Powered By Blogger

Tuesday, June 28, 2011

Mchungaji Mbaroni kwa kumuua Mkewe.

MCHUNGAJI wa Kanisa la World Missionery Fellowship of Tanzania (WMF) katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Bw. Gaspar Joseph (52) anashikilizwa na polisi kwa kumuua mke wake baada ya kumpiga kwa fimbo katika ugomvi baina yao.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Bw. Henry Salewi alimtaja mwanamke huyo aliyeuawa kuwa ni Godeliver Gaspar (48) mkazi wa Migera katika Manispaa ya Bukoba, na kuwa alifariki dunia Juni 26, mwaka huu katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.

Bw. Salewi alisema kuwa mchungaji huyo alikuwa akimpiga mke wake kwa muda mrefu, ambapo Juni 22 baada ya kumpa kipigo kikali, mchungaji huyo alimpeleka hospitali bila kutoa taarifa zozote, ambapo Juni 26 alifariki dunia wakati akipatiwa dawa.Alisema jeshi la polisi linamshikilia mchungaji huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi na kuwa atafikishwa mahakamani baada ya taratibu muhimu kukamilika.

Kamanda Salewi alisema kabla ya kifo cha mwanamke huyo, polisi walipokea taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu kuwa Bi. Gaspar hali yake ni mbaya na amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kutokana na kipigo cha mme wake.
 
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa na kuwa chanzo cha ugomvi huo uliosababisha kifo hicho bado hakijafahamika, ingawa taarifa kutoka eneo la tukio zinadai kuwa ugomvi huo ulitokana na binti yao wa kike kupata mimba.

Taarifa hizo zinasema kuwa mchunguji huyo alikuwa akimshtumu mke wake kusababisha mtoto wao wa kidato cha kwanza kupata mimba kwa madai ya kutomlea katika maadili, pia akimtuhumu kwa kuficha siri za binti huyo juu ya ujauzito aliokuwa nao.

Taarifa hizo zinadai wiki mbili kabla ya mwanamke huyo kuzidiwa na kupelekwa hospitali kila mara alikuwa akimpiga, hali inayodaiwa kusababisha maumivu na hatimaye kifo chake. Chanz gazeti la majira.

No comments: