Powered By Blogger

Wednesday, June 15, 2011

Mtoto atekwa shuleni na kuchinjwa

Katika habari iliyolipotiwa na gazeti la Habari leo, MWANAFUNZI Doris Lutego (12) wa Shule ya Msingi Livingstone, wilayani Njombe mkoani Njombe ameuawa kinyama baada ya kuchinjwa na watu wasiofahamika, akitenganishwa kichwa na kiwiliwili chake. Habari zilizolifikia gazeti hilo( juzi jioni )na kuthibitishwa jana na Polisi Mkoa wa Iringa, zinaeleza kwamba mwanafunzi huyo, alikutwa na mkasa huo wa kusikitisha usiku wa kuamkia juzi saa 10 alfajiri.

Taarifa kutoka shuleni hapo zinadai kwamba watu wasiofahamika walivamia shule hiyo na kumteka mwanafunzi huyo. Hata hivyo haikufahamika mara moja sababu za wavamizi hao kumteka na hatimaye kumchinja mwanafunzi huyo, mkazi wa mtaa wa shule ya Uhuru, mjini Makamambo wilayani humo.

Taarifa hiyo inaonesha kwamba baada ya mwanafunzi huyo kutekwa na taarifa kuzagaa shuleni na maeneo yanayozunguka shule hiyo, jitihada za kumtafuta zilizofanywa na wanafunzi kwa kushirikiana na wananchi na viongozi wa shule hiyo hazikuzaa matunda.

Chanzo cha  habari  cha gazeti hilo, kilieleza kuwa, sehemu za mwili wa mwanafunzi huyo zilikutwa katika maeneo tofauti ya Kitongoji cha Kambarage, wilayani humo.

“Mapema Jumatatu asubuhi, ulionekana mfuko wa Salfeti nyuma ya nyumba ya Balozi wa Kitongoji hicho, ukiwa na kiwiliwili cha mwanafunzi huyo, huku kichwa chake kikikutwa karibu na nyumba ya Mwenyekiti wa Kitongoji hicho kikiwa kimehifadhiwa kwenye mfuko wa madaftari ya mwanafunzi huyo,” alisema mtoa habari wetu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarit Mangalla alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuongeza kuwa mwanafunzi huyo alikuwa akisoma darasa la tano katika shule hiyo. Mangalla alisema kuwa taarifa zilizofika Polisi juzi zilikuwa ni za kutekwa kwa mtoto huyo, huku baadhi ya meno yake na damu vikikutwa katika kitanda chake.

Kwa mujibu wa  vifungu vya 196 na 197 vya Sheria Ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekemisho mwaka 2002, ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuuwa, kusababisha mauti ya mtu mwingine. Iwapo wauaji hao watapatikana na hatia watahukumiwa kunnyongwa mpaka kufa.

No comments: