Powered By Blogger

Tuesday, July 17, 2012

JAJI KIONGOZI AKANUSHA MADAI YA TUNDU LISSU.


MH.JUNDU WA KWANZA MBELE


JAJI  Kiongozi Fakhii Jundu amekanusha madai yaliyotolewa na Mnadhimu wa Upinzani Tundu Lisu kuwa majaji wengi wanaoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete huteuliwa bila ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Akizungumza na  mahakimu na wafanyakazi wa Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kinondoni, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na  Mahakama ya Mwanzo ya Kinondoni, alisema majaji wote wanaoteuliwa na Rais Kikwete wanateuliwa baada ya kufuata taratibu zote ikiwamo na ile ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Kumekuwapo na malalamiko kuwa kuna majaji wanateuliwa na Rais bila ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama,  malalamiko hayo si ya kweli hakuna jaji aliyewahi kuteuliwa bila ya kuwapo kwa  ushauri  wa Tume ya Mahakama,”alisema Jaji Kiongozi.Pia  alisema  kumekuwepo na malalamiko  mengi yanayoelekezwa  katika idara za mahakama ikiwamo ucheleweshwaji wa utoaji wa haki, mrundikano wa mashauri mahakamani na kutolewa kwa hukumu zenye utata.

Jaji Jundu alisema  jamii na wadau mbalimbali  wamekuwa wakipeleka malalamiko kwao ya  kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama  Kuu  kuhusu ucheleweshwaji wa utoaji haki katika mashauri yanayowakabili kwa wakati.

Hivyo aliwaagiza mahakimu  kuwahimiza mawakili wa serikali katika kila shauri  kukamilisha upelelezi  haraka iwezekanavyo  na dhamana zitolewe bila ya kuwapo kwa masharti magumu ili kupunguza mrundikano wa mahabusu gerezani.

“Mahakimu wengi wamekuwa wakipenda kutoa adhabu za vifungo kitu ambacho kinasababisha mrundikano wa mahabusu gerezani, angalieni  uwezekano wa  kutumia adhabu mbadala kwa sababu sheria inaruhusu ili kupunguza mrundikano huo wa mahabusu katika magereza, huko hali siyo nzuri,”.Alisema mashauri yanayo suasua wayapunguze mahakamani kwa kuzingatia kanuni ya siku 60 na aliwaonya  kwamba wasiitumie kanuni hiyo vibaya.

Kwa upande wa mashauri yaliyokaa muda mrefu, Jaji Jundu alisema  ‘kama shauri limekaa  muda mrefu, washtakiwa wakiachiliwa huru  kuwakamata ni mchezo unaoiabisha mahakama’.

Jaji huyo  pia aliwataka mahakimu nchini kujipanga, kuwahi kazini na  kusikiliza mashauri kwa wakati na kutoa hukumu mapema  iwezekanavyo zikiwamo kesi za madai.

Aliwasisitiza mahakimu  kuacha  kutumia vifungu vya sheria vya kiufundi vinavyopokonya haki na kusababisha  mrundikano wa mahabusu magerezani.

“Kuna baadhi ya mahakimu katika mashauri ya mirathi  wanajifanya wao ndiyo wagawa mali au wananufaisha watu wengine wasiostahili  na familia husika; hakimu kazi yake ni kuteua msimamizi wa mirathi na si vinginevyo ,”alisisitiza kusema Jaji huyo Kiongozi.

Hivyo aliwataka mahakimu kuepuka rushwa, wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wanaongoza kwa kupokea rushwa kitendo ambacho kinaifedhehesha idara hiyo ya mahakama na kuwaonya kuwa wanapopokea rushwa wasione kuwa hiyo ni siri  ikibainika hatua kali zitachukuliwa. Chanzo gazeti la Mwananchi.

No comments: