivyo, kutokana na mjadala
uliojitokeza ndani na nje ya Bunge kutokana na hotuba yake, ushahidi umepatikana
unaoonyesha kwamba baadhi ya majaji wameteuliwa bila ya kwanza kuwafanyia
uchunguzi juu ya maadili yao.
MAJAJI
KASSIM NYANGARIKA NA ZAINAB G.
MURUKE
Kassim Nyangarika alikuwa
wakili wa kujitegemea na wakili mwenza wa Jaji Kiongozi Jundu kabla ya uteuzi
wake kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003. Kama wakili, Bwana Nyangarika aliwahi
kumwakilisha mlalamikaji katika kesi ya Peter Muti dhidi ya CIELMAC Ltd., Kesi
ya Madai Na. 314 ya 2003 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.
Katika kesi hiyo mteja wa wakili Nyangarika
alishinda.
Hata hivyo, kufuatia rufaa dhidi ya
uamuzi huo, Mahakama Kuu ilifutilia mbali mwenendo wa kesi hiyo baada ya
kugundua kwamba Wakili Nyangarika alikuwa amefanya vitendo vyenye kuashiria
uvunjifu mkubwa wa maadili. Kwa mfano, Mahakama Kuu iligundua kuwa Wakili
Nyangarika alimwelekeza hakimu – kwa kutumia ‘kipande cha karatasi cha rafu na
kilichoandikwa kirafiki’ - namna ya kuendesha kesi hiyo. Mahakama Kuu iligundua
makosa makubwa zaidi ya hilo. Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, “... kulikuwa na
mawasiliano yasiyokuwa rasmi kati ya Mahakama na Wakili.” Jaji Kalegeya alikuta
ushahidi wa uwezekano mkubwa kwamba Wakili Nyangarika ndiye aliyeandaa uamuzi wa
Mahakama katika kesi hiyo. Aidha, Mahakama Kuu iligundua kwamba Wakili
Nyangarika “... aliielekeza Mahakama kutokutoa uamuzi kwa tarehe iliyopangwa
badala yake aliielekeza itoe uamuzi huo tarehe
nyingine.”
Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, kama
kilichoonyeshwa katika mawasiliano ya Wakili Nyangarika na Mahakama ya Wilaya
kilikuwa cha kweli basi “... utoaji haki katika Mahakama hiyo uko katika hatari
kubwa kama sio jina la Mahakama yote, kitu kinachohitaji marekebisho ya haraka.”
Kwa sababu hiyo, Jaji Kalegeya alielekeza kwamba “mamlaka husika zichukue hatua
za kufichua ukweli kuhusu barua ya Wakili Nyangarika ya tarehe 18/03/2004.”
Hukumu na maelekezo ya Jaji Kalegeya yalitolewa tarehe 22 Julai, 2005. Miezi
saba baadaye, Wakili Nyangarika aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania!
Wakili mwingine mwenye maadili ya
mashaka yanayofanana na ya Jaji Nyangarika ambaye pia ameteuliwa Jaji Mahakama
Kuu ni Zainab Muruke. Kama wakili, Zainab Muruke alimwakilisha Stephen Hill
Forwood ambaye alikuwa amepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha
miaka miwili bila faini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu. Baadaye
kampuni ya mawakili ya Z.G. Muruke & Co. Advocates iliwasilisha Hati ya
Mapitio (Memorandum of Review) katika Mahakama hiyo hiyo ikiomba Bwana Forwood
abadilishiwe hukumu.
Ombi hilo lilikubaliwa na
Hakimu Mkazi Mfawidhi Kabuta na tarehe 26 Julai, 2004, Bwana Forwood
akabadilishiwa adhabu kuwa faini ya shilingi 20,000 au kifungo cha miaka miwili.
Jambo hili liliripotiwa kwa Jaji Kiongozi ambaye aliamuru uchunguzi ufanywe
uliopelekea kushushwa cheo cha Hakimu Mkazi Kabuta. Jaji Kiongozi pia aliamuru
Wakili Muruke atoe maelekezo ya ushiriki wake katika sakata hilo. Hiyo ilikuwa
tarehe 14 Desemba, 2004. Mwaka mmoja na miezi miwili baadaye, Zainab Muruke
aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
MAJAJI PELAGIA B. KHADAY NA
PATRICIA FIKIRINI
Bi. Pelagia B.
Khaday ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeteuliwa mwaka 2009. Kabla ya
uteuzi huo Bi. Khaday alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na kabla ya hapo alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu na Msajili wa Wilaya, Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha. Agosti 12, 2004, alipewa taarifa ya kusimamishwa kazi kama
Msajili wa Wilaya na kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na
‘uzito wa shutuma’ zilizotolewa dhidi yake kwa Jaji
Mkuu.
Taarifa hiyo iliandikwa na Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Edward Rutakangwa, kwa maelekezo ya Jaji Mkuu na
ilieleza kwamba Bi. Khaday alikuwa anatuhumiwa kwa “kuwashinikiza au
kuwashawishi baadhi ya mahakimu mkoani Arusha kushughulikia au kuamua kwa
upendeleo mashauri yaliyowahusu ... jamaa au rafiki zake”; na “kuwaandalia
sababu za rufaa baadhi ya washitakiwa waliotiwa hatiani na mahakama za mahakimu
hapa mkoani.”
Kabla ya kumsimamisha Bi. Khaday
kazi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alikuwa amemteua Mheshimiwa Jacob Somi, wakati
huo akiwa Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, kuwa Afisa Uchunguzi
(Enquiry Officer) ili kuchunguza tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Taarifa ya
Uchunguzi wa Awali ya Afisa Uchunguzi Somi inasema kwamba Bi. Khaday alikuwa
amelalamikiwa na mahakimu kwa kuwashinikiza ili watoe maamuzi ya kesi zilizokuwa
zinawakabili jamaa au marafiki zake.
Kwa mujibu
wa Taarifa hiyo, Hakimu Mkazi Elvin Mugeta “alikiri kuwa-approached na Bi.
Khaday ili atoe hukumu ya upendeleo kwa mshtakiwa Richard Bareto ambaye
inasadikiwa kuwa ni jamaa wa rafiki yake wa karibu.” Ijapokuwa Bi. Khaday
alikanusha kufanya hivyo, Afisa wa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “Bi. Khaday
alikuwa amejiwekea utaratibu, kama alivyodai mwenyewe, wa kuwasiliana na
Mahakimu kwa lengo la kuwafahamisha pamoja na mambo mengine malalamiko
yaliyokuwa yakimfikia dhidi yao ili kuwanusuru
wasiharibikiwe.”
Hata hivyo, Afisa Uchunguzi
Somi aliridhika kwamba “utaratibu huu ulikuwa kero kwa mahakimu pale alipoutumia
kwa kushinikizwa na jamaa zake na/au rafiki zake kwa lengo la kupata maamuzi ya
upendeleo. Kitendo cha kumtoa mahakamani Hakimu kwa lengo la kutaka kujua hatima
ya mshtakiwa Bareto aliyekuwa asomewe hukumu siku hiyo, ni mfano wa matumizi
mabaya ya utaratibu huo.”
Afisa Uchunguzi Somi
hakupata uthibitisho wa madai ya Bi. Khaday kuwaandalia sababu za rufaa
washtakiwa waliotiwa hatiani. Hata hivyo, kwa mujibu wa Taarifa yake, “...
sikuridhishwa na utaratibu wake wa kupeleka nakala ya hukumu kwa Bi. Mushi na
kumtaka aisome ili kuona kama kuna uwezekano wa mshtakiwa Hussein Ramadhani
Kitema kukata rufaa Mahakama Kuu baada ya kufungwa jela na Bw. Mugeta.” Afisa
Uchunguzi Somi alipendekeza kwamba Bi. Khaday – “ambaye ni mtumishi wa Mahakama
kwa kipindi kisichopungua miaka 20...” - apewe nafasi ya
kujirekebisha.
Baada ya kuwasilishwa kwa
Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alimteua Mh. Samuel
Karua, Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kuwa Investigation Officer.
Tarehe 23 Februari 2007, Investigation Officer Karua aliwasilisha Taarifa ya
Uchunguzi wake kwa Jaji Mkuu. Taarifa ya Investigation Officer Karua ilimkosha
Bi. Khaday kwa tuhuma zote dhidi yake.
Hata
hivyo, Taarifa ya Investigation Officer Karua ina maeneo mengi yanayoleta
mashaka. Kwanza, kama Investigation Officer Karua mwenyewe alivyosema, shahidi
muhimu katika uchunguzi wake alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi. Vile vile,
shahidi huyu alikuwa ‘star witness’ katika uchunguzi wa awali mbele ya Afisa
Uchunguzi Somi na ndiye aliyetoa ushahidi wa yeye na mahakimu wengine kuingiliwa
katika kazi zao na Bi. Khaday.
Hata hivyo,
mbele ya Investigation Officer Karua, shahidi huyu muhimu alikana kila kitu
alichokisema mbele ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa kiasi kikubwa, Investigation
Officer Karua aliitumia about turn hii kumkosha Bi. Khaday dhidi ya tuhuma zote
zilizokuwa zinamkabili. Cha kushangaza ni kwamba Investigation Officer Karua
hakujiuliza na hakumuuliza shahidi huyu sababu za kukana ushahidi wote alioutoa
mbele ya Afisa Uchunguzi Somi.
Je, alirubuniwa
au kutishwa ili amsaidie Hakimu na mtumishi mwenzake katika Mahakama ya Tanzania
asifukuzwe kazi? Kama sio hivyo, je, ni sababu zipi zilizomfanya shahidi huyu
muhimu kubadili ushahidi wake kwa kiasi hicho? Je, ushahidi alioutoa shahidi
huyu mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ulikuwa wa uongo? Na kama ulikuwa wa uongo,
ushahidi wake wa pili kwa Investigation Officer Karua ni wa kweli kiasi gani
mpaka kumfanya Investigation Officer Karua kutamka kuwa shahidi huyu ‘anaweza
... kuwa anasema ukweli.’
Inaelekea
Investigation Officer Karua, Hakimu Mkuu Mkazi mwenye uzoefu wa miaka mingi
katika Mahakama, alifanya kazi yake kwa mtazamo wa kimahakama zaidi badala ya
kutumia mtazamo wa kiupelelezi na/au kiuchunguzi ambayo hasa ndiyo ilikuwa kazi
yake katika uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Kwa mtazamo wa kimahakama,
ukweli kwamba shahidi muhimu kama Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi alikana ushahidi
wake wa awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ilikuwa inatosha kumfutia Bi. Khaday
hatia yote. Kwa mtazamo wa kiupelelezi/kiuchunguzi, about turn ya shahidi huyu
ingemfanya Investigation Officer Karua kuchunguza zaidi sababu za kigeugeu
hicho.
Pili, Investigation Officer Karua
hakuipa uzito wa kutosha Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa mfano, Taarifa ya
Afisa Uchunguzi Somi – yenye kurasa 14 zilizochapwa - imeelezewa katika Taarifa
ya Investigation Officer Karua kwa aya moja tu! Kwa sababu hiyo, ni vigumu
kukubaliana na Investigation Officer Karua kwamba Taarifa ya Afisa Uchunguzi
Somi ‘ilikuwa muhimu sana’ wakati umuhimu huo haujafafanuliwa wala kuelezewa
hata kidogo katika Taarifa yake.
Aidha,
Investigation Officer Karua alitakiwa kueleza sababu za kutofautiana na Afisa
Uchunguzi Somi kwamba Bi. Khaday alikuwa anakera mahakimu kwa kuwasiliana nao
baada ya kushinikizwa na ndugu au rafiki zake ili wapatiwe upendeleo katika kesi
zilizokuwa zinawakabili. Investigation Officer Karua hakufanya hivyo. Vile vile,
Investigation Officer Karua hakuona ajabu wala kujiuliza kama ilikuwa ni kitu
cha kawaida kwa Bi. Khaday kumleta Richard Bareto – mshtakiwa aliyehusishwa na
shinikizo la Bi. Khaday kwa Hakimu Mkazi Mugeta – kama shahidi wake wa
utetezi.
Tatu, Investigation Officer Karua
hakutoa sababu za maana za kutochukua ushahidi wa mahakimu wengine waliodaiwa
kushinikizwa na Bi. Khaday. Katika aya moja tu iliyowahusu mahakimu hao,
Investigation Officer Karua alisema kwamba siku ya kutoa ushahidi wao kwake,
watu hao “... walishikilia msimamo wa kauli walizotoa mbele ya Bwana Somi ... na
baada ya tafakuri ya muda ... mashahidi hawa
waliachiwa.”
Mbele ya Afisa Uchunguzi Somi,
mashahidi hawa wawili, Hakimu Mkazi Msumi na Hakimu Mkuu wa Wilaya Mlay,
walikuwa wamesema kwamba “... huko nyuma (Bwana Msumi) aliwahi kuitwa na
mlalamikiwa baada ya wadhamini walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana ...
kumpelekea malalamiko ya kukataliwa dhamana, maelezo ambayo hayakuwa na ukweli
wowote.” Aidha, kwa mujibu wa Afisa Uchunguzi Somi, “... katika hali isiyokuwa
ya kawaida Bw. Mlay, PDM hakuwa tayari kueleza kilichomsibu hadi kujiengua
katika usikilizaji wa kesi ambayo Bi. Mushi alidai ilikuwa inamkabili rafiki
yake wa karibu na Bi. Khaday.” Investigation Officer Karua hakuona sababu yoyote
ya kufuatilia ushahidi wa mahakimu hawa
wawili!
Nne, Investigation Officer Karua
anakubali kwamba hali ilikuwa tete katika Kituo cha Arusha: “Inaelekea mtuhumiwa
alikuwa na mahusiano mabaya na baadhi ya mahakimu.” Kama hivyo ndivyo
ilivyokuwa, Investigation Officer Karua alikuwa na wajibu wa kuchunguza chanzo
cha mahusiano hayo mabaya, hasa kwa vile kulikuwa sio tu na tuhuma bali pia
ushahidi wa mahakimu husika kwamba Bi. Khaday alikuwa anawaingilia mahakimu
katika kazi zao. Hakufanya hivyo. Badala yake Taarifa ya Investigation Officer
Karua inaonekana kama jitihada za kumkosha Bi. Khaday dhidi ya tuhuma nzito za
ukosefu wa maadili ya kimahakama. Jitihada hizi zilifanikiwa kwani miaka miwili
baada ya Taarifa ya Investigation Officer Karua, Bi. Khaday aliteuliwa kuwa Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Na wala siyo Bi.
Khaday pekee aliyeneemeka na taarifa hiyo. Bi. Patricia Fikirini, ambaye Taarifa
ya Afisa Uchunguzi Somi inamwelezea kama mmoja wa mahakimu waliosikiliza kesi ya
mfanyabiashara maarufu wa Arusha, Justin Nyari iliyokuwa chanzo cha tuhuma dhidi
ya Bi. Khaday – alihusishwa na tuhuma dhidi ya Bi. Khaday kwa maneno yafuatayo:
“... Kama mtawala ... (Bi. Khaday) ... alisema aliwahi, tena kwa nia njema,
kumweleza Bi. Fikirini ... kuhusu uvumi kwamba mume wake alikwenda gerezani na
kuchukua mamilioni ya fedha kwa Bw. Nyari na hivyo kumshauri awe mwangalifu
zaidi”! Katika uteuzi wa majaji uliofanywa na Rais Kikwete mwezi Juni mwaka huu,
Bi. Patricia Fikirini naye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
Wapo wanaoweza kusema kwamba Bi.
Khaday hakupatikana na hatia yoyote na kwa hiyo haikuwa makosa kuteuliwa kuwa
Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, inaweza kudaiwa kwamba Bi. Fikirini hajawahi
kutuhumiwa kwa kosa lolote la maadili na kwamba ‘uvumi’ pekee hautoshi kumnyima
mtu mwenye sifa haki ya kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa wenye hoja za aina
hii jibu langu ni kwamba kiwango cha ‘sifa maalum’ kinachotakiwa na Katiba kwa
mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ni mtu ambaye “... kwa kila hali anafaa
kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu....” Kiwango hiki ni cha juu kiasi
kwamba kutokuwa na hatia pekee haitoshi kumfanya mhusika kuwa ‘kwa kila hali
anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.’ Kwa maoni yangu, mtu
aliyeundiwa uchunguzi wa kimaadili au ambaye kuna uvumi unaomhusisha na rushwa
‘hafai kwa kila hali’ kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu. Majaji
Khaday na Fikirini wapo kwenye kundi
hili.
JAJI ALOYSIUS
MUJULIZI
Jaji Aloysius Mujulizi
alikuwa miongoni mwa watu ishirini walioteuliwa Majaji wa Mahakama Kuu mwezi
Februari, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Jaji Mujulizi alikuwa wakili wa
kujitegemea katika kampuni ya mawakili ya Ishengoma, Masha, Magai & Mujulizi
Advocates (IMMMA) ya Dar es Salaam. Kampuni hii ya mawakili ndiyo iliyoshiriki
katika kuanzishwa kwa kampuni iitwayo Deep Green Finance Co. Ltd. mnamo tarehe
18 Machi 2004. IMMMA Advocates vile vile walikuwa mawakili wa Tangold
Ltd.
Makampuni haya mawili yanatuhumiwa
kutumika kupitishia mabilioni ya fedha zilizoibiwa Benki Kuu ya Tanzania kati ya
mwaka 2005 na 2006. Kwa mfano, katika kipindi kifupi cha miezi minne kati ya
Agosti 1 na Desemba 10, 2005 kampuni ya Deep Green Finance ilipokea jumla ya
shilingi 10,484,005,815.39 kutoka akaunti ya kulipia madeni ya nje (EPA)
iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania. Katika kipindi hicho hicho, kampuni ya Tangold
Ltd. ililipwa dola za Marekani 13,736,628.73 kutoka kwenye akaunti hiyo ya EPA.
Nyaraka zilizowasilishwa BRELA na mawakili wa IMMMA Advocates na kusainiwa na
Gavana wa Benki Kuu wa wakati huo Daudi Ballali tarehe 20 Mei 2005 zinaonyesha
kwamba Tangold Limited ilikuwa kampuni ya kigeni kutoka Jamhuri ya Mauritius.
Haya yote yalitokea wakati Jaji Mujulizi akiwa wakili mwenza wa IMMMA
Advocates.
‘SIFA MAALUM’ ZENYE
SHAKA
JAJI WA RUFAA MBAROUK
SALIM MBAROUK
Mbarouk Salim Mbarouk
aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania mwaka 2008.
Kabla ya uteuzi huo Jaji Mbarouk alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Sifa
za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa zimeainishwa katika ibara ya 118(3) ya
Katiba: “Majaji ... wa Rufani watateuliwa na Rais, kwa kushauriana na Jaji Mkuu,
kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ...
zilizoainishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka miongoni mwa watu
wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria
zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka kumi na
tano.”
Kwa mujibu wa Ibara ya 94(3) ya Katiba
ya Zanzibar, 1984, “mtu hatoweza kuteuliwa kuwa Jaji au Kaimu Jaji wa Mahkama
Kuu mpaka awe na shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu kinachotambuliwa au Chuo cha
aina hiyo; au awe au amewahi kuwa Jaji wa Mahkama zilizofanana na hii kwa kesi
zote za jinai na madai katika Tanzania au sehemu yoyote ya Jumuiya ya Madola au
Mahkama ya Rufaa kutoka Mahkama hizo; au awe Mwanasheria wa Zanzibar au Tanzania
kwa kipindi kisichopungua miaka saba; au awe na uzoefu wa Jaji au mwanasheria
kwa pamoja usiopungua miaka saba.” Jaji Mbarouk hajatimiza hata moja ya masharti
hayo ya Katiba ya Zanzibar. Jaji huyu hana shahada yoyote ya sheria
inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanzania kama inavyotakiwa na Ibara ya
109(7) ya Katiba. Jaji huyu ana stashahada ya juu ya sheria (Post Graduate
Diploma in Law) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili ya Sanaa
ya Chuo Kikuu cha nchini Uingereza.
Uteuzi wa
Jaji Mbarouk kuwa Jaji wa Rufaa ulileta minong’ono mingi katika taaluma ya
sheria kiasi kwamba marehemu Wakili Leopold Kalunga anasemekana kufungua shauri
katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka uteuzi huo utenguliwe. Hata hivyo, Wakili
Kalunga alifariki kabla ya shauri lake kusikilizwa na kwa hiyo liliondolewa
mahakamani. Aidha, monong’ono hiyo ilimfanya Jaji wa Rufaa Mbarouk kujiunga na
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambako bado ni mwanafunzi hadi ninapoandika
Addendum hii.
MAJAJI ‘WALIOTOLEWA
MITAANI’
Katika Maoni ya Kambi tulidai
kwamba “... sasa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ambao hawajawahi
kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na - kwa sababu hiyo -
hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba....” Ukiacha uteuzi wa
Jaji wa Rufaa Mbarouk ambao haubanwi na masharti ya Ibara ya 109(1) na 113(1)(a)
ya Katiba, majaji wengine waliotajwa kwenye Addendum hii hawakupendekezwa na
Tume ya Utumishi wa Mahakama. Majaji wengine ambao pia hawajawahi kupendekezwa
na Tume hiyo ni pamoja Fatuma Massengi, Mary Sumari, Imani Mkwawa-Aboud na
Sekela Mushi.