Powered By Blogger

Monday, June 27, 2011

LHRC yaomba Hati ya kuwakamata Viongozi wa Dowans:

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimewasilisha ombi chini ya hati ya dharura Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuomba itoe hati kukamatwa kwa Wakurugenzi wa Kampuni za Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited kwa kudharau amri ya Mahakama.

Maombi hayo yaliwasilishwa baada ya taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari Mei 21 mwaka huu, kuwa mitambo ya Dowans imeuzwa kwa Kampuni ya Symbion Power ya Marekani kwa thamani ya Dola milioni 120.Maombi hayo yaliwasilishwa na wakili wao LHRC Dkt. Sengondo Mvungi, kupitia hati ya dharura.

Jaji anayesikiliza kesi ya kuomba kusajiliwa kwa tuzo ya Dowans, Bi. Emilian Mushi, Machi 3, mwaka huu alitoa amri kutaka pande zote mbili katika kesi hiyo kutogusa lolote linalohusiana na kampuni hizo.

Katika amri hiyo ya Mahakama iwapo upande wowowte ungehitaji kufanya lolote ni lazima kwanza waombe kibali cha mahakama.Kituo hicho ni miongoni mwa wanaopinga Mahakama Kuu ya Tanzania kusajiliwa kwa Tuzo ya Dowans ya sh. bilioni 94 iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).

Kituo hicho kinaomba pia mahakama itoe amri ya kuwataka wadaiwa hao waweke Dola za Marekani milioni 120 kama dhamana na kulipa gharama za kesi hiyo.

Mbali na LHRC Mwandishi wa Habari Mwandamizi Bw.Timoth Kahoho, naye amewasilisha maombi kama hayo.Bw.Kahoho naye ni miongoni mwa wanaopinga tuzo ya Dowans isisajiliwe pamoja na Shirika la Umeme (Tanesco).

Januari 25 mwaka huu Dowans iliwasilisha ombi la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania isajili tuzo waliyopewa na ICC na siku chache baadaye Tanesco, LHCR na Bw.Kahoho waliwasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe.

ICC ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco, Novemba 15, mwaka jana, na kutaika  iilipe fidia ya fedha ambazo kwa tahamani ya fedha za kitanzania ni takriban bilioni 94.Chanzo gazeti la Majira.

No comments: