Powered By Blogger

Tuesday, April 26, 2011

'Siasa' mahakamani zamkera Hakimu, ajitoa

HAKIMU Wilberforce Luhwago wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam aliyekuwa akisikiliza kesi ya kukaidi amri ya Mahakama inayomkabili Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, amejitoa katika kesi hiyo huku akionya siasa itaimaliza nchi.

Luhwago amesema, siasa ikiingia mahakamani nchi itayumba na watoto wa shule hawatowaelewa walimu wao kuwa Tanzania kila mtu yuko sawa mbele ya sheria, “wakati hati za kukamatwa na zile za miito mahakamani zinawalenga wauza vitumbua tu na wa misokoto ya bangi.”

Kutokana na uamuzi huo, aliwataka mawakili waliokuja kusikiliza kesi hiyo katika mahakama hiyo kupata habari zote za shauri hilo kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joyce Minde na si yeye tena.

Awali jalada halisi la kesi hiyo lilipelekwa katika Mahakama Kuu kwa mapitio, hali iliyozua mjadala wa kisheria katika mahakama hiyo.

Mmoja wa wanasheria wanaomtetea Fuime, alihoji kwanini mahakama hiyo inaendelea na kesi ambayo jalada lake lipo Mahakama Kuu.

Hakimu Luhwago, alimjibu wakili huyo kuwa kama alitambua katika mahakama hiyo hakukuwa na kesi hiyo, alifika mahakamni hapo kufanya nini na kumtaka aende ilipo kesi hiyo. Hata hivyo wakili huyo alikaa kimya.

“Kwa maneno ya wakili naamini hakuna kesi mbele ya Mahakama hii, basi sasa niamuriwe nikae au niondoke katika meza kuu na nikae kama wasikilizaji wengine waliopo katika chumba hiki cha kusikilizia kesi,” alisema Luhwago.

Awali mahakama hiyo ilitoa hati ya kumuita Faume mahakamani ambayo ilidharauliwa hivyo mahakama ikatoa amri ya kukamatwa kwa mkurugenzi huyo lakini haikutekelezwa.

Faume alitakiwa kufika mahakamani hapo kusikiliza shauri linalohusu mgogoro kati yake na kampuni ya usafi ya TECA uliotokea mwaka 2009.

Mgogoro huo ulianza baada ya Mkurugenzi huyo kutoa hati ya kusimamishwa kwa kazi ya uzoaji taka iliyokuwa ikifanywa na kampuni hiyo, kampuni hiyo ikaenda mahakamani.

No comments: