Powered By Blogger

Saturday, June 18, 2011

Jaji Mkuu awaonya wanasisa.

Mh. Jaji Mkuu(Mwenye suti nyeusi)akionyesha Vitabu akiwa na IGP Mwema.
VIONGOZI wa siasa nchini wametakiwa kupanda mbegu za maadili mema kwa wafuasi wao, huku wao wenyewe wakionesha mfano wa kuwa mstari wa mbele kutii sheria za nchi. Aidha, wametakiwa kuelewa, kwamba tafsiri ya kupenda nchi si kufanya harakati za kuchochea ukiukwaji wa sheria.

Hayo yalisemwa jana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu utii wa sheria bila shuruti uliofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Alisema uzinduzi wa kampeni hizo umekuja kwa wakati mwafaka, hasa katika kipindi ambacho nchi imekumbwa na matukio ya wananchi kujifanya wanadai haki, lakini bila kuzingatia wajibu walionao kisheria.

Katika hotuba yake, aliyoitoa mbele ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwamo makamanda wa Polisi wa mikoa yote nchini, wawakilishi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wa asasi za kiraia, alisisitiza juu ya utekelezaji wa kampeni hiyo kwa vitendo, kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Jaji Mkuu pia aliwataka viongozi wa dini kuelewa kwamba wana wajibu mkubwa wa kuongoza dhamira za wafuasi wao kutenda mema, kuhimiza na kulinda maadili ya jamii kwa ajili ya kujenga amani na umoja wa kitaifa.

Kwa upande wa asasi za kiraia, alisema nazo zina jukumu kubwa kwa umma wa Watanzania wanaopaswa kupewa elimu chanya ya uraia na uzalendo, huku wakitimiza maadili mema ya kitanzania.

“Wananchi wetu wakitii sheria bila kushurutishwa, watavisaidia vyombo vyenye mamlaka ya utoaji haki kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha na ufanisi zaidi.

“Aidha, kutaiwezesha jamii kuishi kwa amani, usalama na utulivu, kupunguza hali ya watu kuishi kwa mashaka na wasiwasi, kupunguza matumizi ya nguvu na kuimarika kwa uhusiano wa kiutendaji kati ya vyombo vya Dola na wananchi,” alisema Jaji Mkuu aliyeonesha kukerwa na tabia za baadhi ya wananchi kujichukulia madaraka ya vyombo vingine vya Dola kwa kuchukua uamuzi kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria.

Akimkaribisha Jaji Mkuu kuzindua kampeni hiyo, IGP Mwema alisema kampeni hiyo itakayosambaa hadi ngazi za mashina, inalenga kuwaamsha na kuwapa hamasa Watanzania kuirejea misingi ya uwajibikaji katika harakati za kudumisha amani, usalama na utulivu, kama mtaji wa kujiletea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii nchini.Chanzo gazeti la Habari leo.

No comments: