Powered By Blogger

Thursday, June 9, 2011

Waajiri wakaidi kupandishwa kizimbani

Mh.Gaudensia Kabaka
SERIKALI imewataka waajiri kuwaruhusu wafanyakazi wao kushiriki katika mafunzo ya sheria za kazi yanayotolewa nchini kote kinyume na hivyo Idara ya Ukaguzi inaweza kuwafikisha  mahakamani. Mpango huo wa elimu unagusa wadau wote waliopo katika sekta binafsi na sekta ya umma.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema hayo juzi Dar es Salaam wakati akizungumzia elimu inayotolewa kwa wadau hao ili kuwaongezea uelewa juu ya sheria za kazi, haki na wajibu wao katika utekelezaji wake.

Sheria hizo ni za mwaka 2004 ambazo ni sheria namba sita ya ajira na mahusiano kazini na sheria namba saba ya taasisi za kazi.

Alisema, mpango huo umeanza kutekelezwa rasmi Machi mwaka huu kupitia ofisi zao nchini kote na kwamba hadi sasa zaidi ya wafanyakazi 1,000 kutoka sehemu mbalimbali wameshiriki katika mafunzo hayo.

“Licha ya kwamba mpango huo unahusisha waajiri na wafanyakazi, lakini wapo waajiri wanaowakataza wafanyakazi wao kushiriki, jambo ambalo halileti tija katika utendaji kazi,” alisema Waziri Kabaka bila ya kuwataja waajiri wanaofanya hivyo.

Waziri Kabaka alisema, kwa waajiri wanaowakataza wafanyakazi wao kushiriki katika mafunzo hayo kanuni za sheria hizo zinaruhusu Idara yaUkaguzi kuwapeleka mahakamani waajiri ambao hawatotekeleza.

Alisema, hakuna mwitikio wa wafanyakazi kushiriki katika mafunzo hayo, huku waajiri wakidai kuwa kwa kufanya hivyo kunaweza kupunguza uzalishaji kwenye sehemu zao za kazi.

Alisema, upo umuhimu wa wafanyakazi kuhudhuria katika mpango huo na kuzifahamu sheria hizo za kazi ili ziwasaidie kuondoa manung’uniko na migogoro inayojitokeza mara kwa mara katika sehemu za kazi kutokana na kila upande kufahamu haki na wajibu unaowapasa.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwepo kwa amani na utulivu na mahusiano baina ya waajiri na wafanyakazi ambapo kwa kufanya hivyo kutaongeza uzalishaji na utoaji wa huduma sehemu za kazi na kuongeza pato lao na hivyo kukuza uchumi.

No comments: