MH.JUNDU WA KWANZA MBELE |
JAJI Kiongozi Fakhii Jundu amekanusha madai
yaliyotolewa na Mnadhimu wa Upinzani Tundu Lisu kuwa majaji wengi wanaoteuliwa
na Rais Jakaya Kikwete huteuliwa bila ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
Akizungumza na mahakimu na wafanyakazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Mahakama ya Wilaya ya
Kinondoni na Mahakama ya Mwanzo ya
Kinondoni, alisema majaji wote wanaoteuliwa na Rais Kikwete wanateuliwa baada
ya kufuata taratibu zote ikiwamo na ile ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
“Kumekuwapo na malalamiko kuwa
kuna majaji wanateuliwa na Rais bila ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama, malalamiko hayo si ya kweli
hakuna jaji aliyewahi kuteuliwa bila ya kuwapo kwa ushauri
wa Tume ya Mahakama,”alisema Jaji Kiongozi.Pia alisema
kumekuwepo na malalamiko mengi
yanayoelekezwa katika idara za mahakama
ikiwamo ucheleweshwaji wa utoaji wa haki, mrundikano wa mashauri mahakamani na
kutolewa kwa hukumu zenye utata.
Jaji Jundu alisema jamii na wadau mbalimbali wamekuwa wakipeleka malalamiko kwao ya kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu
kuhusu ucheleweshwaji wa utoaji haki katika mashauri yanayowakabili kwa
wakati.
Hivyo aliwaagiza mahakimu kuwahimiza mawakili wa serikali katika kila
shauri kukamilisha upelelezi haraka iwezekanavyo na dhamana zitolewe bila ya kuwapo kwa
masharti magumu ili kupunguza mrundikano wa mahabusu gerezani.
“Mahakimu wengi wamekuwa
wakipenda kutoa adhabu za vifungo kitu ambacho kinasababisha mrundikano wa
mahabusu gerezani, angalieni uwezekano
wa kutumia adhabu mbadala kwa sababu
sheria inaruhusu ili kupunguza mrundikano huo wa mahabusu katika magereza, huko
hali siyo nzuri,”.Alisema mashauri yanayo suasua
wayapunguze mahakamani kwa kuzingatia kanuni ya siku 60 na aliwaonya kwamba wasiitumie kanuni hiyo vibaya.
Kwa upande wa mashauri yaliyokaa
muda mrefu, Jaji Jundu alisema ‘kama
shauri limekaa muda mrefu, washtakiwa
wakiachiliwa huru kuwakamata ni mchezo
unaoiabisha mahakama’.
Jaji huyo pia aliwataka mahakimu nchini kujipanga,
kuwahi kazini na kusikiliza mashauri kwa
wakati na kutoa hukumu mapema
iwezekanavyo zikiwamo kesi za madai.
Aliwasisitiza mahakimu kuacha
kutumia vifungu vya sheria vya kiufundi vinavyopokonya haki na
kusababisha mrundikano wa mahabusu
magerezani.
“Kuna baadhi ya mahakimu katika
mashauri ya mirathi wanajifanya wao
ndiyo wagawa mali au wananufaisha watu wengine wasiostahili na familia husika; hakimu kazi yake ni kuteua
msimamizi wa mirathi na si vinginevyo ,”alisisitiza kusema Jaji huyo Kiongozi.
Hivyo aliwataka mahakimu kuepuka
rushwa, wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wanaongoza kwa kupokea rushwa kitendo
ambacho kinaifedhehesha idara hiyo ya mahakama na kuwaonya kuwa wanapopokea
rushwa wasione kuwa hiyo ni siri
ikibainika hatua kali zitachukuliwa. Chanzo gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment