Kwa mujibu wa vyanzo vya habari mtumishi wa kike wa usafi wa Hoteli ya Sofitel mwenye umri wa miaka 32 amedai kuwa majira ya saa saba mchana (saa za NY) aliingia chumbani kwa Bw. Strauss-Kahn kwa ajili ya kufanya usafi na kujikuta uso kwa uso na Mkurugenzi huyo ambaye alikuwa uchi wa mnyama. Kwa mujibu wa malalamiko yaliyotolewa na mfanyakazi huyo Bw. Strauss-Kahn alijaribu kumuangusha chini na kutaka kumuingia kimwili lakini aliweza kumzidi nguvu na kuponyoka.
Mara baada ya kuponyoka mtumishi huyo (jina lake limehifadhiwa) alitoa taarifa kwa uongozi wa hoteli hiyo ya kifahari ambao uongozi huo ulitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambapo maafisa wa Kikosi Maalum kinachochughulikia mambo hayo ya mashambulizi ya kingono (Special Victims Unit) walifika hoteli hiyo ili kufanya uchunguzI. Hata hivyo walipofika walikuta Bw. Strauss-Kahn amekwishaondoka huku akiwa ameacha baadhi ya vitu mbalimbali hotelini hapo na kufanya ihisiwe kuwa aliondoka kwa haraka haraka.
UchunguzI wa haraka wa NYPD ulionesha kuwa Bw. Kahn alikuwa uwanja wa ndege wa John F. Kennedy na taarifa zilitolewa kwa kikosi cha Polisi cha Mamlaka za Usafiri kilimfuatilia na kumkuta akiwa ndani ya ndege hiyo ambapo waliweza kumtaka ashuke na kufuatana nao kwa ajili ya kutoa maelezo ambayo yataisaidia Polisi kuona kama kuna mashtaka yoyote yanaweza kuletwa dhidi yake.
Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa Bw. Kahn hata kama itakutwa amejihusisha na kitendo kama hicho asikutwe na mkono mkali wa sheria kwani yawezekana analindwa na Kinga ya Kibalozi na hivyo kitu pekee ambacho kinaweza kufanyika ni yeye kuondoka Marekani. Hadi jioni ya Jumamosi Shirika la Fedha Duniani halikuwa na kauli yoyote rasmi dhidi ya Mkurugenzi wake huyo. Iwapo mahakama ikiona hana kinga ya kutoshtakiwa na iwapo itamkuta na hatia, huenda bosi huyo akatumikia miaka 25 jela.
Miaka minne tu iliyopita kashfa ya mahusiano ya kingono ilimkumba Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Bw. Paul Wolfowitz ambaye alidaiwa kumpandishia mshahara kinyume cha taratibu mpenzi wake Shaha Riza. Pamoja na kashfa hiyo na nyingine ambazo zilimkuta Bw. Wolfowitz alilazimika kujiuzulu nafasi yake hiyo mwezi Mei 2007. Maoni ya wadadisi wa masuala ya uwajibikaji yanaonesha kuwa uzito wa tuhuma hidi dhidi ya Bw. Strauss Kahn vitasababisha ajiuzulu nafasi yake aibu na kupoteza hata uwezekano wa kuwa Rais wa Ufaransa.
Bw. Kahn amekuwa na uhusiano wa karibu na serikali ya Tanzania katika kuisaidia kwenye sera zake mbalimbali za Uchumi. Mwaka 2009 alikuwa ni mmoja wa wageni mashuhuri katika Mkutano wa IMF uliofanyika nchini ambao Rais Kikwete alikuwa ni mwenyeji wake.Bw. Strauss-Kahn ambaye ni mjamaa amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi huko Ufaransa ikiwa ni pamoja na Uwaziri wa Viwanda na Uwaziri wa Fedha. Ameoa na ana watoto wanne. Baadhi wa wadadisi wa masuala ya kisiasa wamesema huanda tuhuma izo zinamlengo wa kumchafua bosi huyo wa IMF, ambae anampango wa kugombea kiti cha uraisi huku ufaransa.
No comments:
Post a Comment