Powered By Blogger

Tuesday, July 17, 2012

WAZIRI NA MWANASHERIA WATISHIWA KUUAWA.


Dr. Huvisa

SERIKALI imepata hasara ya sh. milioni 50 katika utekelezaji wa bomoa bomoa kwa wakazi waliojenga ndani ya hifadhi ya bahari ya Hindi, eneo la Mbezi Beach na Kawe, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Dkt. Terezya Huvisa, aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa bomoa bomoa ambayo ilifanyika Julai 10 mwaka huu katika maeneo hayo na kusisitiza kuwa, Serikali itawadai wote waliobomolewa nyumba zao ili kurejesha gharama zilizotumika.


Alisema mbali ya kufanikisha bomoa bomoa hiyo, amepokea vitisho vya kuuwawa na watu wasiofahamika kupitia simu yake ya mkononi kama ataendelea na mpango huo.

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi za Mazingira (NEMC), Bw. Heche Manchare, nae alikumbana na vitisho vya kuuawa ambapo taarifa hizo zimeripotiwa polisi.

“Sheria ya mazingira inatamka wazi kuwa, gharama zinazotokana na hatua mbalimbali za kuondoa tatizo la kimazingira, zitarejeshwa na watuhumiwa waliosababisha tatizo husika.


“Kimsingi mimi sitishiki na vitisho hivi, Serikali itaendelea  kusimamia sheria ya mazingira na haitamvumilia mtu, watu au kikundi kinachotishia watumishi wa Serikali ambao wanatekeleza kazi za usimamizi wa sheria za nchi.

“Endapo watagundulika, hatua kali dhidi yao zitachukuliwa, tukumbuke kuwa Serikali imeazimia kukabiliana na tatizo hili ambalo ni kubwa hasa wakati huu tunapokumbwa na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Dkt. Huvisa.

Aliongeza kuwa, gharama hizo ni kubwa lakini kama wananchi watafuata sheria zitaepukwa na uzingatiaji sheria na taratibu za nchi uwe wajibu wa kila mwananchi ili kuepuka hasara inayotokea Serikali inapoamua kutumia nguvu kutekeleza sheria.

Dkt. Huvisa alisema bomoa bomoa hiyo ilifanywa na ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Manispaa ya Kinondoni na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo polisi walihusika kuimarisha ulinzi katika utekelezaji.

Alisema ubomoaji huo ni utekelezaji wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ambapo nyumba 17 zilibomolewa yakiwemo majengo ambayo ujenzi wake ulikuwa ukiendelea katika mkondo wa mto.

“Lengo la kufanya hivi ni kuiepusha jamii na madhara yatokanayo na mafuriko ya mara kwa mara, fukwe, mito na vijito vinatakiwa kuwa wazi ili maji ya mvua yaweze kupita kwa wingi kama iliyonyesha Desemba 2011.

“Mvua hii ilisababisha vifo na uharibifu mali katika Bonde la Msimbazi, vitendo vya kuzuia mikondo ya maji, kuipindisha, kuichepusha au kuifinya upana wake kwa kujaza kifusi ni makosa chini ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004,” alisema.

Hata hivyo, Dkt. Huvisa aliwataka wote waliojenga au kuendelea na ujenzi katika maeneo yenye vyanzo vya maji, kando ya bahari, maziwa, mito, mabwawa na misitu inayolindwa kisheria kuondoka mara moja na wale ambao watakiuka agizo hilo, hatua za kisheria zitachukuliwa, kubomolewa nyumba, kuondolewa katika maeneo hayo na kulipia gharama zote za ubomoaji.

“Agizo hili pia linawahusu wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika vyanzo vya maji,” alisema Dkt. Huvisa na kusisitiza kuwa, baada ya Bunge kazi hiyo itaendelea katika mikoa yote ya Tanzania ili kusimamia sheria husika.

Pia Dkt. Huvisa alitolea ufafanuzi wa nyumba iliyojengwa kwenye kiwanja namba 2019/2020 na kudai kuwa, Wizara yake imepokea zuio la Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi na zuio la kuivunja.

“Hata hivyo, hakuna mamlaka yoyote ya Serikali iliyotoa kibali kwa ujenzi huo hivyo hatua stahiki zitachukuliwa baada ya kesi kuamuliwa na imepangwa Septemba 20 mwaka huu,” alisema.Chanzo gazeti la Majira.

No comments: