Watu wawili wameuawa kwa kucharangwa mapanga na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi baada ya kuvamia hoteli ya kitalii ya Mbweni Ruins, iliyoko nje kidogo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi majira ya alfajiri na kuwataja waliouawa kuwa ni dereva wa hoteli hiyo, Pius Paulo na mlinzi, Abdalla Simba.
Kamanda Juma alisema dereva huyo alikufa papo hapo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kucharangwa kwa mapanga kichwani na Mlinzi huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambako alikimbizwa kwa matibabu.Alisema mlinzi mwingine wa hoteli hiyo, Said Abdalla, anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo kutokana na majeraha aliyoyapata kwa kucharangwa kwa mapanga na majambazi hayo.
Alisema majambazi hayo ambayo yalikuwa na silaha za kienyeji baada ya kuvamia hoteli hiyo na kufanya mauaji hayo yaliiba kompyuta tatu ikiwemo moja ndogo (laptop) na kubwa mbili na fedha taslim zinazokadiriwa kufikia sh. 104,000 Alisema baada ya majambazi hayo kufanya uvamizi huo, walinzi walijaribu kupambana nao, lakini walizidiwa. Katika tukio hilo hakuna mgeni aliyejeruhiwa.Kamanda huyo alisisitiza kuwa polisi wanaendelea kuyasaka majambazi hayo na kuwaomba wananchi kulisaidia jeshi hilo kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaowatilia mashaka katika maeneo yao.
Habazi zaidi zinadai kuwa dereva huyo amezikwa kijijini kwao Kizimbani katika Wilaya ya Magharibi Unguja na mlinzi makaburi ya Mwanakwerekwe. Habari zinaeleza kuwa baada ya majambazi hao kumcharanga mapanga Pius kichwani pia walimvua nguo zote alizokuwa amevaa na kumchoma na vitu vyenye ncha kali katika baadhi ya maeneo ya mwili wake.
Kwa upande wao wafanyakazi wa hoteli hiyo, walisema dereva huyo alilala hotelini hapo ili kuwahi kuwapeleka uwanja wa ndege watalii kwa ajili ya kurudi nchini kwao." Tukio hili ni la pili kwa hoteli yetu kuvamiwa na majambazi. Kwa mara ya kwanza tukio kama hili lilitokea mwaka 2001, lakini hakuuawa mtu,” alisema mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo.
Mfanyakazi huyo ambaye alikataa kutaja jina lake alidai wamesikitishwa na huduma duni katika chumba cha wagonjwa mahatuti cha Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.Hospitali hiyo inakabiliwa na hali mbaya baada ya mashine zote tano za kusaidia wagonjwa mahatuti kuharibika kwa zaidi ya mwaka mmoja na kusababisha madaktari kutumia mitungi ya oxygen.Wafanyakazi wengi wa hoteli za kitalii Zanzibar wameshauri vyombo vya dola kuimarisha ulinzi katika miradi ya kitalii hasa wakati huu wa msimu wa utalii unaoendelea Zanzibar. source IPP.
No comments:
Post a Comment