Powered By Blogger

Wednesday, August 8, 2012

Prof. Shivji Aja Juu kwa kulishwa maneno kuwa anaukana Muungano

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgStux7h_9-RiR_fH4oMmM4XIFthF9PLC-_Yokxx5VoTuJZbAtKvB1cpSW95I-5KH4okCB2vHezX6tRVAr0KwvvKhhzYBPaOQ0AyEMvD44pHmepnCoidgUKAGvroVONxQsv4_9kbxpPNBoO/s1600/sh1.jpg 

 

Hukumu ya Mahalu kutolewa leo.



Prof.Mahalu akiwa na Mawakili wake(Maktaba)

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Ilvin Mgeta leo anatarajiwa kutoa hukumu ya kesi Na.1/2007 inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Mkuu wa Fedha na Utawala katika ubalozi huo, bi. Grace Martin, wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara.

Hukumu hiyo ambayo awali ilikuwa imepangwa kusomwa tarehe 10 Juali mwaka huu, iliahirishwa na sababu  zikitajwa na Hakimu Aloyce Katemana kuwa ni Hakimu aliyekuwa asome hukumu hiyo, Ilvin Mgeta alipata dharura na hivyo hukumu hiyo ilisogezwa mbele kusubiri atakaporejea.

Kesi hiyo hiyo ambayo imedumu mahakamani hapo kwa miaka saba sasa, ilifunguliwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 22 mwaka 2007.

Serikali yaridhia mabadiliko Sheria ya Mafao

Picha ya mzee kutoka Maktaba


SIKU moja baada ya Bunge kupitisha azimio la kutaka kuwasilishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambao kipengele cha muda wa ukomo wa kuchukua mafao kimekuwa kikipingwa na wadau, Serikali imekubali ombi hilo.

Juzi, jioni Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), aliwasilisha maelezo binafsi akitaka muswada huo urejeshwe bungeni ili ufanyiwe marekebisho.

Jafo alitaka kupitishwa kwa azimio ili sheria hiyo irejeshwe bungeni na kufanyiwa mabadiliko ya kifungu cha muda wa ukomo wa kuchukua mafao ya mteja kutoka cha sasa, ambacho ni kati ya miaka 55 hadi 60 na kisha kimruhusu mwanachama kuchukua fao la kujitoa kabla ya umri rasmi wa kustaafu.

Akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema sheria hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na umma na kutangazwa kwa hisia tofauti na vyombo mbalimbali vya habari.

Waziri Kabaka alisema baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa Serikali, iliweka kifungu cha kufuta fao la kujitoa kutokana na mifuko mingi ya jamii kuwa katika hali mbaya kifedha.

“Wengine walisema NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii) iko hatarini kufilisika baada ya Serikali kushindwa kulilipa shirika hilo kutokana na uwekezaji mbaya uliofanywa,” alisema Kabaka.
Kabaka alisema wapo waliodai kuwa hatua hiyo ya Serikali ina lenga kutunisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili baadaye ichukue fedha hizo kwa ajili ya chaguzi mbalimbali.

Alisema sababu zote hizo hazikuwa sahihi na kwamba Serikali inachokiona ni kuwa haikutoa elimu ya kutosha kabla ya kuwasilisha muswada huo wa sheria Aprili, mwaka huu.

“Serikali imesikia malalamiko ya wafanyakazi na hoja za wabunge na kuzingatia yote yaliyopo katika azimio la Bunge na imekubali kuleta muswada kwa hati ya dharura,” alisema Kabaka.
Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, imeishauri Serikali kuirekebisha sheria hiyo haraka kwa vile imeleta mtafaruku mkubwa kwa wafanyakazi.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama alisema imebaini kuwa sheria mpya ilianza kutumia hata kabla ya kutungwa kwa kanuni zake.

Kutokana na upungufu huo, kamati hiyo imependekeza kurejeshwa kwa fao la kujitoa na mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kulipia mkopo wa nyumba.

Kamati hiyo imependekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo ili mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kwa ajili ya kugharimia shughuli nyingine yoyote kwa lengo la kuandaa mazingira mazuri ya maisha baada ya kustaafu.

Kuwasilishwa kwa maelezo binafsi ya Jafo yaliyosababisha Bunge kupitisha azimio lake juzi jioni na maelezo ya Waziri Kabaka kulizima mjadala mkali uliotarajiwa kuibuka bungeni hiyo jana.

Wabunge wengi walikuwa wamepanga kukwamisha bajeti ya wizara hiyo endapo Serikali ingeshikilia msimamo wake wa kukataa kuleta muswada huo bungeni katika Bunge lijalo.

Sheria hiyo iliibua chuki na hasira za wafanyakazi nchi nzima, huku baadhi ya vyama vya wafanyakazi vikijiandaa kuendesha maandamano na migomo nchi nzima kupinga sheria hiyo. Chanzo gazeti la Mwananchi.

Monday, August 6, 2012

NAIBU JAJI MKUU KENYA ATIWA HATIANI.



Bi. Nancy Baraza
Jopo maalum la majaji lililoteuliwa na rais Mwai Kibaki kuchunguza tuhuma zilizokuwa zinamkabili Naibu Jaji Mkuu wa Kenya Nancy Baraza kumdhalilisha mlinzi mmoja katika duka moja kubwa mjini Nairobi, imependekeza, jaji huyo kuondolewa madarakani.

Akisoma hukumu hiyo mjini Nairobi leo, mwenyekiti wa jopo hilo, Jaji mkuu mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhan, amesema Nancy Baraza akiwa mtumishi wa chombo cha kusimamia sheria na haki hakutakiwa kwa namna yoyote kutenda kosa hilo dhidi ya mlalamikaji Bi Rebecca Kerubo.

Amesema kitendo alichofanya Nancy Baraza na ni cha utomvu mkubwa wa nidhamu na hivyo kupendekeza kwa Rais Mwai Kibaki kumwondoa katika wadhifa wake wa naibu jaji mkuu.

Nancy Baraza alituhumiwa kumnyanyasa na kumpiga Bi Kerubo tarehe 31 Desemba 2011, baada ya kutakiwa kufanyiwa ukaguzi kabla ya kuingia katika duka hilo, utaratibu ambao umekuwa ukitekelezwa kwa wateja wote.

Saturday, August 4, 2012

JOHN MNYIKA APELEKA MUSWADA BINAFSI WA: MAREKEBISHO YA SHERIA ZA HIFADHI YA JAMII

Mh. John Mnyika(Mb)





Jana tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.

Nimeomba muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa.

Pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo nimechukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi juu ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii anapoacha kazi na kuhitaji kupewa mafao yake kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.

Nimeomba kupatiwa ushauri na usaidizi wa kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 21 (1) (d), (e) na (2) ili kuweza kuandaa Muswada Binafsi wa Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1), Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2), hati ya kuwasilisha muswada kwa dharura na hoja ya kutengua masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).

Kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria yanaweza kuwekwa kando na kutenguliwa kwa hoja kutolewa na kuamuliwa kama kutawasilishwa Bungeni hati iliyowekwa saini na theluthi mbili ya Wajumbe wote wa Kamati kama ni Muswada wa Kamati na kwa Muswada wa Mbunge hati iliyowekwa saini na Wabunge wasiopungua kumi inayoeleza kuwa muswada binafsi uliotajwa katika hati hiyo ni wa dharura.

Naomba kutoa taarifa kwamba kuanzia jumatatu tarehe 6 Agosti 2012 nitaanza kukusanya saini za wabunge wanaounga mkono kuwasilishwa kwa muswada tajwa kwa hati ya dharura kufanya haraka marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii.

Nimeomba pia kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Cap 296 R.E 2002 kupatiwa nakala ya taarifa na nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kujiandaa kuwasilisha muswada husika: Social Security Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012, Sheria za Hifadhi ya Jamii zinazohusika, Taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na kupelekea kufutwa kwa mafao ya kujitoa (withdrawal benefits) na maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika kiliingizwa na hatimaye kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.

Pamoja na kuomba taarifa na nyaraka kupitia kwa Katibu wa Bunge natoa mwito kwa wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutunipatia maoni na mapendekezo kwa ya kuzingatiwa kwenye Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 katika kipindi cha wiki moja.

Ikumbukwe kwamba kifungu cha kufuta mafao ya kujitoa kilichozua mgogoro hakikuwepo wakati muswada uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni tarehe 1 Februari 2012 bali kiliwasilishwa kupitia jedwali la marekebisho ya Wizara lililowasilishwa tarehe 13 Aprili 2012 bila malengo na madhumuni yake kuelezwa kwa ukamilifu.

Kupitishwa kwa kifungu hicho kumethibitisha maneno niliyoyatoa bungeni kuwa tumefika hapa tulipo kutokana na ‘uzembe wa bunge na wabunge’ na kwa hili pamoja na mchango nilioutoa bungeni kwa maandishi siku hiyo juu ya haja ya kuwa mfumo mpana zaidi wa pensheni na hifadhi ya jamii (universal pension and social security) pamoja na kuwa sikuunga mkono kifungu husika kilichoingizwa kinyemela naomba radhi kwa wananchi wa Ubungo na wafanyakazi kwa kutokuwasilisha jedwali la marekebisho kupinga kifungu hicho kuingizwa.

Izingatiwe kuwa ili kurekebisha hali hiyo tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.

Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika migodi mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe 1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini. Kufutwa kwa fao la kujitoa kumelalamikiwa pia na wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii katika Jimbo la Ubungo na katika taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, suala hili na tukio husika litumike kama rejea ya bunge na wabunge kuikatalia Serikali kuwasilisha marekebisho yenye athari kubwa kipindi cha mwisho na hivyo wabunge kukosa fursa ya kupata maoni ya wananchi na pia Serikali itakiwe kuomba radhi kufuatia kulipotosha bunge kuwa wadau wa hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi na vyama vyao walishirikishwa na kuridhia wakati ambapo wamejitokeza na kukanusha madai hayo yaliyotolewa na Wizara bungeni.

Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.

Hivyo, naungana na wote wenye kutaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.
Aidha, pamoja na Mamlaka kueleza kwamba sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za Kiserikali au Mifuko kufilisika ni vizuri mamlaka ikaeleza kwa uwazi na ukweli sababu zingine za kufanyika kwa marekebisho hayo zaidi ya ile ya kutimiza malengo ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha ya uzeeni. Tahadhari za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za Hesabu za mwaka 2010/2011 na miaka mingine zinaashiria masuala ya ziada ambayo yanaweza kuwa yameisukuma Serikali kuja na mbinu zingine za kuhakikisha uendelevu wa mifuko ikiwemo kupitia marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii.

Ili bunge liweze kutimiza wajibu wa kuishauri na kuisimamia serikali kufanya marekebisho yanayostahili ya sheria husika kwa haraka ni muhimu ratiba ya bunge ikabadilishwa.

Tafsiri ya marekebisho ya ratiba yaliyofanyika ni kuwa hoja binafsi niliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge kutaka bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka haitapata nafasi ya kujadiliwa bungeni. Aidha ratiba hiyo mpya hoja binafsi iliyoelezwa kuwa itawasilishwa na Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo kuhusu kufutwa kwa mafao ya kujitoa kufuatia marekebisho ya sheria za Hifadhi za Jamii nayo haitawasilishwa kwenye mkutano huu wa Bunge unaoendelea kama ratiba haitafanyiwa marekebisho.

Hata hivyo, izingatiwe kuwa chanzo cha kufutwa kwa mafao ya kujitoa ni marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii hivyo ufumbuzi wa kurejesha fao la kujitoa unapaswa kuwa ni marekebisho ya sheria hatua ambayo njia ya haraka ya kuifikia ni kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ama na serikali au kamati au mbunge badala ya hoja binafsi.

Hoja binafsi inaweza kuwezesha bunge kujadili na kupitisha maazimio ya kuitaka Serikali kuwasilisha marekebisho ya sheria au kuishauri na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika utekelezaji wa sheria lakini sheria itaendelea kuwa palepale mpaka marekebisho yatakapofanywa kwa kuwasilishwa muswada wa sheria hatua ambayo nimeamua kuanzisha mchakato wa kuwezesha ichukuliwe.

Wenu katika kuwawakilisha wananchi,

John Mnyika (Mb)

Wednesday, August 1, 2012

MTOTO WA GHADAFI ATAKA SHITAKIWE ICC.



Saif al- Islam

Mtoto wa marehemu Ghadafi Saif al-Islam alisema iwapo kesi yake itaendeshwa Libya basi inakuwa sawa na kuuawa, kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakama ya ICC(International Criminal Court).Kijana huyo mwenye umri wa miaka 40 anashikiliwa na wapiganaji mjini Zintan. Amekuwa akishikiliwa Libya tangu Novemba 2011Alishtakiwa na  ICC kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Serikali ya mpito ya Libya mpaka sasa imekataa kumkabidhi Saif Uholanzi ambako mahakama ya ICC iko ikisema kuwa hana budi kukabiliana na mashataka yake nchini Libya.Kanali Gaddafi, ambaye utawala wake wa kidikteta ulidumu kwa miaka 42 aliuawa katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukamatwa na waasi mwezi Octoba, katika kitendo ambacho kilishutumiwa vikali na makundi ya haki za binadamu.

'Ulinzi wa bandia'

"Siogopi kufa lakini ikiwa itaendeshwa hapa hiyo muuite tu kuwa ni uuaji na mmalizane," Saif al-Islam alinukuliwa na mawakili akisema.Mwezi Juni, wafanyakazi waliotumwa na ICC walikamatwa baada ya kukutana na Saif al-Islam, na kushikiliwa kwa zaidi ya wiki tatu.Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinasema wakati wa mkutano huo afisa aliyejifanya mlinzi alimzuia mwanasheria wa ICC kuchukua kiapo kutoka kwa Saif al-Islam.

"Mlinzi huyo ambaye kimsingi ni Bw Ahmed Amer – mwanasheria anayezungumza lugha kadhaa alijumuishwa kwenye timu hiyo makusudi kuwalaghai " nyaraka ziliandika, kwa mujibu wa Reuters."Alirejea chumbani na (mkalimani wa ICC akiwepo) alianza kupiga kelele kuwa maelezo hayo yalikuwa hatari sana, yamekiuka usalama wa Libya na kwa Ulinzi wasingeyarudisha"Mkutano ulistishwa baada ya dakika 45 na nyaraka zao kuharibiwa, wakili alisema. Baadaye walikamatwa.

Hatua hiyo ilionekana kuwa "kimyume cha sharia, uhaini na ukiukwaji wa taratibu za usalama wa Taifa kwa ama Bw Gaddafi au washauri wake na kuonyesha kuwa Gaddafi hataki kesi yake iendeshwe na mahakama za Libya." Walisema mawakili kwenye nyaraka.

Maafisa wa Libya walimshutumu wakili Melinda Taylor, aliyekuwa akiongoza ujumbe wa ICC, kwa kuwa na vifaa vya upelelezi vikiwa vimeshikizwa kwenye barua ya Saif al-Islam wakati wa mkutano.

TAARIFA YA ZITTO JUU YA TUHUMA ZA RUSHWA

Mh.Zitto Kabwe akiongea na Waandishi hapo jana

Ndugu Waandishi,

Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote  zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.

Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.

Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:

1.Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
 2.Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari  zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo nundu’’  zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
3.Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.

Ndugu Waandishi,

Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na Madini:-

    1. Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya  Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali  (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;

    2. Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio la kipekee;

    3.Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu  kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!

    4.Baada ya  tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!

    5.Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.

Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya rushwa.

    1.Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;

    2.Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na  Madaraka  ya  Bunge kwa kina;

    3.Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;

    4.Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;

 5.Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.

Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-

    Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;

    Nafarijika na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;

    Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.

    Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.

    Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge.

    Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.

    Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni

Mwisho

Kumejengeka tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.

Naamini katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.

Daima nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
Ahsanteni sana.