Mh.Zitto Kabwe akiongea na Waandishi hapo jana |
Ndugu
Waandishi,
Nalazimika
kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa
zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya
rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya
Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa
kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu
nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi
na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote
nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika
zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu
zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na
kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye
dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati
huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea
Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
1.Kumekuwa na kauli za watendaji wa
serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya
kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
2.Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena
katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa
na popo nundu’’ zikiashiria kwamba na
mimi ni mla rushwa; na
3.Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla
wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto
Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya
Upinzani.
Ndugu
Waandishi,
Naomba
kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika masuala ya
rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na Madini:-
1. Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania
(TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza
kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando
ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika
kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na
pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote
zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
2. Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe.
Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa
Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini
kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na
tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka
kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya
Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la
TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na
pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili
la TANESCO sio tukio la kipekee;
3.Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa
Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu
kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa
sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi
wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati
ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
4.Baada ya
tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja
alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu
wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa
rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
5.Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri
Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC
kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu
ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana
kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira
ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa
naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo
yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya
rushwa.
1.Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya
aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio
imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi
kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu
imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho
tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili
nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
2.Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa
nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge kwa kina;
3.Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama
changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na
tuhuma hizo;
4.Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya
Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
5.Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo
nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo
nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda
niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja
kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi
kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili
ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma
katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii
ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;
Nafarijika na salam mbali mbali
zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika mapambano
haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook na niko
pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini
katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu
lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania
kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa,
Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango
wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na
haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na
kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi
karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na
uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa
tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati ya
POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia
mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii
imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC
isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama
mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika
tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru
Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo
itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi
kuliko mimi.
Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa
Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka
kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa
Bunge.
Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba
baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa
kupokea rushwa.
Ni lazima tufike mahali kama viongozi
kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani
tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia
ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya
msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya
kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji
wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka
tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo.
Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna
zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia
vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine
nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini
katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga
wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao
ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea
rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima
nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa
na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao
kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa
kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo
utakapojitenga”.
Ahsanteni
sana.
No comments:
Post a Comment