Powered By Blogger

Thursday, June 23, 2011

Sheria ya Gharama za Uchaguzi kufanyiwa marekebisho.

Mh.William Lukuvi
Serikali imekubali kufanyia marekebisho Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa kuzingatia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo Wabunge.Hayo yalisemwa Bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mkanyageni, Habib Juma Mnyaa (CUF).

Awali, Mnyaa, alisema sheria hiyo haikushirikisha upande wa pili wa muungano (Zanzibar), kwasababu hakuna Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).Alihoji serikali ina mpango gani wa kufanyia marekebisho sheria hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuondoa mapungufu yaliyoonekana.

Akijibu swali hilo , Lukuvi, alisema serikali itaendelea kuifanyia tathimini sheria hiyo kwa kukusanya maoni ya wadau mbalimbali.Katika swali lake la msingi, Mnyaa, alitaka kufahamu kama sheria hiyo ilisaidia kuondoa rushwa wakati wa uchaguzi au iliwakinga baadhi ya wagombea na kuwatisha wengine.

Pia alitaka kujua serikali imepata uzoefu gani katika kutekeleza sheria hiyo.Lukuvi, alisema sheria hiyo ilitungwa na Bunge si kwa lengo la kumkinga mtu yeyote, bali kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unakuwa huru na wa haki.

Alisema sheria hiyo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kupunguza vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

No comments: