Powered By Blogger

Monday, September 17, 2012

Majaji kesi ya Lulu 'wawazodoa' mawakili pande zote


Mojawapo wa Picha za Lulu akiwa Mahakamani
Gazeti la Majira limeandika; MAWAKILI wa pande zote mbili katika shauri la umri wa mshtakiwa wa kesi ya mauaji ya Elizabert Michael 'Lulu' wamejikuta katika wakati mgumu wakati wa uwasilishwaji wa hoja za shauri hilo katika Mahakama ya Rufaa.

Mawakili hao walikutwa na hali hiyo mahakamani hapo jana baada ya Jopo la Majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo kuwahoji kuwa wanabishania umri wa mshtakiwa huyo ili iweje?, ikiwa kesi ya mauaji husikiliwa katika Mahakama Kuu hata kama kosa hilo likiwa limetendwa na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.

Jopo la majaji wanaosikiliza shauri hilo ni Jaji Benard Luanda, Jaji January Msoffe na Jaji Benard Mtakagwa.

Jaji Msoffe aliieleza mahakama hiyo kuwa suala la umri lingeweza kutazamwa katika utolewaji wa hukumu hata kama wasingeomba mshtakiwa huyo achunguzwe umri wake.

Alisema  suala hilo pia  lingeweza kuingizwa wakati kesi hiyo itakapofikishwa Mahakama kuu wakati wa uwasilishwaji wa hoja za awali.

Alisema  malumbano hayo hayamsaidii mshtakiwa huyo kwani anaendelea kusota lumande kwa sababu katika kesi za mauaji sheria ya mtoto haihusiki.

"Kesi itahamishiwa Mahakama Kuu hata Kama inamuhusu mtoto wa miaka saba,ubishani wa umri kuanzia Mahakama ya Kisutu hadi hapa ili iwe nini?"alihoji Jaji Msoffe

Naye Jaji Luanda alihoji mawakili hao kuwa wanalumbana umri ili iwe nini, kwani kosa la mauaji hata kama likimhusisha mtoto wa umri wa mwaka mmoja sheria ya mtoto haihusiki.

Alisema  labda upande wa utetezi uieleze  mahakama hiyo kuwa mtoto wa miaka 17 hashtakiwi kwasababu mshtakiwa huyo sio wa kwanza kushtakiwa kwa kesi ya mauaji.

Wakati akiwasilisha hoja za upande wa mashtaka,wakili wa serikali mwandamizi Faraja  Nchimbi alidai kuwa msingi wa malalamiko yao ni dosari zilizojitokeza katika uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu na Jaji Fauz Twaib.

Alidai  uwauzi wa Mahakama hiyo kukubali kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo haukuwa sahihi kwa sababu katika uamuzi wake Jaji Dkt.Twaib alikiri kuwa maombi ya upande wa utetezi hayakuwasilishwa mahakamani hapo kihalali kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa,hivyo jaji huyo hakupaswa kukubali kuendelea kufanya uchunguzi na badala yake angetupilia mbali ombi hilo.
Alidai kuwa  Jaji huyo alikosea kutoa tafsiri ya kifungu namba 44(1) cha sheria ya Mahakimu na kwamba alipaswa kutoa maelekezo kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika uamuzi wake.

Aliongeza kuwa waliomba mahakama ya rufaa ifanye marejeo ya uamuzi wa Jaji Twaibu badala ya kukata rufaa kwakuwa marejeo husikilizwa haraka ukilinganisha na rufaa.

Kwa upande wake wakili wa utetezi Bw.Peter Kibatala akiwasilisha hoja zake alidai kuwa hoja yao ya msingi kutaka umri wa mshtakiwa huyo uchunguzwe ilikuwa kulida maslahi ya mtoto.

Kibatala alidai kuwa kulinda maslahi hayo sio tu shauri hilo kuhamishiwa mahakama ya watoto bali pia  katika utolewaji wa adhabu hukumu itakapofika.

Alidai kuwa hawakuwa na namna ya kuingiza ushahidi wa umri wa mshtakiwa huyo isipokuwa kwa njia hiyo.

Kibatala alisema  msimamo wa upande wa utetezi ni kwamba shauri hilo lirudishwe katika Mahakama ya Kisutu liendelee na taratibu za awali za kimahakama.

Katika kesi hiyo Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakamaya Hakimu Mkazi Kisutu,ambapo anadaiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba Aprili 7, mwaka huu. Chanzo gazeti la Majira.

No comments: