Mojawapo ya Picha za Lulu, akipelekwa Kotini |
UMRI
wa msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayekabiliwa na
mashtaka ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba jana ulizua utata katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya mawakili wanaomtetea kutaka kesi hiyo
iondolewe mahakamani hapo ili akashtakiwe kwenye Mahakama ya Watoto.
Kesi
hiyo ilitajwa jana huku mawakili wanaomtetea wakiongozwa na Keneth Fungamtama,
wakiwasilisha maombi kuhusu suala hilo la umri wa mteja wao wakitaka
asishtakiwe mahakamani hapo kama ilivyo sasa. Fungamtama ambaye alikuwa
akisaidiana na Mawakili Peter Kibatala na Fulgence Masawe, alidai mahakamani
hapo kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17 hivyo, kesi yake ilipaswa
kusikilizwa katika Mahakama ya Watoto. “Mshtakiwa ana umri wa miaka 17 na tuna
uthibitisho wa cheti cha kuzaliwa ambacho kinaonyesha mahali na tarehe
aliyozaliwa mshtakiwa,” alidai Fungamtama.
Fungamtama
alisema Kifungu cha 4 cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 Kipengele namba 21,
kinatamka wazi kuwa mtoto ni yule aliye na umri chini ya miaka 18. Wakili huyo
aliendelea kunukuu vifungu mbalimbali vya Sheria ya Mtoto kama 98 (i) na 114
(ii), ambavyo alidai kuwa vyote vinawapa nguvu ya kuwasilisha maombi yao hayo
ya kuihamisha kesi hiyo. “Hata katika suala la Mahakama, vifungu vyote vya
sheria hii vimefafanua, hivyo tunawasilisha maombi yetu kwamba mteja wetu ana
umri wa miaka 17 na shauri hili lingepaswa kusikilizwa Mahakama ya Watoto,”
alidai.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Elizabeth
Kaganda aliomba wapewe muda zaidi kwa sababu bado wanaendelea na upelelezi wa
kesi hiyo. “Kesi hii imekuja mahakamani hapa kama ya mauaji na upelelezi bado
haujakamilika. Tunaposema haujakamilika, tunapeleleza kila kitu, likiwamo suala
la umri,” alieleza Kaganda. Alisema hata jina linaloonekana katika cheti cha
kuzaliwa kilichowasilishwa mahakamani hapo, linasomeka Diana Elizabeth wakati
mshtakiwa ametajwa mahakamani hapo, kwa jina la Elizabeth Michael. “Tunaomba
muda tuweze kuchunguza kuhusu umri wa mshtakiwa kwa sababu aliwaeleza polisi
kwamba ana umri wa miaka 18 halafu mawakili wake wanakuja kueleza hapa mahakamani
kwamba ana umri wa miaka 17,” alidai Kaganda. Wakili huyo wa Serikali alidai
kuwa kutokana na mvuto wa kesi hiyo katika jamii, wanaomba wapewe muda zaidi
kufanya upelelezi ili kumtendea haki mshtakiwa huyo.
Kuhusu cheti hicho kusomeka Diana Elizabeth,
Wakili Fungamtama alikiri na kudai kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa Wakristo
kuwa na majina mawili. Fungamtama alidai kuwa hawana pingamizi na maombi ya
upande wa mashtaka kwamba wapewe muda zaidi wa kufuatilia cheti cha kuzaliwa
cha mshtakiwa, ingawa alidai kuwa suala hilo halina ugumu. Akitoa uamuzi baada
ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi Augustina Mbando alisema:
“Mahakama imesikiliza maombi yaliyoletwa na Fungamtama na Kaganda na imeona
kesi iliyopo hapa ni ya mauaji na jinsi kesi hii ilivyo, hatuwezi kufanya hoja
yoyote hadi upelelezi utakapokamilika.”
“Kama
defence (upande wa utetezi) wana maombi yoyote wanaweza kufanya hivyo kupitia
Mahakama Kuu,”.Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Mei 21, mwaka huu itakapotajwa tena. Inadaiwa kuwa Aprili
7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam msanii huyo wa kike,
alimuua Kanumba. Jana Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 2:50 asubuhi akiwa
peke yake kwenye gari linalobeba mahabusu, huku akisindikizwa na magari mengine
mawili.
Alipoingia
mahakamani alikuwa amezingirwa na askari Magereza na Polisi zaidi ya 10 na
kuufanya umati mkubwa wa watu uliofurika
mahakamani hapo kushindwa kumwona. Miongoni mwa watu waliofika mahakamani hapo
jana ni baba mzazi wa msanii huyo, Michael Kimemeta na ndugu zake wengine
kadhaa. chanzo Gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment