Powered By Blogger

Wednesday, May 25, 2011

…Mbunge, AG warushiana maneno kuhusu Katiba


                        MBUNGE wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka

MBUNGE wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, wamezozana hadharani wakipishana maneno kuhusu Muswada wa Mabadiliko ya Katiba.

Mzozo huo ulizuka wiki iliyopita baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, kutoa utangulizi wa mada ya Mabadiliko ya Katiba kwenye mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (Alat) uliofanyika Kunduchi, Dar es Salaam.Kombani alitoa utangulizi wa mada hiyo na baadaye kumwita Masaju, ili atoe ufafanuzi kuhusu madhumuni ya muswada huo kipengele kwa kipengele, baadaye washiriki waliruhusiwa kuuliza maswali.

Baada ya Masaju kumaliza kuelezea madhumuni ya muswada huo, Sendeka alisimama na kuhoji kuhusu kauli iliyotolewa awali kwenye mkutano huo na Waziri Kombani kuwa, moja ya sababu za kuandikwa kwa Katiba mpya ni mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar iliyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Sendeka alisema mabadiliko hayo yameifanya Zanzibar kuwa nchi kamili, hivyo ni muhimu sasa kwa Watanganyika nao wadai serikali yao. “Waziri amesema moja kati ya mambo yaliyosababisha mabadiliko ya Katiba, ni mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Mabadiliko yale yameifanya Zanzibar kuwa nchi kamili. Na sisi tudai Serikali ya Tanganyika. Mwambieni Rais (Jakaya) Kikwete hivyo,” alisema Sendeka.

Hata hivyo, wakati wa kujibu maswali, Masaju alisema Zanzibar siyo nchi kwa maana ya dola, bali ni kwa maana ya mipaka.“Siyo kweli kwamba Zanzibar ni nchi kwa maana ya dola, bali ni nchi kutokana na mipaka yake,” alisema Masaju kwa hasira huku akinukuu baadhi ya vifungu vya Katiba ya Zanzibar na kuongeza:“Someni Katiba ya Zanzibar na hati za muungano.”

Baada ya Masaju kukaa, Sendeka alisimama tena na kusema: “Sawa, yaani unatujibu kwa hasira hivyo? Katiba ya Zanzibar imetoa madaraka makubwa. Zamani kwa kesi za Mahakama ya Rufaa walikuwa wakija huku (Tanzania Bara), lakini siku hizi mahakama yao ina mamlaka ya mwisho.Wewe si umesoma sheria na sisi hatujui sheria, basi tunakwenda kutunga sheria na wewe utaitumia tu. Kidumu Chama Cha Mapinduzi.”

Kauli hiyo ya Sendeka iliibua shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo, hali iliyosababisha Kombani kuingilia kati na kumtaka Sendeka kuwa mtulivu.“Lazima tujue kuwa kuna watu wa aina tofauti. Kuna watu kutoka Tarime ambao wakiulizwa kitu lazima waje juu, ila sisi wengine tunakuwa wapole tu. Kwa hiyo, Sendeka hebu jaribu kuwa mvumilivu. Hata mimi kipindi hiki cha mabadiliko ya Katiba nimejifunza kuwa mvumilivu,” alisema Kombani.

Waziri Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, aliyekuwepo kwenye mkutano huo, alidakia huku akimtania Waziri Kombani kuwa aliwahi kuolewa Tarime ndiyo maana anawajua watu wa huko.Alisisitiza kuwa Zanibar iliachwa iunde Serikali ili kulinda hadhi yake, huku Serikali ya Tanganyika ikiwekwa ndani ya Serikali ya Muungano.Habari hii Chanzo chake ni gazeti la Mwananchi.

                      

No comments: