Powered By Blogger

Tuesday, July 17, 2012

MBUNGE"MTUHUMIWA WA RUSHWA" ASOMEWA MAELEZO YAKE.



Mh. Badwel akiwa akiwa na Maofisa wa Polisi


MBUNGE wa Bahi, mkoani Dodoma, Bw. Omary Badwel (CCM), anayekabiliwa na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya sh. milioni moja, amedai Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Bi. Sipora Liana, ameshindwa kuonesha ushirikiano kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kama wanavyofanya wenzie.


Mbele ya Hakimu Bw. Faisal Kahamba, wakili wa Serikali kutoka Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Janeth Machullya, alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakati akimsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali.

Bi. Machullya alidai kuwa, mshtakiwa alitoa aneno hayo kwa Bi. Liana walipokutana katika Hotel ya Peacock, baada ya kumpigia simu kwa ahadi ya kumpa ujumbe muhimu.

Alidai Bw. Badwel alimwambia Bi. Liana kuwa, Wakurugenzi wenzake huwa wanatoa kiasi cha fedha kwa wajumbe wa kamati hiyo kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa mahesabu katika Wilaya zao kabla kamati haijaenda kufanya ukaguzi.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo anatakiwa kutoa sh. milioni nane kwa kamati hiyo ili kila mjumbe apate sh. milioni moja ambapo Bi. Liana alimjibu kuwa, wakati huo hakuwa na kiasi hicho ila anaweza kwenda ATM na kumpatia sh. milioni moja.

Baada ya kumueleza hayo, Bw. Badwel alichukuwa karamu, karatasi na kuandika namba yake ya akaunti katika Benki ya NMB ambayo ni 5051602671, kumpa Bi. Liana na kumueleza fedha ambazo zitakazobaki, aziingine katika akaunti hiyo kabla ya kikao cha kamati Juni 4 mwaka huu.

Walipomaliza mazungumzo hayo, mshtakiwa alimruhusu Bi. Liama akatowe hizo fedha na baada ya muda, alirudi nazo kwenye bahasha ambazo ni noti za sh. 10,000 na Bw. Badwel alizipokea na kuziweka pembeni mwa sahani yake ya chakula pamoja na simu.

Ilidaiwa kuwa, baada ya hapo Bi. Liana aliondoka ndipo mshtakiwa alikamatwa na Maofisa wa TAKUKURU, kwa kukutwa na rushwa ya sh. milioni moja na kuomba sh. milioni nane.

Baada ya maofisa wa taasisi hiyo kuzikagua fedha hizo, walikuta nyingine zikiwa zinafanana namba na zile wanazotumia wao kwa ajili ya mitego.

Katika maelezo hayo, ilidaiwa LAAC ilipangiwa kufanya ukaguzi wa hesabu katika Wilaya ya Bagamoyo na Mkuranga ambapo Bw. Badwel alimpigia simu Bi. Liana kwa mara ya kwanza Mei 30 mwaka huu, kupitia namba 0784858255 na kujitambulisha kwake.

Katika mawasiliano yao, Bw. Badwel alimwambia Bi. Liana kuwa ana ujumbe wake kutoka kamati ya LAAC, hivyo anataka wakutane haraka kabla ya Juni 4 mwaka huu ili ampatie ambapo mambo si shwari katika kamati hiyo.

Juni mosi mwaka huu, Bw. Badwel alipiga simu kwa mara nyingine bila kueleza ujumbe huo unahusu nini zaidi ya kusisitiza wakutane ndipo Juni Juni 2 mwaka huu, walipokutana katika hoteli hiyo,  upande wa Kasuku Bar.

Katika kesi hiyo, Bw.Badwel anadaiwa kuomba rushwa ya sh milioni nane, kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Bi. Sipora Liana.

Ilidaiwa kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Mei 30 na Juni 2, 2012, katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa Juni 2, 2012 katika hoteli ya Peacock, Dar es Salaam, akipokea rushwa ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Mshtakiwa ambaye ni mjumbe wa LAAC, aliomba kiasi hicho cha fedha ili kuwashawishi wajumbe wa kamati hiyo waweze kupitisha taarifa ya fedha ya mwaka 2011/2012.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi. Upande wa mashtaka umedai kuwa na na mashahidi 16 na vielelezo mbalimbali. Chanzo gazeti la Majira.

No comments: