Powered By Blogger

Thursday, July 26, 2012

SAKATA LA FAO LA KUJITOA "MAMLAKA YA HIFADHI YA JAMII"YATOA TAMKO.



Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), inapenda kutoa ufafanuzi juu ya mafao ya kujitoa. Ufanunuzi  huu unakwenda sambamba na taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na vyombo vya habari  na kuleta mkanganyiko  miongoni mwa Wanachama na Wadau wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.

Kufuatia hali hiyo Mamlaka inatoa ufafanuzi ufuatao:

Marekebisho kuhusu  kusitisha fao la kujitoa  yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha uzeeni.

Ni kweli kuwa Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Sheria ya Mamlaka zimefanyiwa marekebisho. Mchakato wa marekebisho hayo ulihusisha wadau kwa kuzingatia utatu yaani wawakilishi kutoka  vyama vya wafanyakazi, Chama cha waajiri pamoja na Serikali. 

Kwa kutambua  tofauti ya ajira, tofauti ya mazingira ya kazi, tofauti ya  sababu za ukomo wa ajira, na umuhimu wa Mwanachama  kunufaika na michango yake wakati angali katika  ajira, Mamlaka inaendelea na mchakato wa kuandaa miongozo na kanuni za mafao ambazo lengo lake ni kuboresha maslahi ya  wanachama. Miongozo na  kanuni hizo zitajadiliwa na wadau wakiwemo  wafanyakazi, waajiri na Serikali kabla ya kuanza  kutumika.

Kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo maombi mapya ya  kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuiwezesha Mamlaka na Mifuko ya  Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa wadau. 

Tangazo hili halitowahusu wanachama waliojitoa kabla ya  tarehe 20/07/2012.
Mamlaka inakanusha vikali kwamba  sitisho la fao la kujitoa si  kwasababu za kiserikali au kwasababu mifuko imefilisika. Tunapenda kuwahakikishia kwamba Mifuko yote ipo thabiti na  michango yote ya wanachama ipo salama.

Hivyo, Mamlaka inawaomba wanachama na wadau wote wa  sekta ya Hifadhi ya Jamii kuwa na utulivu wakati mchakato huu ukiendelea  kwa lengo ya kulinda na kutetea maslahi ya mwanachama.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji

SSRA-Makao Makuu

No comments: