Powered By Blogger

Monday, May 7, 2012

MTAZAMO WANGU KATIKA DHANA KWAMBA RAIS AMEVUNJA KATIBA KATIKA UTEUZI WAKE WA MAWAZIRI


Siku chache zilizopita Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliteua Baraza lake la mawaziri.Baraza hilo limekuja baadbaadhi ya mawaziri, kushutumiwa kwa utendaji mbovu wa shughuli zao na kila siku na kutumia mamlaka yao aidha kujinufaisha au kufisadi mali ya Umma. Kimsingi,lengo langu si kudadisi kwa kina sababu zilizopelekea Mh.Rais kufanya mabadiliko hayo. Nimehamasika kuandika suala hili baada ya vyombo mbalimbali vya habari, wanazuoni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kua namaoni tofauti, wengine wakienda mbali sana na kusema Rais amevunja kaika kwa kuwachagua baadhi ya Mawaziri kushika wadhifa huo wakati wao si wabunge. Niseme kwamba katika maoni yangu hayo nitarejerea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania(1977), kama "Katiba".

Kimsingi, nikiwa Mwanasheria nimeona si vibaya nikitoa mawazo yangu katika mkanganyiko huu ambapo jamii isiyo na uelewa wa kisheria” layman”, huweza kukumbwa na mkanganyiko usiostahili katika jambo hili. Mfano katika gazeti la mtanzania la leo Jumapili, lilimnukuu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) likiwa na kichwa cha habari” MBOWE AMSHUKIA JK, ADAI AMEVUNJA KATIBA UTEUZI WA MAWAZIRI”. Katika gazeti hilo lenye namba. ISSN 0856-5678 Toleo Na. 6049, gazeti hilo lilimnukuu Mh.Mbowe akisema mafuatayo,” inasikitisha Kuona Rais anaendesha nchi kihuni na kuvunja kwa makusudi Katiba,wakati akifahamu kuwa hawezi kumpa mtu uwaziri bila kuapishwa ubunge na kwamba kwa hatua hiyo Rais Kikwete ameridharau bunge.

Niaze kueleza kwamba Ibara ya 66(1) e kinatoa Mamlaka ya Kikatiba kwa Rais kuteua wabunge wasiozidi 10 wenye sifa atakazoona inafaa kuitumikia nafasi hiyo, sanjali na mamlaka hayo aliyopewa Rais aina nyingine ya mtu kuwa Mbunge pia zinaainishwa katika Ibara hiyo hiyo; na kwamba mtu anaweza kua mbunge kwa kuchaguliwa na wananchi au vilevile kupitia kwa viti maalum, ay nafasi aliyonayo kama ya Mwanzaasheria Mkuu wa Serikali.  Hivyo basi Uteuzi wa Rais kwa Prof. Sospether Muhongo na Bi.Jane kuwa wabunge na hatimaye uwaziri ni uteuzi wa kikatiba.

Watu wanaosema Raisi amevunja katiba, wanamaoni ya kwamba wabunge walioteuliwa na Rais kuwa mawaziri hawajaapa  kuwa wabunge kabla ya kushika na Kuteuliwa na Raisi kuwa Mawaziri. Nina wiwa kusema ya Kwamba huu ni upotoshwaji mkubwa  na pengine uelewa mdogo wa Katiba pamoja na Sheria za nchi yetu.

Kimsingi Swali la kutuongoza ni kwamba, ni wakati gani mtu anakua Mbunge? Je ni pale mtu anapotangazwa na Tume kuwa Mbunge ?AU Je ni Pale ambapo mtu anapoteuliwa na mtu mwenye mamlaka kuwa Mbunge? Au Je ni pale mtu anapokua kiapo cha Ubunge? Ni rai yangu kwamba Sura ya 343 iliyofanywa marekebisho mwaka 2002 na 2010 ,kifungu cha 98 kinasema mtu anakua mbunge pale baada ya kutangazwa na Tume ya uchaguzi kupitia kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuwa mbunge kupitia Jimbo husika, au pale mtu anapoteuliwa kwa mujibu wa Katiba kushika wadhifa huo(Kama ambavyo Rais amefanya katika Ibara ya 66(1)e). Suala la kwamba mtu huyo amekula kiapo cha kutumikia wadhifa huo wa ubunge au la! Hilo ni suala jingine. Na kuapa au kutokuapa kwa mtu huyo hakumuondolei ubunge wake( does neither disqualify him or her from holding that post nor invalidate the same). Ninachomaanisha ni kwamba Mtu anapotangazwa au kuteuliwa kuwa mbunge, mtu huyo atahesabika kuwa mbunge pale tu atakapotangazwa au kuteuliwa kushika wadhifa huo. Kwa Mfano. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni Mbunge Kikatiba kwa nafasi aliyonayo yeye kama Mwanasheria Mkuu katika Ibara ya 66(1)d na 55(5). Kama Rais akiingia Madarakani na Kumteua Mwanasheria Mkuu wa serikali, Mwanasheria huyo baada ya kuapa Kwa Rais anaanza majukumu yake kama Mwanasheria Mkuu, lakini hataanza majukumu yake kama mbunge mpaka pale atakapoanza kushiriki katika shughuli za Kibunge. Hii haina tofauti na uteuzi wa Mawaziri.

Pamoja na hayo ibara ya 68 ya Katiba inaeleza wazi kwamba, na nanukuu Kila Mbunge atatakiwa kuapishwa katika Bunge kiapo cha uaminifu kabla hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge. Kwa mantiki ya Ibara hii ni kwamba Mawaziri hao walioteuliwa na Rais ni wabunge isipokua hawawezi kushiriki katika shughuli za ubunge bila kula kiapo au pasipo kuapishwa na Bunge.  Swali la kujiuliza ni shughuli gani za bunge zinazozungumziwa na Ibara hii ya 68. Shughuli za bunge kama inavyoelezewa ni kutunga sheria pamoja na majukumu mingine ya waliyopewa Kikatiba.

Kwa upande wa Pili, Rais amepewa mamalaka ya Kikatiba katika Ibara ya 55 (1),(2),(3) kuteua Mawaziri na manaibu wao, hata hivyo mawaziri hao hawaruhusiwi kutekeleza majukumu yao ya kiuwaziri pasipo kutii masharti ya Ibara ya 56 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, inayowataka Mawaziri hao kula kiapo kwa raisi kabla ya kuanza majukumu yao.  Ningekua na maoni tofauti kama, Mawaziri hao wangeanza kufanya shughuli zao za kiutendaji kama Mawaziri kabla ya kuapishwa na Rais..hapo ndipo tungesema wamekosa uhalali wa kiutendaji kama Mawaziri.

Kwa mantiki hii basi ya tafrisi ya Kikatiba ni Kwamba Mh. Rais hajafanya kosa lolote la kuwateua wabunge hao kua Mawaziri kabla ya kuapishwa na Bunge.
Ni rai yangu kwamba, Wanasiasa waache maneno ya uchochezi kupotasha raia ilikuepuka migogoro isiyokua na tija katika Taifa. Iwapo wadau wanaona ya kwamba kuna ulazima wa Mawaziri kuapishwa na Bunge kabla ya kuanza majukumu yao ya uwaziri, basi wapeleke maoni na mapendekezo yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Sheria kutoa maoni yao, pale Tume inapoanza kupokea maoni hayo.

No comments: