Powered By Blogger

Wednesday, April 27, 2011

Kashfa na athari zake katika sheria."Defamation"


SHERIA kwa ujumla wake inazingatia na kutegemea kwamba kila mtu ana haki ya kuwa salama na kwamba mawazo ya watu wengine yatolewe kwa kuzingatia taratibu na sheria ili kwamba mawazo au mtazamo wa watu hao usimuumize mlengwa.

Hivyo basi kutoa maneno yenye lengo la kumdhalilisha, kumuumiza au kumfanya mtu aonekane kwamba hafai mbele ya watu wanaomheshimu na jamii nzima kwa ujumla (kashfa) ni kosa katika sheria.
Kashfa hapa nchini inazungumziwa katika Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, hususan kifungu cha 38 mpaka cha 47. Kwa tafsiri, kashfa ni tamko la maneno ya mdomo au maandishi lililo na lengo la kujeruhi kuvunja hadhi ya mtu fulani katika jamii kwa minajili ya kumfanya achukiwe au kudharauliwa.
Zaidi ya hapo, mahakama katika maamuzi mbalimbali imetafsiri kashfa kwa namna tofauti lakini ikiwa na msingi mmoja. Kwa mfano, katika shauri la Hamisi dhidi ya Akilimali, (1971) HCD, 111 mahakama ilitamka kwamba kashfa ni kuwasilisha akilini mwa mtu mwingine masuala ambayo si ya kweli na yakiwa na uwezekano wa kusababisha kuharibika hadhi ya mtu au watu.

Hivyo basi ndugu msomaji, kuna mambo kadhaa yanayohitajika kuthibitika ili tamko litafsiriwe kama kashfa, mojawapo ni kwamba tamko hilo liwe la kashfa maana yake, mahakama itatakiwa kutafsiri maneno hayo kwa kuzingatia usawa na maana halisi ya neno lenyewe kama mtu mwenye uelewa wa kawaida anavyoweza kulitafsiri neno au tamko hilo.

Kwa hiyo, kiwango cha kupima neno au tamko kama ni kashfa au la ni kwa kumuangalia mtu wa kawaida angelichukuliaje neno au tamko hilo.Hili ni suala la msingi kwa kuwa maneno mengine yakichukuliwa katika mazingira yalipo tamkwa au kuandikwa hayawezi kuhesabika kama ni kashfa ingawa wakati mwingine maneno hayohayo yakitamkwa au yakiandikwa yanaweza kuhesabika kama kashfa.

Kitu kingine ambacho kinatakiwa kuthibitishwa ili neno au maneno yahesabike kwamba ni kashfa ni kwamba maneno hayo yalilengwa kwa mdai na siyo mtu mwingine. Hapa ndugu msomaji, sheria inahitaji mdai awe ametajwa moja kwa moja katika maneno hayo ya kashfa.

Ikiwa vinginevyo mahakama haitahesabu kwamba mdaiwa alikusudia kumtaja mtuhumiwa. Katika shauri la P.M Jonathan dhidi ya Athuman Khalfan, (1975)LRT,65 ambapo mdaiwa aliandika barua kwa Jaji Mkuu na kutoa tamko la mdomo katika tume ya uchunguzi na kwa Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa mkoa wa Dodoma akimshtumu mdaiwa ambaye alikuwa Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi ya mdaiwa na mtu mwingine kwamba amependelea upande mmoja,mla rushwa na asiyefuata maadili.Wakati kesi ikiendelea, swali lilikuwa kama barua ya mdaiwa kwenda kwa Jaji Mkuu na tamko la mdomo kwa RCO ilikuwa ni kashfa. Mdaiwa katika utetezi wake mahakamani, alidai kwamba hakutaja jina lolote Katika tume na kwamba kwa RCO, ushahidi ulionesha kwamba ilikua baada ya kualikwa na mdai mwenyewe.

Katika maamuzi yake mahakama iliamua miongoni mwa mengineyo kwamba pale mdai akitoa taarifa moja kwa moja au kupitia mtu au kitu kingine na taarifa hiyo ikawa ni kashfa basi tamko hilo halitahesabika kuwa ni kashfa kwa kuwa mdai amefanya hivyo kwa kutaka mwenyewe au kwa maneno ya kisheria volent non fit injuria.

Hivyo kwa kuangalia jinsi taarifa inavyotolewa kuna aina mbili za kashfa. Aina ya kwanza ni kashfa inayotolewa kwa njia ya maneno ya mdomo au kwa lugha ya kisheria "slander." Katika aina hii, mdaiwa anatamka maneno yenye lengo la kumchafua na kumdhihaki mdaiwa akitumia maneno ya mdomo.Hii ni aina ya kashfa ambayo kitu kilichotumika kusambaza maneno hayo ya kashfa ni cha muda mfupi na kinasikika kwa masikio. Aina ya pili ni kashfa inayotolewa kwa njia ya maandishi au kwa lugha ya kisheria "libel 
Maandishi hayo yanaweza kuwa katika machapisho, kuchora, mwanasesere au kuchapa maneno yoyote yakiwa na lengo la kumkashifu mtu mwingine. Hivyo aina hii ya kashfa ni ile inayokuwa katika chombo cha kudumu (kama gazeti, jarida, kaseti) na maneno hayo yanaonekana kwa macho sio kusikika kwa masikio.
Hata hivyo kashfa ya maneno ya mdomo itahesabika pale tu itakapothibitika kuna madhara ya kipekee (ya kifedha) ambayo mdaiwa amepata kutokana na maneno hayo ya kashfa. Maneno hayo yanatakiwa yatambuliwe na kuthaminishwa na mdai mwenyewe.

Hata hivyo ndugu msomaji unatakiwa kujua kwamba kashfa ya maneno ya mdomo haitahesabika ikiwa tu maneno yaliyotamkwa yatahesabika ni kosa la jinai linaloadhibiwa kwa kifungo au inahusiana na maneno ya magonjwa ya kuambukizwa kwa lengo la watu wengine wasijihusishe na mdaiwa au kama maneno hayo ni yale yanayozungumzia ushoga, usagaji, uzinifu au kama ni kuhusiana na ushirikina.

Wakati mwingine kuna kashfa kwa kutumia katuni, picha au maneno ambayo ukiyaangalia yenyewe hayana madhara kwa hadhi ya mtu lakini yakiwa na uwezo wa kumkashfu mdai kwa mfano, katika kesi ya Thanker dhidi ya B.G Chipungahelo,[1965],EA,82 ambapo gazeti liliripoti ajali ya gari iliyomhusisha mtuhumiwa na kwamba katika gari hilo kwa mujibu wa gazeti kulikuwa na chupa ya pombe ya Brandy kitu ambacho kilikuwa na lengo la kumuonyesha mdai kama mtu mlevi.

Kwa upande wa adhabu dhidi ya kashfa, sheria imetoa adhabu kadhaa kwa mtu atakayethibitika kuwa ametoa maneno ya kashfa mojawapo ni kwa mdaiwa kutakiwa kumlipa fidia mdai au mhanga wa kashfa.Hapa mahakama itazingatia nakala ngapi za taarifa hiyo ya kashfa zilichapishwa eneo ambalo taarifa hiyo ya kashfa ilizunguka (ukubwa wa eneo, je ni mkoa, nchi au nje ya mipaka ya nchi).Adhabu nyingine kwa mdaiwa ni kukatazwa kuchapishwa tena kwa taarifa hizo katika gazeti, jarida au runinga. Adhabu nyingine inaweza kuwa kwa mdaiwa kuamriwa na mahakama kumuomba radhi mdaiwa katika njia ileile aliyoitumia kumkashfu.

Mara nyingi kama ni jarida au gazeti, mdaiwa atatakiwa kuandika taarifa tena ya kuomba radhi ukurasa wa kwanza na kwa maandishi makubwa. Na Allan Kajembe.

No comments: