Powered By Blogger

Tuesday, August 21, 2012

Mawakili kesi ya Hamad Yashid"wapinga uwezo wa Makama kuu"

Gazeti la Mwananchi limeandika, Kwamba Mawakili wa wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) katika kesi dhidi ya mbunge wa Wawi, Zanzibar, Hamad Rashidi na wenzake 10, wamedai kuwa Mahakama Kuu Tanzania haina uwezo wa kuwachukulia hatua kwa kumvua uanachama Rashid na wenzake.

Mawakili hao Taslima Law Chamber ( Advocates) na J C Kerariy& Co Advocates wametoa madai hayo wakati wa usikilizwaji wa maombi ya Rashid na wenzake wanaoiomba Mahakama Kuu Dar es Salaam kuwatia hatiani na kuwafunga wadhamini wa CUF.

Rashid na wenzake waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo  Januari 10 mwaka huu , wakidai kuwa Baraza la Taifa la Uongozi la CUF lilipuuza amri ya mahakama hiyo iliyolizuia kuwajadili wala kuwachukulia hatua zozote wakati wa mkutano wake wa Januari 4, 2012, mjini Zanzibar.Amri hiyo ya Mahakama kulizuia baraza hilo kuwachukuliwa hatua yoyote Rashid na wenzake ilitolewa na Jaji Agustine Shangwa Januari, 2012 kufuatia maombi waliyoyawasilisha mahakamani hapo Januari 3, 2012, chini ya hati ya dharura.

Katika maombi hayo (ya Januari 3) Rashid na wenzake walidai  kuna kesi ya madai namba 1 ya mwaka 2012  waliyoifungua mahakamani hapo wakihoji muundo wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho   na uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo.

Katika maombi hayo walidai kuwa licha ya baraza hilo kupata taarifa za kuwepo kwa amri hiyo ya mahakama saa tatu kabla, lakini baraza hilo liliendelea na azma yaka na hatimaye kuwafukuza uanachama.

Mbali na wadhamini hao, wengine ni wajumbe wa Baraza Taifa la Uongozi la chama hicho, Hivyo wanaiomba mahakama iwatie hatiani na kuwafunga jela wadhamini hao a pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la Uongozi la chama hicho akiwemo Makamu wa kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika utetezi wao waliouwasilisha mahakamani hapo kwa njia ya maandishi wadhamini hao wa CUF kupitia kwa mawakili wao, wanadai wakati baraza hilo likitoa uamuzi wa kuwavua uanachama Rashid na wenzake, hapakuwa na amri halali ya Mahakama.

Mawakili hao wa CUF wanadai kuwa amri hiyo inayodaiwa na waombaji haikuwa  nakala halisi bali nakala iliyonakiliwa kwa njia ya kielektroniki [scanned] na kwamba hata hivyo hakuna ushahidi kwamba iliwafikia wadaiwa.

Hata hivyo kwa mujibu wa mawakili hao, hata kama amri hiyo ingekuwa ni halali na hata kama kungekuwa na ushahidi kuwa iliwafikia wadaiwa kabla ya kutoa uamuzi wa kuwavua uanachama walalamikaji bado Mahakama Kuu haiwezi kuwachukulia hatua.

Wanadai kuwa utaratibu wa kuwasilisha taarifa na utekelezaji wa amri zinazotolewa na mahakama zote kwa jumla nchini Tanzania kama unavyoelezwa katika  Amri ya V Kanuni ya 22 (2) CPC haukufuatwa.

Mawakili hao wanadai kuwa kwa mujibu wa amri na kanuni hizo kama mlalamikiwa anaishi katika mamalaka ya Mahakama  Kuu ya Zanzibar , amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania Bara kwenda kwa malalamikiwa ambaye ni mkazi wa Zanzibar ilipaswa ipitie kwanza Mahakama Kuu ya Zanzibar.“Utaratibu huu haukufuatwa na mlalamikaji wa kwanza na kile mlalamikaji wa kwanza alichokuwa akijaribu kufanya hakiko katika matakwa ya kisheria inayotumika,” wanadai  mawakili hao.

Wanadai katika jedwali la kwanza la Katiba ya Tanzania, Mahakama Kuu si miongoni mwa mambo ya Muungano, isipokuwa Mahakam a ya Rufani tu, hivyo Mahakama Kuu ya Tanzania haina mamlaka ya kisheria kwa mambo yanayofanyika Zanzibar.

Mbali na Hamad Rashid wengine waliofukuzwa uanachama CUF ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma na Juma Saanane, wote wakiwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho. 

No comments: