Powered By Blogger

Wednesday, June 22, 2011

Mh.Hakimu afa Chumbani kimyakimya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke
HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo ya Pangani iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Jaffar Mselem (62), amekutwa amekufa katika nyumba anayoishi na mwili wake kukaa ndani kwa zaidi ya siku mbili bila kujulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, amesema, kifo cha Hakimu huyo, kinasadikiwa kutokea usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu nyumbani kwake eneo la Kwa Azizi Ali wilayani Temeke.

Misime amesema, uchunguzi wa awali umebaini kuwa kifo cha hakimu huyo mstaafu anayefanya kazi kwa mkataba, kilisababishwa na umeme alipokuwa akiwasha kifaa cha kuchemshia maji ya kuoga.

“Kwa mujibu wa majirani zake na mtoto wake, Jumapili Mselem alishinda kwa mtoto wake anayeishi eneo hilo hilo hadi aliporejea nyumbani kwake jioni,” amesema Misime.

Amesema, baada ya kurejea katika nyumba hiyo ambayo anaishi peke yake upande mmoja huku upande mwingine ukikaliwa na wapangaji wake, Mselem hakuonekana tena hadi mwili wake ulipokutwa juzi sakafu chumbani mwake.

Kamanda Misime amesema, kugundulika kwa kifo, kulitokana na mmoja wa wafanyakazi wa Mahakama anakofanyia kazi Mselem, kufika katika nyumba hiyo juzi kwa lengo la kumwangalia baada ya kutoonekana kazini Jumatatu na kukuta mlango wa nyumba yake umefungwa.

Alisema baadaye walitoa taarifa Polisi ambao walifika na kuvunja mlango, wakamkuta Hakimu huyo tayari amekufa na mwili umeanza kuharibika, suala ambalo majirani walidai kuhisi harufu kwa muda bila kujua ilikokuwa ikitokea.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa uchunguzi huku upelelezi wa tukio hilo ukiendendelea.Chanzo gazeti la habari leo.

No comments: