Picha ya mzee kutoka Maktaba |
SIKU moja baada ya Bunge
kupitisha azimio la kutaka kuwasilishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambao kipengele cha muda wa ukomo wa kuchukua mafao
kimekuwa kikipingwa na wadau, Serikali imekubali ombi hilo.
Juzi, jioni Mbunge wa Kisarawe,
Seleman Jafo (CCM), aliwasilisha maelezo binafsi akitaka muswada huo urejeshwe
bungeni ili ufanyiwe marekebisho.
Jafo alitaka kupitishwa kwa
azimio ili sheria hiyo irejeshwe bungeni na kufanyiwa mabadiliko ya kifungu cha
muda wa ukomo wa kuchukua mafao ya mteja kutoka cha sasa, ambacho ni kati ya
miaka 55 hadi 60 na kisha kimruhusu mwanachama kuchukua fao la kujitoa kabla ya
umri rasmi wa kustaafu.
Akiwasilisha bungeni Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni jana, Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema sheria hiyo imepokewa kwa hisia tofauti
na umma na kutangazwa kwa hisia tofauti na vyombo mbalimbali vya habari.
Waziri Kabaka alisema baadhi ya
vyombo vya habari vilidai kuwa Serikali, iliweka kifungu cha kufuta fao la
kujitoa kutokana na mifuko mingi ya jamii kuwa katika hali mbaya kifedha.
“Wengine walisema NSSF (Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii) iko hatarini kufilisika baada ya Serikali kushindwa
kulilipa shirika hilo kutokana na uwekezaji mbaya uliofanywa,” alisema Kabaka.
Kabaka alisema wapo waliodai kuwa
hatua hiyo ya Serikali ina lenga kutunisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili
baadaye ichukue fedha hizo kwa ajili ya chaguzi mbalimbali.
Alisema sababu zote hizo hazikuwa
sahihi na kwamba Serikali inachokiona ni kuwa haikutoa elimu ya kutosha kabla
ya kuwasilisha muswada huo wa sheria Aprili, mwaka huu.
“Serikali imesikia malalamiko ya
wafanyakazi na hoja za wabunge na kuzingatia yote yaliyopo katika azimio la
Bunge na imekubali kuleta muswada kwa hati ya dharura,” alisema Kabaka.
Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya
Jamii, imeishauri Serikali kuirekebisha sheria hiyo haraka kwa vile imeleta
mtafaruku mkubwa kwa wafanyakazi.
Akiwasilisha maoni ya kamati
hiyo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama alisema imebaini kuwa sheria mpya
ilianza kutumia hata kabla ya kutungwa kwa kanuni zake.
Kutokana na upungufu huo, kamati
hiyo imependekeza kurejeshwa kwa fao la kujitoa na mwanachama aruhusiwe kutumia
sehemu ya mafao yake ya uzeeni kulipia mkopo wa nyumba.
Kamati hiyo imependekeza
kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo ili mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu
ya mafao yake ya uzeeni kwa ajili ya kugharimia shughuli nyingine yoyote kwa
lengo la kuandaa mazingira mazuri ya maisha baada ya kustaafu.
Kuwasilishwa kwa maelezo binafsi
ya Jafo yaliyosababisha Bunge kupitisha azimio lake juzi jioni na maelezo ya
Waziri Kabaka kulizima mjadala mkali uliotarajiwa kuibuka bungeni hiyo jana.
Wabunge wengi walikuwa wamepanga
kukwamisha bajeti ya wizara hiyo endapo Serikali ingeshikilia msimamo wake wa
kukataa kuleta muswada huo bungeni katika Bunge lijalo.
Sheria hiyo iliibua chuki na
hasira za wafanyakazi nchi nzima, huku baadhi ya vyama vya wafanyakazi
vikijiandaa kuendesha maandamano na migomo nchi nzima kupinga sheria hiyo. Chanzo gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment