Powered By Blogger

Monday, June 20, 2011

Muasia aliyeficha maiti sandukuni ahukumiwa kunyongwa hadi kufa.


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania,Kanda ya Dar es salaam imemhukumu mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia, Vinoth Plavin Nadhesan, kunyongwa kwa kamba hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumwua mwenzake kwa kumchoma visu na mishale. Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Faudh Twaibu, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.

Jaji Twaibu alisema mazingira ya kesi yanaonesha kuwa mshitakiwa alimwua Abdulbassit Abdallah, mkazi wa Dar es Salaam, kwa kukusudia na si kwa kujitetea kama anavyodai. “Mshitakiwa amepatikana na hatia ya mauaji na hukumu yake ni kunyongwa kwa kamba hadi kufa, kama hajaridhika na uamuzi huu ana haki ya kukata rufaa,” alisema

Alisema Mahakama inaamini taarifa za Polisi kuliko ushahidi wa upande wa utetezi uliotolewa mahakamani hapo, kuwa Abdallah ndiye aliyeanzisha ugomvi kwa kumpiga Nadhesan kwa fimbo, kwani ushahidi huo kwa mujibu wa Jaji Twaibu, ni wa kujitetea. Kwa mujibu wa taarifa za Polisi zilizotolewa mahakamani hapo kwa ajili ya ushahidi, mshitakiwa alikiri kuua katika kituo cha Polisi na mbele ya shahidi na wakati akikiri, alimtaka askari asipeleke shahidi wakati akitoa maelezo yake.

Kwa mujibu wa ushahidi huo wa Polisi, Nadhesan alisema hahitaji shahidi wakati wa kutoa maelezo yake Polisi, kwa kuwa wakati anaua, alikuwa peke yake na aliamua kumweleza ukweli askari huyo kwa kuwa alimjali.

Awali ilidaiwa mahakamani kuwa Februari 6 katika eneo la Kariakoo mtaa wa Kipata, Nadhesan alimwua Abdallah kwa kumchoma na visu vya jikoni.

Mbali na kumchoma visu hivyo, Nadhesan pia alimchoma Abdallah na mshale mgogoni, tumboni, shingoni na mdomoni na kuuweka mwili wake kwenye begi na kulitelekeza ndani ya gari katika maegesho ya magari ya jengo la JM Mall (Habour View).

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, chanzo cha ugomvi huo ni fedha na ulianza Abdallah alipomkopesha mshitakiwa dola 20,000 za Marekani, kwa makubaliano ya kumlipa baada ya mwaka mmoja. Katika utetezi wake, Nadhesan alidai kwamba Abdallah ndiye aliyeanzisha ugomvi kwa kumpiga fimbo na ngumi na katika kujitetea, alichukua kisu na kumchoma nacho.

Nadhesan alijitetea kwamba alipoona Abdallah anapiga kelele, alimchoma mshale kwa kuhofia kwamba kama angenyanyuka, yeye angekuwa hatarini. Ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulionesha kuwa mwili wa marehemu ulikutwa na vipande vya mishale mdomoni. Kwa Mujibu wa vifungu vya 196 na  197 vya Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 kama ilivyofayiwa marekebisho mwaka 2002, ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kuua au kusababisha mauji wa mtu mwingine. Mtu yoyote anayetiwa hatiani na kosa la mauaji adhabu yake ni kuhukumiwa kunyongwa mpaka Kufa. Hata hivyo hukumu hiyo ya kifo japokua kwa miaka ya hivi karibuni haijaekelezwa kwa muuaji yeyote inapingwa kwa kiasi kikubwa na wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu nchini na duniani kwa ujumla, kwamba inakinzana na kifungu cha 14 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inyobainisha ya kwamba Kila mtu anay haki ya kuishi.

Nadhesan alikamatwa na Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Februari 7 akijiandaa kutoroka kwenda India.

No comments: