Powered By Blogger

Wednesday, August 8, 2012

Serikali yaridhia mabadiliko Sheria ya Mafao

Picha ya mzee kutoka Maktaba


SIKU moja baada ya Bunge kupitisha azimio la kutaka kuwasilishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambao kipengele cha muda wa ukomo wa kuchukua mafao kimekuwa kikipingwa na wadau, Serikali imekubali ombi hilo.

Juzi, jioni Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), aliwasilisha maelezo binafsi akitaka muswada huo urejeshwe bungeni ili ufanyiwe marekebisho.

Jafo alitaka kupitishwa kwa azimio ili sheria hiyo irejeshwe bungeni na kufanyiwa mabadiliko ya kifungu cha muda wa ukomo wa kuchukua mafao ya mteja kutoka cha sasa, ambacho ni kati ya miaka 55 hadi 60 na kisha kimruhusu mwanachama kuchukua fao la kujitoa kabla ya umri rasmi wa kustaafu.

Akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema sheria hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na umma na kutangazwa kwa hisia tofauti na vyombo mbalimbali vya habari.

Waziri Kabaka alisema baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa Serikali, iliweka kifungu cha kufuta fao la kujitoa kutokana na mifuko mingi ya jamii kuwa katika hali mbaya kifedha.

“Wengine walisema NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii) iko hatarini kufilisika baada ya Serikali kushindwa kulilipa shirika hilo kutokana na uwekezaji mbaya uliofanywa,” alisema Kabaka.
Kabaka alisema wapo waliodai kuwa hatua hiyo ya Serikali ina lenga kutunisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili baadaye ichukue fedha hizo kwa ajili ya chaguzi mbalimbali.

Alisema sababu zote hizo hazikuwa sahihi na kwamba Serikali inachokiona ni kuwa haikutoa elimu ya kutosha kabla ya kuwasilisha muswada huo wa sheria Aprili, mwaka huu.

“Serikali imesikia malalamiko ya wafanyakazi na hoja za wabunge na kuzingatia yote yaliyopo katika azimio la Bunge na imekubali kuleta muswada kwa hati ya dharura,” alisema Kabaka.
Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, imeishauri Serikali kuirekebisha sheria hiyo haraka kwa vile imeleta mtafaruku mkubwa kwa wafanyakazi.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama alisema imebaini kuwa sheria mpya ilianza kutumia hata kabla ya kutungwa kwa kanuni zake.

Kutokana na upungufu huo, kamati hiyo imependekeza kurejeshwa kwa fao la kujitoa na mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kulipia mkopo wa nyumba.

Kamati hiyo imependekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo ili mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kwa ajili ya kugharimia shughuli nyingine yoyote kwa lengo la kuandaa mazingira mazuri ya maisha baada ya kustaafu.

Kuwasilishwa kwa maelezo binafsi ya Jafo yaliyosababisha Bunge kupitisha azimio lake juzi jioni na maelezo ya Waziri Kabaka kulizima mjadala mkali uliotarajiwa kuibuka bungeni hiyo jana.

Wabunge wengi walikuwa wamepanga kukwamisha bajeti ya wizara hiyo endapo Serikali ingeshikilia msimamo wake wa kukataa kuleta muswada huo bungeni katika Bunge lijalo.

Sheria hiyo iliibua chuki na hasira za wafanyakazi nchi nzima, huku baadhi ya vyama vya wafanyakazi vikijiandaa kuendesha maandamano na migomo nchi nzima kupinga sheria hiyo. Chanzo gazeti la Mwananchi.

No comments: