Powered By Blogger

Thursday, June 23, 2011

Wananchi wapambana na polisi kuwaokoa wenzao.

MABOMU ya machozi, risasi zilirindima jana kwa saa mbili huku wakazi wa Mji wa Bunda wakifunga maduka na kukimbia ovyo kwa hofu wakati polisi wa Kituo cha Bunda mkoani Mara walipokuwa wakipambana na wananchi wenye hasira kali waliotaka kuvamia kituo hicho.

Askari hao wakiwa na silaha hizo walionekana wametanda kuzunguka kituo hicho wakiwa na magari na kusababisha barabara kubwa ya Mwanza-Sirari kufungwa kwa muda wakati wa mapambano hayo.Milio ya risasi ilisikika mfululizo kuanzia saa 2:30 hadi saa 4:30 asubuhi jana ililenga kutawanya mamia ya wakazi wa Kijiji cha Tairo waliojichanganya na wenyeji wa mji huo huku na silaha za jadi na mawe kwa ajili ya kutaka kuvamia kituo hicho na  kuwaokoa watu wawili ambao walidai wanashkiliwa na jeshi hilo bila hatia.

Kabla ya kuvamia kituo hicho, wananchi hao walichoma moto na kuteketea nyumba 10 za familia nne tofauti kijijini hapo ambao waliwatuhumu kuhusika katika matukio matatu ya kuvamia zahanati na Ofisi ya Shule ya Tairo na kupora viti vitatu, magunia mawili ya pamba ya mwalimu mmoja wa shule hiyo aliyetajwa kwa jina la moja la Bw. Marekera na duka moja la Bw. Kikore Magwega.

Watu hao Bw. Jekonia Abiero ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Tairo katika miaka ya hivi karibuni na Bw. Kikore Magwega ambaye ni mfanyabiashara aliyeporwa bidhaa zake katika tukio hilo la ujambazi katika kijiji hicho wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano huku wananchi wakishinikiza waachiwe huru.

Hata hivyo, bila madhara makubwa polisi hao walifanikiwakuwatawanya wananchi hao ambapo walisema kwa sasa jeshi hilo limepewa mbinu mpya ya kupambana na wananchi wanaoshikilia sheria mikononi bila madhara na kuwataka wazingatie haki ya sheria.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi wilayani Bunda watuhumiwa wawili wa ujambazi wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo wamekamatwa  baada ya kujeruhiwa vibaya na wananchi wenye hasira na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda chini ya ulinzi wa polisi na kwamba juhudi za kuwakamata wengine zaidi bado zinafanywa na jeshi hilo.

Akithibitisha tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Tairo, Bw. Raimond Misana aliwataja watuhumiwa wa ujambazi katika matukio hayo kuwa ni Bw. Amos Machele, Bw. Marwa Ghati ambao wameshikiliwa na polisi.

Alitaja watuhumiwa waliokimbia kwa kuwatoroka wananchi kuwani Bw. Nyango Mgore na Bw. Bhoke Nyitambe na kwamba wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuhusika katika matukio hayo ya ujambazi.

Bw. Misana alitaja baadhi ya nyumba za watuhumiwa zilizochomwa moto na wananchi wenye hasira ni pamoja na nyumba 4 za Bw. Nyango Mgore, nyumba 3 za Bw. Bhoke Nyitambe, nyumba 2 za Bw. Amos Machela zilizochomwa pamoja na kibanda 1 cha biashara cha Bw. Amos Machela.

matukio ya wananchi wanaojidai kuwa na hasira kali imeendelea mkoani Mara ambapo hivi karibuni baadhi ya wananchi wa Nyamongo wilayani Tarime walipambana na polisi katika migodi wa North Mara na kusababisha vifo vya watu watano siku chache kabla wananchi wengine kuvamia Kituo cha Polisi mjini Mugumu, Serengeti kwa lengo la kutaka polisi kuachia baadhi ya watuhumiwa wa mauaji.Chanzo gazeti la majira

No comments: