Powered By Blogger

Thursday, May 26, 2011

Wauhumiwa wa EPA wawasilisha rufani yao.

Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala Hussein waliohukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia kwa njia isiyo halali Sh1.8 bilioni, kutoka katika  Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania, wamewasilisha rufani kupinga hukumu hiyo.

Rufani hiyo iliwasilishwa jana na wakili wa utetezi Majura Magafu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kile alichodai kuwa wateja wake hawakurishwa na hukumu hiyo.Alisema kwa sababu hiyo, wameamua kukata rufani katika Mahakama Kuu ya Tanzania, ili ikibidi itengue hukumu hiyo na wateja wake waachiwe huru.

Hukumu dhidi ya warufani hao ilitolewa Jumatatu iliyopita na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mgeta, ambaye alifanya hivyo kwa niaba ya jopo la mahakimu watatu.
Mahakimu wengine waliosikiliza kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi ni Focus Bampikya na Saul Kinemela.

Katika hukumu hiyo, hakimu huyo alisema mahakama ililiridhika kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo. Washtakiwa katika kesi hiyo walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manane ambayo ni kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanyifu.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa walijipatia  Sh 1.8 bilioni kutoka katika akaunti ya Epa baada ya kuonyesha kuwa kampuni yao ya Kiloloma & Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la Kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India.Katika  hukumu hiyo, iliamuriwa kuwa baada ya kifungo, washtakiwa watalazimika kurejesha Sh 1.8 bilioni  walizochukua na kwamba vinginevyo, watafilisiwa mali zao.

No comments: