Powered By Blogger

Monday, June 13, 2011

Majambazi yaua, yapora Mil.12 Muhimbili.

WATU wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, jana asubuhi walivamia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam,wakampiga risasi na kumuua mlinzi wa hospitali hiyo, Juma Nagungu, kisha kupora fedha kiasi cha zaidi ya Sh milioni 12. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha tukio hilo lilitokea majira ya saa mbili asubuhi jirani na eneo la mapokezi na kusababisha hofu kwa watu mbalimbali wakiwemo wagonjwa, kufuatia risasi zilizofyatuliwa na majambazi hao.

Eligaesha alisema, awali Nagungu na wafanyakazi wawili wanawake wa Idara ya Fedha hospitalini hapo, walikuwa wakizihamisha fedha hizo ambazo ni makusanyo ya siku za mwisho wa wiki kuanzia Ijumaa kutoka mapokezi kwenda idara ya uhasibu.

Amesema walipokaribia kufika huku wakiwa ndani ya gari aina ya Nissan lenye namba za usajili SU 36713, ghafla walishambuliwa kwa risasi ambayo mojawapo ilimpiga sehemu za mbavuni mlinzi na wao kuzipora fedha hizo zilizokuwa kwenye mkoba kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wametoka kuzichukua kisha kutoweka nazo.

“Lengo ilikuwa wazikusanye fedha hizo na zingine zilizokuwamo ndani ya idara ya uhasibu ili wazipeleke benki kwa pamoja, lakini kwa bahati mbaya kabla hawajafika nazo tukio hilo likatokea,” amesema Eligaesha.

Kwa mujibu Eliegesha, mlinzi huyo alifariki dunia muda mfupi wakati wakimuwahisha kitengo cha dharura kwa ajili ya matibabu na kuongeza kuwa majambazi hao walikimbia kwa kutumia mlango wa kawaida wa kutokea magari. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Faustine Shilogile, alisema hakuna mtu anayeshikiliwa kufuatia tukio hilo huku upelelezi ukiendelea.

Alisema hadi Polisi wanafika katika eneo hilo majambazi hao walikuwa tayari wameshakimbia na bila kujua mahali walikoelekea.

No comments: