Powered By Blogger

Tuesday, June 21, 2011

Mbunge na Hakimu wabanwa kwa kutokuwasilisha tamko la mali.

Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma jana liliwafikisha kwenye baraza hilo, Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Yusuph Nassir, na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Usevya iliyopo Wilayani Mpanda, Vultan Kundy, kwa kushindwa kurejesha fomu za mali zao.

Akijitetea mbele ya baraza hilo chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Nassir alikana mashitaka hayo na kujitetea kuwa alitimiza wajibu wake wa kuchukua fomu na kuirejesha katika ofisi za maadili za mkoani Dodoma.Alisema hata hivyo alishangaa kuona anaitwa katika baraza hilo wakati alikuwa ni miongoni mwa wale waliojaza na kurejesha fomu hizo na kukiri kwamba Desemba 22, mwaka jana ndipo aliporejesha.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, nakili kwamba mimi si kiongozi mzembe, kwa sababu nilitekeleza agizo la kujaza fomu iliyonitaka kuorodhesha mali zangu na nilifanikiwa kurejesha Desemba 22, mwaka jana hivyo kosa si langu bali ni tatizo la kimasijala,” alisema.

Aidha, aliliambia baraza hilo kuwa tatizo la malalamiko ya kushindwa kurejesha fomu, amelisikia kwa baadhi ya wabunge ambao wengi wao wanalilalamikia kwa kuwaita katika baraza japokuwa walirejesha fomu hizo.
Kwa upande wake, Vultan Kundy alisema tangu alipoajiriwa kuwa hakimu katika mahakama ya mwanzo ya Isevya wilayani Mpanda mwaka 2008, hajawahi kujaza fomu hizo kutokana na kushindwa kuzipata kwa wakati.

Hata hivyo, baraza liliwaachia watuhumiwa kuendelea na shughuli zao kwa lengo la kusubiri maamuzi yatakayotolewa baadaye dhidi yao

No comments: