Mh. John Mnyika(Mb) |
Jana tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge
ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na
hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.
Nimeomba
muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili
kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu
niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012
kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya
kujitoa kuendelea kutolewa.
Pamoja na
hatua hiyo ya kuomba muongozo nimechukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu
wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi juu ya Marekebisho ya
Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka
2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za
Bunge (Toleo la Mwaka 2007).Lengo la
Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la
kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa
mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii anapoacha kazi na kuhitaji kupewa mafao
yake kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima
(miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
Nimeomba
kupatiwa ushauri na usaidizi wa kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 21 (1) (d),
(e) na (2) ili kuweza kuandaa Muswada Binafsi wa Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya
81 (1), Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2), hati ya
kuwasilisha muswada kwa dharura na hoja ya kutengua masharti kuhusu muda wa
utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 81 (5) masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria
yanaweza kuwekwa kando na kutenguliwa kwa hoja kutolewa na kuamuliwa kama
kutawasilishwa Bungeni hati iliyowekwa saini na theluthi mbili ya Wajumbe wote
wa Kamati kama ni Muswada wa Kamati na kwa Muswada wa Mbunge hati iliyowekwa
saini na Wabunge wasiopungua kumi inayoeleza kuwa muswada binafsi uliotajwa
katika hati hiyo ni wa dharura.
Naomba
kutoa taarifa kwamba kuanzia jumatatu tarehe 6 Agosti 2012 nitaanza kukusanya
saini za wabunge wanaounga mkono kuwasilishwa kwa muswada tajwa kwa hati ya
dharura kufanya haraka marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la
kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa
mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii.
Nimeomba
pia kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga
na Madaraka ya Bunge Cap 296 R.E 2002 kupatiwa nakala ya taarifa na nyaraka
zifuatazo kwa ajili ya kujiandaa kuwasilisha muswada husika: Social Security
Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012, Sheria za Hifadhi ya Jamii zinazohusika,
Taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na kupelekea kufutwa kwa mafao ya
kujitoa (withdrawal benefits) na maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika
kiliingizwa na hatimaye kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.
Pamoja na
kuomba taarifa na nyaraka kupitia kwa Katibu wa Bunge natoa mwito kwa wadau wa
mifuko ya hifadhi ya jamii kutunipatia maoni na mapendekezo kwa ya kuzingatiwa
kwenye Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi
ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 katika
kipindi cha wiki moja.
Ikumbukwe
kwamba kifungu cha kufuta mafao ya kujitoa kilichozua mgogoro hakikuwepo wakati
muswada uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni tarehe 1 Februari 2012 bali
kiliwasilishwa kupitia jedwali la marekebisho ya Wizara lililowasilishwa tarehe
13 Aprili 2012 bila malengo na madhumuni yake kuelezwa kwa ukamilifu.
Kupitishwa
kwa kifungu hicho kumethibitisha maneno niliyoyatoa bungeni kuwa tumefika hapa
tulipo kutokana na ‘uzembe wa bunge na wabunge’ na kwa hili pamoja na mchango
nilioutoa bungeni kwa maandishi siku hiyo juu ya haja ya kuwa mfumo mpana zaidi
wa pensheni na hifadhi ya jamii (universal pension and social security) pamoja
na kuwa sikuunga mkono kifungu husika kilichoingizwa kinyemela naomba radhi kwa
wananchi wa Ubungo na wafanyakazi kwa kutokuwasilisha jedwali la marekebisho
kupinga kifungu hicho kuingizwa.
Izingatiwe
kuwa ili kurekebisha hali hiyo tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka
Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13
Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao
walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal
benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO)
kililikanusha.
Hata
hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe
28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo
imesababisha migongano kuendelea katika migodi mbalimbali kuhusu madai hayo
hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe 1 na 2 Agosti 2012 inaweza
kusababisha migomo migodini. Kufutwa kwa fao la kujitoa kumelalamikiwa pia na
wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii katika Jimbo la Ubungo na katika taifa
kwa ujumla.
Hata
hivyo, suala hili na tukio husika litumike kama rejea ya bunge na wabunge
kuikatalia Serikali kuwasilisha marekebisho yenye athari kubwa kipindi cha
mwisho na hivyo wabunge kukosa fursa ya kupata maoni ya wananchi na pia Serikali
itakiwe kuomba radhi kufuatia kulipotosha bunge kuwa wadau wa hifadhi ya jamii
hususan wafanyakazi na vyama vyao walishirikishwa na kuridhia wakati ambapo
wamejitokeza na kukanusha madai hayo yaliyotolewa na Wizara bungeni.
Kwa
upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye
marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu
katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini hali ambayo
inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.
Hivyo,
naungana na wote wenye kutaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa
“kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya
kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo
itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu
kwa Wadau”.
Aidha,
pamoja na Mamlaka kueleza kwamba sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za
Kiserikali au Mifuko kufilisika ni vizuri mamlaka ikaeleza kwa uwazi na ukweli
sababu zingine za kufanyika kwa marekebisho hayo zaidi ya ile ya kutimiza
malengo ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu
anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha ya uzeeni. Tahadhari
za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za Hesabu za mwaka
2010/2011 na miaka mingine zinaashiria masuala ya ziada ambayo yanaweza kuwa
yameisukuma Serikali kuja na mbinu zingine za kuhakikisha uendelevu wa mifuko
ikiwemo kupitia marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii.
Ili bunge
liweze kutimiza wajibu wa kuishauri na kuisimamia serikali kufanya marekebisho
yanayostahili ya sheria husika kwa haraka ni muhimu ratiba ya bunge
ikabadilishwa.
Tafsiri
ya marekebisho ya ratiba yaliyofanyika ni kuwa hoja binafsi niliyoiwasilisha
kwa katibu wa Bunge kutaka bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za
haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka
haitapata nafasi ya kujadiliwa bungeni. Aidha ratiba hiyo mpya hoja binafsi
iliyoelezwa kuwa itawasilishwa na Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo kuhusu
kufutwa kwa mafao ya kujitoa kufuatia marekebisho ya sheria za Hifadhi za Jamii
nayo haitawasilishwa kwenye mkutano huu wa Bunge unaoendelea kama ratiba haitafanyiwa
marekebisho.
Hata
hivyo, izingatiwe kuwa chanzo cha kufutwa kwa mafao ya kujitoa ni marekebisho
ya sheria za hifadhi ya jamii hivyo ufumbuzi wa kurejesha fao la kujitoa
unapaswa kuwa ni marekebisho ya sheria hatua ambayo njia ya haraka ya kuifikia
ni kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ama na serikali au kamati au mbunge
badala ya hoja binafsi.
Hoja
binafsi inaweza kuwezesha bunge kujadili na kupitisha maazimio ya kuitaka
Serikali kuwasilisha marekebisho ya sheria au kuishauri na kuisimamia serikali
na mamlaka zake katika utekelezaji wa sheria lakini sheria itaendelea kuwa
palepale mpaka marekebisho yatakapofanywa kwa kuwasilishwa muswada wa sheria
hatua ambayo nimeamua kuanzisha mchakato wa kuwezesha ichukuliwe.
Wenu
katika kuwawakilisha wananchi,
John
Mnyika (Mb)
No comments:
Post a Comment