Powered By Blogger

Wednesday, July 6, 2011

Wazuia maiti asizikwe, risasi zawatawanya

POLISI jijini Dar es Salaam jana ililazimika kutumia risasi kutawanya kundi la vijana lililovamia msikiti kuzuia mwili wa Bakari Hamisi aliyefariki juzi baada ya kuanguka wakati akicheza mpira katika viwanja vya Faru, Manzese, usizikwe.

Saa 7 mchana, mwili wa Hamis anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 25, ulishaandaliwa na kupelekwa msikitini kuswaliwa kabla ya kwenda kuuzikwa, lakini kundi la watu, wengi wao wakiwa vijana liliingilia kati na kwenda kufukia kaburi kushinikiza usizikwe.

Taarifa kutoka msibani zinasema, vijana hao wanadai kuwa kifo cha kijana huyo ni cha kutatanisha kutokana na madai kwamba, baadhi ya watu walimuona akitembea nje. “Wakati tukijiandaa kuswalia maiti hiyo, ndipo zikaanza tetesi kwamba marehemu ameonekana nje akitembea. Kauli hiyo ilianza kuenea miongoni mwa watu waliokuwa msibani, na hatimaye kujaa kila upande wa msikiti,” alisema ndugu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Baada ya kuibuka mzozo baina ya pande mbili zinazounga mkono azikwe na wengine wakipinga, polisi walifika msikitini hapo kutuliza vurugu.

Wakati baba wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Hamisi kutangaza kuwa mwili ukazikwe, kundi lingine lililokuwa likitaka asizikwe, lilikwenda moja kwa moja hadi makaburi ya Msikiti wa Jumuiya Manzese kwa Mfuga Mbwa na kufukia kaburi.

Polisi ilibidi wapige risasi hewani kwa ajili ya kutuliza vurugu katika eneo ulipo msikiti huo. Hata hivyo, waombolezaji hao walianza kuwarushia polisi chupa, mawe na vipande vya miti. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kuwepo tukio hilo. “Sasa hivi natoka safarini ila nitaelekea kwenye tukio,” alisema na kuongeza kwamba amewatuma polisi kwenda kuchunguza chanzo.

Alisema, ingawa amesikia, lakini chanzo hakijajulikana kama ni imani za kishirikina au ipo sababu nyingine. Polisi waliamua kuuchukua mwili na kuupakia kwenye gari na kuupeleka kwenye Hospitali ya Mwananyamala. Kijana huyo ambaye alianguka katika viwanja vya mpira vya Faru, vilivyopo karibu na Kituo cha Polisi Mpakani Manzese, alichukuliwa hadi nyumbani alikofia kabla ya kumpeleka hospitali.Chanzo Habari leo.

No comments: