Powered By Blogger

Wednesday, July 27, 2011

WENJE ATOLEWA KWA NGUVU, MBUNGE CCM ANUSRIKA KUPIGWA

Wabunge katika zogo
MBUNGE wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, jana alijikuta akitolewa bungeni na askari (wapambe) wa Bunge waliotii amri ya Mwenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba, aliyeongoza kikao siku hiyo.Katika tukio ambalo ni la kwanza kutokea tangu kuanza kwa Bunge la Kumi linaloongozwa na Spika Anne Makinda, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alinusurika kupigwa na wabunge wa kambi ya upinzani baada ya kuwakejeli Chadena akisema waache mambo ya kitoto.

Mabumba alitoa amri ya Wenje kutolewa nje baada kukaidi amri ya Mabumba kumtaka akae chini mbunge huyo wa Nyamagana alipokuwa akiomba mwongozo, katikati ya mabishano yaliyokuwa yakiwajumuisha wabunge wengine wakati huo.Wakati Wenje akisisitiza kuomba mwongozo kwa maelezo kwamba jambo analotaka kusema "lina maslahi ya nchi", Mabumba ghafla aliwaita askari (wapambe) wa Bunge na kuwaamuru wamtoe nje kwa kukiuka kanuni za Bunge.

Kabla ya kuwaita askari hao, Mabumba ambaye ni Mbunge wa Dole alikuwa amemwamuru mara tatu Wenje akae chini, lakini hakutii akisema: "Nina jambo la dharura ambalo ni kwa maslahi ya Taifa"."Sargent Ant Arms, mtoe nje mheshimiwa Wenje," alisema Mabumba na hapo askari watatu waliingia na kumtoa nje Wenje, tukio ambalo liliacha kukiwa hakuna utulivu bungeni.

Pamoja na kusindikizwa na askari wa Bunge, baadhi ya wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi walitoka nje wakimsindikiza Wenje.Walipofika nje ya ukumbi wa Bunge walianza kumlalamika kwamba, Mabumba ameshindwa kuongoza Bunge na kudai kuwa anaonyesha upendeleo wa wazi katika uendeshaji wa vikao vya chombo hicho.

Nje ya Ukumbi wa Bunge
Nje ya Ukumbi wa Bunge ilizuka tafrani nyingine iliyosababisha Mbunge Filikunjombe (CCM), kunusurika kupokea kichapo kutoka kwa wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi baada ya kuingilia mazungumzo yao wakati wanajadili suala la Wenje kutimuliwa ukumbini.

“Tatizo lenu ninyi wabunge wa Chadema mnaishia kuwa wabishi kila wakati, jambo ambalo linawapotezea heshima kwa wananchi,’’ alisema Filikunjombe na kuongeza: “Acheni mambo ya kitoto rudini ndani kuendelea na Bunge. Sio kila siku ninyi Chadema tu, watu wamewachoka.’’

Kauli ya ilikuwa kama kumwaga petroli kwenye moto, kwani kundi la wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi ambao kwa wakati huo wakiongozwa na Moses Machali (Kasulu Mjini NCCR), walimvaa kama nyuki mbunge huyo na kuanza kurushiana maneno makali.

“We mjinga kweli, hapa sio wabunge wa Chadema hata sisi wa NCCR-Mageuzi tupo tunachojadili ni maslahi ya nchi sio ushabiki wa vyama, toka hapa mshamba wewe,’’ alisema Machali.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Kiwanga, alimwambia Filikunjombe aache hadithi za kijinga kwani wananchi wa eneo lake wanaporwa chuma, lakini yeye (Filikunjombe) anashindwa kuwatetea badala yake anarukia mambo yasiyomuhusu.“Tuondolee ujinga wako hapa, wananchi wako katika maeneo ya Liganga wanaporwa mali usiku na mchana unashindwa kuwatetea leo unapotuambia tuna akili ya kitoto, hivi unataka Watanzania wafe ili ninyi mshangailie,’’alisema Kiwanga.
Wabunge wengine waliomwandama zaidi Mbunge huyo ni, Machali (NCCR-Mageuzi), Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), Mariam Msabaha na Susan Kiwanga wote wa Viti Maalum (Chadema) ambao walimzingira mbunge huyo na kuanza kumrushia maneno ya kejeli.Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya wabunge wengine wa Chadema, Godbles Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Vicent Nyerere (Musoma Mjini) walipoingilia ugomvi huo na kutaka Filikunjombe awaombe radhi, lakini alikataa.Kama si busara iliyotumiwa na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM) hali ingekuwa mbaya kwani idadi ya wabunge wa Chadema ilipozidi yalisika maneno kuwa mbunge huyo apigwe, ndipo Nkamia alipofika na kuokoa jahazi akimtaka Filikunjombe aondoke katika eneo hilo.Chanzo Gazeti la Mwananchi.

No comments: