Powered By Blogger

Friday, May 27, 2011

Takukuru yagonga mwamba kwa Mwakalebela na mkewe.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imegonga mwamba kwa mara ya pili, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, kutupilia mbali kesi ya kutoa rushwa katika mchakato wa kura za maoni ndani yaCCM, iliyokuwa ikimkabili kada wa chama hicho, Frederick Mwakalebela na mkewe Selina.

Mwakalebela alikuwa mshindi wa kwanza katika kura za maoni zilizoendeshwa na CCM Manispaa ya Iringa, mwezi Agosti mwaka jana, lakini vikao vya juu vya chama hicho viliondoa jina lake kwa tuhuma za kutumia rushwa.

Katika kesi hiyo, Mwakalebela na mkewe Selina, kwa pamoja walikuwa wakituhumiwa kutoa hongo ya Sh. 100,000 kinyume cha sheria namba 15 (1) , (b) ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambayo inasomwa kwa pamoja na kifungu cha 21 (1) , ( a) na 24 (8) ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.

Akisoma uamuzi mdogo wa mahakama kuhusu pingamizi lililo wasilishwa mahakamani hapo na Takukuru, Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, Mary Senapee, alisema baada ya kupitia kwa kina pingamizi lililowekwa na upande wa utetezi na kusikiliza maelezo ya upande wa mashataka, ameridhika na hoja zilizotolewa na upande wa utetezi na hivyo haoni haja ya kuendelea na shauri hilo.

Mwakalebela akiwa Mahakamani
Hakimu Senapee alitupilia mbali shtaka hilo huku akitoa uhuru kwa Takukuru kukata rufaa Mahakama Kuu kama hawajaridhika na uamuzi wa mahakama hiyo.Takukuru iliwakamata kwa mara ya pili washitakiwa hao mwezi Machi mwaka huu, na kuwafungulia upya mashataka chini ya hakimu mwingine, baada ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika shtaka la awali ambapo ilibainika kuwa walifunguliwa shitaka moja kwa kutumia sheria mbili tofautiHata hivyo, kitendo cha kulirejesha tena mahakamani hapo shtaka hilo kuliwekewa pingamizi la kisheria na upande wa utetezi kupitia wakili wa Mwakalebela na Mkewe, Basil Mkwata ambaye amesisitiza kuwa Takukuru walifungua shitaka jingine kwa makosa yale yale na kusema kuwa sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 inasisitiza makatazo ya kimaadili na hivyo makatazo sio makosa ya jinai kisheria. CHANZO: NIPASHE

No comments: