Powered By Blogger

Monday, June 20, 2011

Kituo cha sheria kutetea waliouawa kinyama Selous


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimejitosa katika sakata la mauaji ya wanakijiji wawili wa Cholesamvula ambayo yanadaiwa kufanywa na  askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Selous mkoani Pwani Februari mwaka huu.Akizungumza Dar es Salaam jana, Mtafiti msaidizi wa kituo hicho, Pasience Mlowe alisema hivi sasa polisi Pwani inawasiliana na ofisi za hifadhi hiyo zilizopo Morogoro ili kuweza kuwatia mbaroni watuhumiwa.

Alisema wameanza kulishughulikia suala hilo ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanafikishwa mbele ya sheria ili haki itendeke na wiki iliyopita walikuwa Kijiji cha Kwala kupata ukweli kuhusiana na sakata hilo ambako walizungumza na Kigwiso Mfanyeje ambaye alinusurika katika tukio hilo.“Tulienda kijijini walipokuwa wanaishi marehemu na kuzungumza na watu wengine na tumefanya mawasiliano na mkuu wa upelelezi wa wilaya pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani ambao wametoa ushirikiano mkubwa”alisema Mlowe.

Alisema wamewasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema na barua imepatikana kutoka ofisi hiyo kwenda ya wanyamapori ambayo ipo Morogoro na wakati wowote watuhumiwa watatiwa mbaroni ili manusura wa tukio hilo, Mfanyeje aweze kwenda kuwatambua.“Unajua polisi wana namna zao za utendaji kazi na ilipofikia ni kuwa barua kutoka kwa IGP kwenda Ofisi ya wanyamapori ililiyopo Morogoro imekwenda na watakuwa wameipata hivyo, wakati wowote watuhumiwa watatiwa mbaroni” alisema.

Mlowe alisema ni kweli tukio hilo lilitokea na linasikitisha na alilipongeza gazeti la Mwananchi kwa kufuatilia tukio hilo ambalo kama lisingeripotiwa pengine lingepita bila kufahamika kutokana na wakazi wa eneo hilo kudai kuwa kuna visa vingi vya watu kuuawa au kutoweka mara wanapoingia katika eneo hilo la Selous.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Absolom Mwakyoma hakuweza kupatikana kuweza kuzungumzia zaidi suala hilo na simu yake muda mwingi ilipopigwa iliita bila kupokelewa. Tukio la mauaji hayo lilitokea Februari 2 mwaka huu na katika tukio hilo watu wawili  wanadauwa kuawa askari hao.

Waliouawa ni pamoja na Hamisi Feruzi ‘Boy’na Mohamed Sutta wakati Mfanyeje Kigwiso alijeruhiwa na hadi hivi sasa ana kilema kutokana na mkono wake wa kushoto uliopigwa risasi kupoteza uwezo wa kufanyakazi.

Tukio hilo liliripotiwa Polisi Kisarawe ambao walienda hadi eneo la tukio na kukuta mabaki ya mafuvu moja likiwa limechomwa moto, viungo vingine na mabaki ya nguo ambazo ndugu wa marehemu waliokuwa katika msafara huo wa polisi waliweza kuzitambua kuwa ni za ndugu zao. Chanzo gazeti la Mwananchi.

No comments: