Powered By Blogger

Tuesday, August 21, 2012

Sababu 7 zilizopelekea C.C.M kushindwa Igunga




Chama cha Mapinduzi jana kilioteza jimbo la Uchaguzi la igunga baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kutengua matokea ya uchaguzi huo, yaliyompa ushingi Dk. Kafumu mapema oktoba mwaka jana.

Akiiongoza Mahakama hiyo Mheshimiwa Jaji Mary Shangali alitangaza kutengua Uchaguzi huo baada ya kurishika na hoja saba kama zifuatavyo:Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali alisema Mahakama ilipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili, lakini baadaye yakaongezwa madai mengine mawili hivyo kufikia 17.“Madai yaliyopokewa na Mahakama ni 17 na kati yake imethibitisha madai saba,” alisema Jaji Shangali katika hukumu hiyo.

1.   Kwamba Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Igunga. 

2.   Kwamba Dk Magufuli akiwa katika moja ya kampeni za uchaguzi huo, alitumia nafasi ya uwaziri kwa kuwatisha wapigakura wa jimbo hilo kwa kusema kama hawatamchagua mgombea wa CCM, watawekwa ndani. 

3.   Kwamba Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage alitangaza kuwa mgombea wa Chadema alikuwa amejitoa katika uchaguzi huo, jambo ambalo Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliokuwa ukitolewa.

4.   Kwamba kitendo cha Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage kupanda na bastola jukwaani, kulipelekea wapiga kura kuhofia na kuleta dosari katika uchaguzi huo.

5.   Kwamba kauli ya Imamu Swaleh Mohamed wa Msikiti wa Ijumaa Igunga, kuwatangazia waumini wa msikiti huo kuwa wasikichague Chadema, kwa kuwa baadhi ya viongozi wake wamemdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

6.   Kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kudai kuwa Chadema kilileta makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuuvuruga.
7.   Hoja nyingine ambayo Jaji Shangali aliikubali ni ugawaji wa mahindi ya kuwawezesha wakazi wa Igunga kukabiliana na njaa wakati wa uchaguzi huo kwamba ulitumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kuwashawishi wananchi wawapigie kura. Jaji huyo alihoji iwapo wakazi wa Jimbo la Igunga walikuwa na njaa sana wakati wa uchaguzi huo kiasi cha viongozi wa Serikali kuona kuwa ulikuwa wakati mwafaka wa kugawa mahindi hayo.

Hata hivyo haijaeleweka mara moja iwapo chama cha mapinduzi kitakata rufaa Mahakama ya rufani au vipi. Ila kwa mujibu wa sheria wanayo nafasi hio.

No comments: