Katika pita pita zangu katika
mitandao ya kijamii, hususani katika mtandao marufu wa” Jamii Forums”
nimekutana na majibu ya mdau juu ya hoja inayotikiza muhimili wa Makama nchini
iliyoibushwa na Mh. Tundu Lissu katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Katiba na
Sheria Mwezi uliopita.
Kimsingi Mh. Tundu lissu
aliwasilisha utetezi wake kwenye kamati ya maadili ya bunge baada ya kutakiwa kufanya hivyo na uongozi wa bunge. Yumkini,
wiki iliyopita Mh. Tundu Lissu katika kikao cha Mawakili( TLS) kilichofanyika
katika ukumbi wa AICC, name nikipata fursa ya kuudhulia aliendelea kuanika wazi
mambo mbalimbali yanayo husiana na Muhimili wa Mahakama hususani Majaji.
Hivyo basi nineona nibora nikuletee alichaoandika
Mdau huyo wa Jamii Forums kama ifuatavyo:
Nimeshangazwa sana na hatua ya
Mh. LISSU ya kuvunja Kanuni za Bunge na kutawanya katika magazeti kile
alichokiita utetezi wake bila kujali haki asilia ya wale anaowatuhumu.
Nitashangaa kama Bunge litashindwa kulinda hadhi na heshima yake kwa kutomchukulia
Mbunge huyu hatua kali za kinidhamu.
Nimeshangazwa sana pia na hatua ya MH. LISSU
kuendelea kulalamika katika Mkutano wa Mawakili na kutaka MAJAJI ALIOWATUHUMU
WAONDOLEWE bila ya yeye kuchukua hatua za KIKATIBA.
Mh. LISSU na “WANASHERIA-HARAKATI” wenzako,
nchi yetu iaongozwa na sheria na sio na kulalama.
Ni Katiba hii hii ya Jamhuri ya Muungano
ambayo imempa Mh. Lissu Ubunge, vinginevyo ni watu wachache sana walikuwa
wanamfahamu Tundu Lissu kabla ya kuukwa UBUNGE. Na ni kwa kutumia KINGA YA Katiba
hii hii ambayo ndiyo Mh. Lissu anaitumia kuwatuhumu na kuwahukumu MAJAJI na
Mhimili wote wa MAHAKAMA.
KINGA YA KIKATIBA YA UHURU WA KUONGEA ANAYOTUMIA MH. LISSU
Ni katiba hiyo hiyo iliyompa uhuru wa kuongea
Mh. Lissu, ndio hiyo hiyo iliyowapa majaji kinga na kuondolewa kwa utaratibu
maalumu. Kinga anayotumia Mh. Lissu kuwatukuhumu na kuwahukumu Majaji ni IBARA
ya 100 inayosema:
100. Uhuru wa majadiliano na utaratibu wa shughuli bungeni
(1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo,
majadiliano na utaratibu katika Bunge, na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa
na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali
penginepo nje ya Bunge.
(2) Bila ya kuathiri Katiba hii
au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa
au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema
au kulifanyw ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada,
hoja au vinginevyo.
Pamoja na Wabunge kuwa na Kinga, Katiba
hiyo hiyo iliyowapa waheshimiwa Wabunge KINGA pia inampa Mh. Rais KINGA, na pia
inawapa Majaji KINGA na utaratibu wa kuwaondoa majaji kwenye nafasi zao za
ujaji. Ibara zinazotoa kinga kwa Mahakama ni hizi. Ibara ya 107B IMETAMKA KUWA
KATIKA KUTEKELEZA MAMLAKA YA UTOAJI HAKI, MAHAKAMA ZOTE ZITAKUWA HURU NA
ZITALAZIMIKA KUZINGATIA TU MASHARTI YA KATIBA NA YALE YA SHERIA ZA NCHI.
UTARATIBU WA KATIBA KUWAONDOA MAJAJI WENYE TUHUMA
Kama ilivyo kuwa kuna utaratibu wa KIKATIBA NA
KISHERIA kwa Mbunge kupoteza Ubunge, pia zipo taratibu za KIKATIBA Rais
kuondolewa kutoka ofisi ya Rais na MAJAJI kuondolewa kutoka katika nafasi zao
za UJAJI. Tanzania ni nchi ya utawala wa Katiba, Sheria na taratibu!
Ni matumaini yangu kuwa Mh. LISSU aliapa
kuilinda na kuitetea Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa
kuwa Katiba ya Tanzania imetoa utaratibu wa kupokea tuhuma dhidi ya Majaji na
Mahakimu na namna ya kushughulikia tuhuma hizo. Nitaeleza baadaye kwa nini mimi
nadhani Mh. Lissu anatumia isivyo KINGA yake ya Ubunge kwa kulalamika KISIASA
bila kuchukua hatua za KIKATIBA NA KISHERIA.
Mh. Lissu anaweza kutoa hoja kuwa haipendi
KATIBA ya sasa. Lakini hii ndio KATIBA iliyompa ngazi ya kupanda na kuwa Mh.
Mbunge. Hii ndio Katiba iliyo halali inayofanya watanzania wamsikilize Mh.
Lissu hata kama wengine hawakubaliani naye!! Tanzania nchi pekee ambayo utakuta
Mbunge akilaani na kulaumu mfumo wa Katiba na sheria alioutumia kuupata ubunge.
Kama Mh. Lissu haipendi KATIBA YA
JAMHURI YA MUUNGANO, basi aachie kiapo chake cha Ubunge na ajiuzulu UBUNGE ili
afanye uharakati wa kupata Katiba anayopenda. Sio uungwana na sio sheria
kutumia Katiba kupata daraja la Ubunge na mara baada ya kupata Ubunge kuihujumu
Katiba hiyo hiyo.
KUWAONDOA MAJAJI KUTOKANA NA
MARADHI, TABIA MBAYA Kwa mujibu wa Katiba, kuna utaratibu wa kikatiba wa
kumtuhumu na kuondolewa kwa JAJI.
JAJI ANAWEZA KUONDOLEWA
kama itathibitishwa na Tume
MAALUM kuwa ameshindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu
nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya inayoathiri Maadili ya Kazi ya
Jaji au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Kamwe JAJI haondolewi kwa mayowe, kelele au
vigelegele vya kisiasa. Jaji haondolewi kwa umahiri wa uongeaji wa Mh. Mbunge.
Tusiwadanganye watanzania kuwa Mbunge Lissu anao uwezo wa kumuondoa JAJI yoyote
kwa yeye kumtuhumu, kumtia hatiani na kumtaka aondoke bila kufuata utaratibu wa
Kikatiba.
Mh. Lissu, kama unavyotegemea kinga ya Wabunge
kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya katiba, kumbuka kuwa Majaji, Rais pia wanayo
kinga ambayo wewe pia ni vyema uiheshimu.
Mh. Lissu, IBARA 110 inazungumzia namna ya
kumuondoa JAJI. JAJI haondolewi kwa kuwa tu Mbunge (Mh. Lissu) katoa tuhuma na
kuchukua jukumu la kuithibitisha yeye mwenyewe na kudai JAJI aliyemtuhumu
aondolewe. Huu ni utaratibu mpya sana ambao Mh. Lissu anautangazia umma wa
Tanzania.
IBARA ya 110 inayoratibu namna ya kumuondoa
JAJI inatamka:
110-(5) Jaji wa Mahakama Kuu
aweza tu kuondolewa katika madaraka ya kazi ya Jaji kwa sababu ya kushindwa
kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa
sababu ya tabia mbaya inayoathiri Maadili ya Kazi ya Jaji au Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma; na hataweza kuondolewa kazini ila kwa mujibu wa masharti
ya ibara ndogo ya (7) ya ibara hii.
(6) Iwapo Rais anaona kuwa suala
la kumwondoa Jaji kazini lahitaji kuchunguzwa, basi katika hali hiyo mambo
yatakuwa ifuatavyo–
(a) Rais atateua Tume ambayo
itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili. Na huyo Mwenyekiti
na angalau nusu ya Wajumbe wengine wa Tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni
Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye
Jumuiya ya Madola;
(b) Tume hiyo itachunguza shauri
lote halafu itatoa taarifa kwa Rais kuhusu maelezo ya shauri hilo lote na
itamshauri Rais kama huyo Jaji anayehusika aondolewe kazini kwa mujibu wa
masharti ya ibara hii kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi
na sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya.
(7) Ikiwa Tume iliyoteuliwa kwa
mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (6) itamshauri Rais kwamba Jaji ambaye
habari zake zimechunguzwa na hiyo Tume aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa
kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya
tabia mbaya, basi Rais atamwondoa kazini Jaji huyo anayehusika.
(8) Ikiwa suala la kumwondoa Jaji
kazini limepelekwa kwenye Tume kwa ajili ya uchunguzi kwa mujibu wa masharti ya
ibara ndogo ya (6) ya ibara hii, Rais aweza kumsimamisha kazi Jaji huyo
anayehusika, na Rais aweza wakati wowote kufuta uamuzi huo wa kumsimamisha kazi
Jaji huyo, na kwa hali yoyote uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri Rais
kwamba Jaji huyo asiondolewe kazini.
(9) Masharti ya ibara hii
yatatumika bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (12) ya ibara ya 109 ya
Katiba hii.
Utaratibu wa kumuondoa Jaji kwa
mujibu wa Ibara ya 110 ya Katiba unazingatia msingi muhimu wa katiba ambao Mh.
Lissu amewanyima Majaji aliowatuhumu, yaani haki ya kusikilizwa kabla ya
kuhukumiwa kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (a) na (b) ya Katiba yaani:-
- haki ya MAJAJI waliotuhumiwa na
MH. LISSU kupewa fursa ya kusikilizwa na chombo cha kikatiba kilichoundwa kwa
mujibu wa IBARA ya 110 ya Katiba;
-haki ya MAJAJI waliotuhumiwa na
MH. LISSU kutotendewa kama TAYARI wana makosa anayodai Mh. LISSU mpaka itakapothibitika
kwa mujibu wa IBARA ya 110 kuwa wanayo makosa anayodai Mh. Lissu;
Mheshimiwa Lissu hana budi kuheshimu kiapo
chake cha kuilinda na kuiheshimu Katiba ya JAMHURI ya Muungano wa Tanzania na
afuate utaratibu wa kikatiba badala ya kutumia kinga yake ya Bunge kutuhumu,
kuhukumu na kutoa adhabu kwa majaji ambao amewataja kwa majina.
Watanzania ni vyema tukachukua tahadhari dhidi
ya watanzania wenzetu ambao wamejiweka katika daraja la juu kuliko hata Katiba
na sheria iliyowapa uongozi.
KAMATI ZA MAADILI ZA MAJAJI NA MAHAKIMU
Mwaka jana, Bunge letu lilipitisha Sheria
iitwayo JUDICIARY ADMINISTRATION ACT, 2011 (SHERIA YA BUNGE NAMBA 4 YA MWAKA
2011) na MH. LISSU alishiriki kikamilifu katika kutunga Sheria hii inayotoa
muongozo wa kupokea malalamiko na tuhuma dhidi ya majaji na mahakimu. Kwa
sababu zake mwenyewe, Mh. Lissu ametumia jukwa la kisiasa kulalamika badala ya
kufuata utaratibu wa malalamiko ili hao anaodai hawafai waondolewe kwa mujibu
wa KATIBA na Sheria.
Kumbu Kumbu za Bunge zinaonyesha
ushiriki wa Mh. Lissu kwa ukamilifu. Sheria hii kimeanzisha KAMATI ZA MAADILI
ZA MAJAJI, MAHAKIMU NA MAAFISA WENGINE WA SHERIA.
Kwa mfano SHERIA YA BUNGE NAMBA 4 YA MWAKA
2011 imeanzisha Kamati ya Maadili ya Majaji (Judges Ethics Committee) iliyopewa
jukumu la:
kupokea tuhuma dhidi ya uvunjifu wa maadili
dhidi ya Majaji wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu.
Tuhuma dhidi ya Majaji hawa ni lazima iwe ni kwa maandishi na iwasilishwe
kupitia Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kazi ya Kamati ya Maadili ya
Majaji ni kuchunguza Tuhuma na kuwasilisha Maoni yake kwa Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama
itasikiliza na kutoa mapendekezo yake kwa Mh. Rais kuhusu kuundwa Tume Maalum ya
Kikatiba ya Kumchunguza Jaji.
SHERIA YA BUNGE NAMBA 4 YA 2011
IMEANZISHA KAMATI YA MKOA YA MAADILI
Kila Mkoa unayo Kamati ya Mkoa ya Maadili
inayoshughulikia nidhamu ya Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Wilaya (Region, the
Regional Judicial Officers Ethics Committee). Kila Wilaya pia inayo Kamati za
Maadili ya Wilaya inayoshulikia nidhamu ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Mh. Lissu anafahamu fika kuwa zipo taratibu
za kushughulikia mapungufu au malalamiko dhidi ya Majaji, Mahakimu na Maafisa
wengine wa Mahakama. Ila amechagua tu kuwadhalilisha Majaji ili wawe waoga na
wasiweze kutoa maamuzi yao bila upendeleo wala uoga.
UKIMYA WA WANASHERIA, WASOMI MAHAKAMA INAPOSHAMBULIWA
Uwoga ni kitu hatari sana katika ujenzi wa
demokrasia. Ufundi wa kuongea Bungeni hauna maana kuwa kila kisemwacho na
muongeaji mahiri ni sahihi!
Ni kwa bahati mbaya WASOMI, WANASHERIA,
magazeti na vyombo vingine vya habari WANA AMINI KUWA KILA KISEMWACHO na Mbunge
LISSU ni sahihi na wamefumba macho kuhusu haki ya msingi ya kila mtanzania
kusikilizwa na kufuata utaratibu.
MAGAZETI YANAONA KUWA ni sahihi kwa Mh. Lissu
kujipa jukumu la kupeleleza “makosa ya majaji”, “kuwatuhumu na kuwatia hatiani
majaji” na “kupendekeza adhabu yeye mwenyewe”.
Watanzania tusicheze na haki asilia ya
kusikilizwa na umuhimu wa wanasiasa wa wanasheria kuheshimu sheria walizotunga
wao wenyewe. Hata MH. LISSU anastahili HAKI asilia ya kutotuhumiwa bila ya
kupewa nafasi ya kusikilizwa na kwa utaratibu uliowekwa kisheria.
JE TUHUMA DHIDI YA MAJAJI NI
MUENDELEZO WA LENGO LA JAMHURI YETU ISITAWALIKE?
Naogopa kuamini kuwa tuhuma dhidi
ya Mhimili wa Mahakama ni muendelezo wa SERA ya kuhakikisha kuwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania haitawaliki.
Mimi nadhani ni Mhimili wa
Mahakama tu ndio ulikuwa umebaki katika mtikisiko huu wa kuhakikisha kuwa
Tanzania haitawaliki.
Na njia pekee ni kuwashambulia na
kuwashushia majaji heshima mbele ya jamii. Lengo ni kuwafanya Majaji wawe waoga
na wasitoe maamuzi magumu.
Kwa Waheshimiwa MAJAJI na MAHAKIMU, huu ni
wakati wenu wa kuwa kitu kimoja. Huu ni wakati wa kutokuwa na uoga na kutimiza
wajibu wenu kwa mujibu wa katiba, sheria na masharti ya viapo vyenu. JAJI
HAONDOLEWI KWA KELELE ZA KISIASA!
Nasikia eti “WANASHERIA-HARAKATI”
wametayarisha WARAKA WA KUWAKATAA MAJAJI. WAKILI YEYOTE ambaye anachukuliwa
kuwa anaelewa utaratibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya JAJI au HAKIMU
akiwasilisha WARAKA basi huyo WAKILI atakiwe ajieleze kwa nini asitolewe katika
orodha ya mawakili kwa kuwa hajui sheria za Tanzania za namna ya kuwasilisha
Malalamiko dhidi ya JAJI au HAKIMU.
WANAOTAKA TANZANIA ISITAWALIKE
WANAJUA KUWA UKITIKISA MAHAKAMA UNATIKISA UTAWALA WA SHERIA NA UNATIKISA UHAI
WA TAIFA LETU.
WANAOTAKA NCHI ISITAWALIKE HUITWA
“ANARCHISTS” au “DEMAGOGUES”. Hawa wameongezeka sana chini ya kivuli cha
demokrasia na haki ya kusema chochote popote bila kjali sheria yoyote au haki
ya mtu mwingine yeyote.
MAHAKAMA MKIYUMBA SISI WANANCHI
WA KAWAIDA NDIO TUTABAKI MIKONONI MWA ANARCHISTS na DEMAGOGUES WASIOHESHIMU
SHERIA NA AZMA YAO YA TANZANIA ISITAWALIKE itatimia.
MUNGU IBARIKI JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment