Powered By Blogger

Friday, August 19, 2011

Wakili maarufu asomewa mashtaka kitandani, anyimwa dhamana, asota magereza.

HATIMAYE wakili maarufu nchini, Mediam Mwale, anayekabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwamo uhujumu uchumi na kupatikana na fedha haramu zaidi ya Sh18 bilioni, amekabidhiwa idara ya magereza baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.

Habari zilizopatikana kutoka polisi na magereza mkoani hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, zinadai mtuhumiwa huyo alipelekwa mahabusu ya gereza la Kisongo, nje kidogo ya Manispaa juzi baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika.Baada ya kukamilisha taratibu hizo, Mwale alichukuliwa na kupelekwa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha lililopo Kisongo hadi kesi yake itakapotajwa Agosti 31, mwaka huu.

Wakili Mwale alisomewa mashtaka 13 akiwa wodini Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, alikokuwa amelazwa baada ya kuugua akiwa mikononi mwa polisi, baada ya mahakama kukataa kupokea hati ya awali mashtaka iliyokuwa na makosa kisheria.

Mwale anatarajiwa kufikishwa mahakamani tena Agosti 31, mwaka huu kesi yake itakapotajwa, anadaiwa kughushi nyaraka mbalimbali na kufanikiwa kujipatia kiasi hicho kikubwa cha fedha, kinyume cha sheria kati ya Januari mwaka jana hadi Julai mwaka huu.

Hati ya mashtaka inataja kosa la kwanza hadi la tatu kuwa, ni kughushi na kuorodhesha majina na kampuni sita zilizotumiwa na mshtakiwa kuhamishia fedha hizo kwa nyakati tofauti kuwa, ni Oliva Green, Nyamao Mbeche Hollo, Gregg Motachwa, Ogembo Meetchel, John H.Adam na Mosoto O. Hoye.
 
Mashtaka ya uhujumu uchumi yanadaiwa kutendeka kuanzia Februari 16, mwaka jana, Wakili Mwale anadaiwa kuhamisha Sh1.9 bilioni kati ya Kampuni ya Ogambo Chacha na Gregg Motachwa Mwita.

Shtaka la nne anadaiwa kuwa Machi 5, mwaka jana, alihamisha dola 200,000 za Marekani wakati shtaka la tano lililotendeka Machi 30, mwaka huohuo alihamisha dola 159,500, huku katika shtaka la sita anadaiwa kuhamisha dola 5,500 Septemba 27, mwaja jana.

Shtaka la saba anadaiwa kuwa, Novemba 2, mwaka jana alihamisha zaidi ya dola 1.2 milioni, kabla kufanya hivyo tena Desemba 21, mwaka huohuo alipohamisha dola 416,000 na kumalizia mwaka kwa kuhamisha dola 521,000 Desemba 24, 2010.

Januari 17, mwaka huu alihamisha dola 808,000 na Februari 9, alihamisha dola 527,000 kabla ya kukamilisha zoezi hilo Julai 13, mwaka huu kwa kuhamisha zaidi  Sh300 milioni.

Katika hatua nyingine, mahakama imeamuru polisi kurejesha mali za mshtakiwa ikiwamo gari la kifahari aina ya BMW na simu ya kiganjani baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Charles Magesa, anayesikiliza shauri hilo kukubaliana na ombi la Wakili wa utetezi, Loomu Ojare kuwa hazijaorodheshwa kwenye hati ya mashtaka.



No comments: