Powered By Blogger

Thursday, July 28, 2011

TUNDU LISSU,LEMA NA BABA MCHUNGAJI WATIMULIA BUNGENI.

Mh.Job Ndugai( Naibu Spika)

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwatimua kikaoni wabunge watatu wa Chadema. Wabunge hao waliofukuzwa bungeni jana asubuhi ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Tundu Lissu (Singida Mashariki).Walifukuzwa kutokana na kile Naibu Spika Ndugai alichoeleza kuwa ni kukiuka Kanuni za Bunge zinazowataka kutozungumza chochote ndani ya bunge bila idhini ya kiti cha spika. 

 Tukio la kufukuzwa kwa wabunge hao limekuja siku moja baada ya mmoja wa wenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba, kumfukuza bungeni Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema),  baada ya kukaidi amri iliyomtaka akae chini wakati akiomba mwongozo.Wakati tukio hilo la juzi likiwa limeonyesha taswira mbaya kwa mhimili huo wa dola wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali,  jana Lissu, Lema na Msigwa kwa pamoja walipewa adhabu hiyo baada ya kubishana na Ndugai bila utaratibu.

Katika tukio hilo, wabunge hao walipinga kile walichokiita  muda mrefu aliokuwa amepewa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kueleza kukiukwa kwa kanuni za Bunge.Lukuvi aliomba kupewa mwongozo wa Naibu Spika mara baada ya Lema ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kusoma hotuba ya maoni ya kambi ya upinzani kuhusu wizara hiyo ambayo ilikuwa na shutuma nyingi dhidi ya Serikali, hasa Jeshi la Polisi

 "Mwongozo wa Spika, mwongozo wa Spika........Mheshimiwa Naibu Spika sasa......," alisikika sauti ya Lissu wakati Lukuvi akiendelea kuzungumza, hali iliyosababisha Naibu Spika kusimama na kumuonya. 

 "Nimesema hairuhusiwi kuwasha mic (kinasa sauti) yako bila ruhusa yangu...waziri endelea...." alisema Ndugai Baada ya kauli hiyo, ndipo vipaza sauti ambavyo haikuwa rahisi kufahamu idadi yake viliwashwa na sauti kuanza kusikika zikimkosoa Ndugai kwamba anapendelea, kwani Lukuvi alipewa muda mrefu wa kuomba utaratibu tofauti na msimamo wa awali aliokuwa ameutoa Naibu Spika huyo

 "Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ..." ilisikika sauti ya Msigwa huku sauti nyingine kadha wa kadha zikisikika bila mpangilio hali iliyosababisha taharuki na kuathiri shughuli za Bunge. Sauti hizo zilisababisha mzozo na kukosekana kwa utulivu na usikivu bungeni hivyo Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM) akaamua kutumia rungu lake kuwafukuza wabunge hao watatu kutoka ndani ya Ukumbi wa Bunge.

 "Nilishasema tangu asubuhi na nimewakumbusha kwamba hakuna mbunge anayeruhusiwa kuwasha microphone (kinasa sauti) na kuzungumza bila idhini ya kiti, sasa naanza kutumia kanuni, nimewaona wabunge watatu, Mheshimiwa Lissu, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa na Mheshimiwa Lema, tokeni nje," aliamuru Ndugai na kuongeza:

"Tena nitafuatilia kuhakikisha kwamba mnaondolewa kabisa nje ya geti (lango kuu) la kuingilia bungeni, muondoke kabisa katika eneo hili."

Kufuatia kauli hiyo, wabunge hao walitoka nje huku wakisindikizwa na askari (wapambe) wa Bunge hadi nje ya ukumbi na baadaye kuondolewa kabisa katika eneo hilo, hivyo kutokuwa na fursa hata ya kuzungumza na waandishi wa habari

 Tafrani hiyo ilishuhudiwa na IGP Mwema pamoja na wakuu wa taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo jana iliwasilisha hotuba yake kwa mwaka 2011/2012.

 Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, wabunge hao jana hawakuruhusiwa kurejea tena bungeni siku hiyo, badala yake watarejea leo kwani adhabu yao ni kukosa kikao kwa siku moja tu.

No comments: