Powered By Blogger

Thursday, December 1, 2011

JERI MURO AACHIWA HURU!

Jerry  Muro  akiongea na waabdishi wa habari baada ya kuachiwa huru.
 MAHAKAMA jijini Dar es Salaam, imewaachia huru aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgasa, baada ya kuonekana kuwa hawana hatia katika mashtaka matatu yaliyokuwa yakiwakabili, likiwamo la kuomba rushwa ya Sh 10 milioni.  

Katika kesi hiyo ilikuwa inadaiwa kuwa Januari 29 mwaka jana, Muro na wenzake walitenda  makosa ya  kula njama, kushawishi kupewa rushwa ya Sh 10 milioni kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Michael Wage na kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru.

Hukumu iliyowaachia huyu washtakiwa hao, ilisomwa jana saa 3:15 asubuhi na Hakimu Mkazi Frank Moshi  wa Mahakama ya Kisutu.Hakimu huyo alisema mahakama imewaachia huru washtakiwa  baada ya upande wa mashtaka, kushindwa kuyathibitisha makosa pasipo kuacha shaka.  Katika shtaka la kula njama, Hakimu Moshi alisema  baada ya mahakama kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka, iliwaona washtakiwa  kuwa wana kesi ya kujibu na kuwataka kuwasilisha utetezi wao . 
Alisema hata hivyo baada ya kupitia ushahidi na utetezi uliotolewa na washtakiwa pamoja na ule wa shahidi wao mmoja (dereva wa Muro) katika shtaka la kula njama, mahakama imewaachia huru washtakiwa wote.

 ”Mahakama imewaachia huru washtakiwa katika shtaka la kula njama kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa  kuithibitishia mahakama kama kweli washtakiwa walikutana na Wage na kufanya mawasiliano kupitia simu ya mkonon,” alisema hakimu Moshi.  Alisema mahakama imeona kuwa ushahidi wa nakala za picha za CCTV za hoteli ya Sea Cliff, zilizowasilishwa  na upande wa mashtaka zikionyesha watu watatu, sura zao zilikuwa hazionekani, jambo linalofanya ushahidi huo kuwa na upungufu.

Hakimu huyo alisema ili  watu waweze kutenda kosa la kula njama lazima wawe wanafahamika na kwamba  hakuna ushahidi mwingine wowote  unaonyesha kuwa kweli washtakiwa hao walitenda kosa hilo.Alisema upande wa mashtaka ulishindwa hata kumuita dereva wa Wage  ili aweze kuthibitisha kama kweli Wage na Muro waliwahi kuwa na mawasiliano au  kukutana katika Mgahawa wa Calfonia.

Alisema upande wa mashtaka pia ulishindwa hata kwenda kwenye makampuni ya simu ili kupata nakala za ujumbe mfupi wa simu (sms) waliokuwa wakitumiana Wage na Muro.

Alisema kitendo hicho kinaifanya mahakama isiamini kama kulikuwa na kosa la kula njama.  “Pamoja na kutokuwepo  kwa ushahidi wa mawasiliano pia upande wa mashtaka ulitakiwa upeleke mahakamani hati ya gwaride la utambuzi  ili kuithibitishia mahakama kama washtakiwa waliwahi kutambuliwa lakini hilo haliufanyika,”alisema hakimu Moshi. 

Katika shtaka la kuomba rushwa, hakimu Moshi alisema  mahakama haijaonyeshwa  ushahidi  wa kuthibitisha kuwa washtakiwa walipokea rushwa ya Sh 1 milioni  kutoka kwa Wage  kama kitangulizi  cha rushwa waliyoiitaji ya Sh10 milioni.

Alisema mahakama ilitegemea kuwa kungekuwa na ushahidi wa mawasiliano au wa kuona ili kuonyesha uhalisia na kwamba eneo la Hoteli ya Sea Cliff,.

Aliongeza kuwa washtakiwa  Kapama na Mgasa walikamatwa katika maeneo tofauti tofauti, jambo liliosababisha mahakama kuwaachia huru hasa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka hilo.  Kuhusu shtaka  la kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru, linalokuwa likiwakabili Kapama na Mgasa, Hakimu Moshi alisema kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na vielelezo, hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa Wage aliwatambua washtakiwa hao katika gwaride la utambuzi.  

Alisema  vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani na upande wa mashtaka vinaonyesha kuwa mshtakiwa Mgasa alikiri kujitambulisha kuwa ni wafanyakazi wa TBC wakati katika maelezo ya mashahidi, inadaiwa kuwa walijitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru.

Alisema kwa msingi huo mahakama inawaachia huru washtakiwa hao kuwa shtaka hilo linajikanganya.
“Washtakiwa wote wameachiwa huru  hata hivyo mahakama hii inazingatia kuwa kuna vielelezo kama risiti, pingu na bastola ambavyo havikuwa na mgogoro  hivyo virejeshwe kwa Muro. Na  kwa Yule  ambaye hajaridhika, haki ya kukata rufaa iko wazi,” alisema hakimu Moshi.  

Muro alipanda kizimbani Agosti 18 mwaka huu ambapo alijitetea na kuiomba mahakama  imuone kuwa hana hatia, akidai kuwa kesi inayomkabili ni ya kubambikiziwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.

Kesi hiyo ilipata hakimu mpya Frank Moshi Mei 2 mwaka huu  baada ya  Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe  kuhamishiwa katika Mahakama Kuu.Machi 8 mwaka huu hakimu huyo aliwaona washtakiwa hao kuwa wana kesi ya kujibu.Kwa kipindi chote hicho cha kusikilizwa kwa kesi hiyo washtakiwa wote walikuwa nje kwa dhamana kwa mujibu wa sheria. 

Yaliyojiri katika kesi
Muro aingia matatani Dar Januari 31 mwaka jana, siku kadhaa baada ya Muro kutoa habari zilizoanika rushwa zinazofanywa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, mwandishi huyo aliingia matatani kwa kukamatwa aidaiwa  kuomba na kupokea rushwa.

Baada ya kukamatwa alishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Muro, ambaye aliwahi kushinda tuzo ya Mwanahabari Bora wa mwaka 2009 kufuatia habari yake ya rushwa inayofanywa na askari wa usalama barabarani, alikumbwa na mkasa huo saa 6:00 jijini Dar es Salaam.

Alikamatwa wakati akiwa katika Hoteli ya Sea Cliff.Taarifa za awali zilisema Muro alikamatwa baada ya kuwekewa mtego na polisi kufuatia taarifa ilizokuwa zimetolewa na  mfanyabiashara mmoja, ambaye jina halijawekwa bayana kuwa mwandishi huyo alikuwa anadai rushwa ya Sh10 milioni.

Apekuliwa, akutwa na Pingu
Baada ya kukamatwa, polisi walilipekuwa gari la alilokuwa akilitumia na kukuta pingu pamoja na bastola.Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Maalum ya Dar es salaam, Suleiman Kova, alisema baada ya kulifanyia upekuzi gari la Muro, polisi walikuta pingu na bastola na baadaye walimwamuru mwandishi huyo awapelekee stakabadhi zinazoonyesha kuwa alinunua pingu hizo kwa njia halali.


Muro apandishwa kizimbani
Februari 5 mwaka jana Muro alipandishwa kizimbani akishtakiwa kwa mashtaka ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh10 milioni.

Alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Alipandishwa kizimbani akiwa na wenzake wawili  waliokuwa wakidaiwa uwa alishirikiana nao katika kutenda kosa hilo. Watu hao walisomewa mashtaka matatu.Washtakiwa walifikishwa mahakamani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari waliokuwa wamevalia nguo za kiraia.

Kesi yaanza kusikilizwa
Kesi dhidi ya Muro na wenzake wawili ilianza kusikilizwa Juni 24 mwaka jana katika hatua ya awali.Hatua hiyo ilikuja baada ya  kukamilika kwa upelelezi wa kesi uliokuwa umekwama kwa muda mrefu.

Wakili wa Serikali, Martha Misonge, alisema mbele ya Hakimu Gabriel Milumbe siku hiyo,  ilikuwa ni ya  kusomewa washtaiwa maelezo ya awali.Hata hivyo  aliomba  wasomewe siku iliyofuatia kwa sababu upande wa mashtaka haukuwa tayari.

Katika hatua hiyo washtakiwa walitakiwa kueleza mambo wanayokubaliana nayo na yale wasiyokubaliana nayo.

Muro alidai kusomea jeshi Marekani, Afrika Kusini
Juni 16 mwaka jana, upande wa mashtaka ulieleza mahakama kuwa  Muro alijinadi kuwa ni askari wa JWTZ mwenye cheo cha Kapteni  ambaye alipata mafunzo yake katika nchi za  Marekani, Uingereza na Afrika Kusini.

Maelezo hayo yalitolewa na wakili wa serikali, Boniface Stanslau mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe.
Ilidaiwa kuwa Muro alimweleza Michael Karoli aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa  kwa  mafunzo hayo alikuwa na uwezo wa kumweka chini ya ulinzi na kwamba alimuonyesha pingu na bastola kama vifaa vyake vya kazi.

Korti yaelezwa njama za kumkandamiza Muro
 Agosti 24 mwaka jana, mshtakiwa Deogratias Mgasa alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Charles Mkumbo na wenzake walimlazimisha  aandike maelezo ya kumkandamiza Muro na kwamba kama angekataa wangembambikia kesi ya mauaji.

Mgasa aliyasema hayo  wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe.

Akitoa ushahidi wake,Mgasa alidai kuwa Februari 3 mwaka jana, alikubali kuandika maelezo yanayomkandamiza Muro, baada ya kulazimishwa na Mkumbo ambao walimwambia kuwa asipofanya hivyo watampa kesi nyingine ikiwamo ya mauaji.

Mahakama yapokea mkanda wa video

Novemba 13 mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, ilipokea nakala za picha zilizotolewa katika mtandao wa CCTV Camera ya Hoteli ya Sea Cliff, kama moja ya  vielelezo vya ushahidi  katika  kesi ya Muro na wenzake wawili.

Nakala hizo za picha , zinawaonyesha washtakiwa Muro , Deogratias Mgasa na aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage Karoli, ambaye inadaiwa walimuomba rushwa,wakiwa katika eneo la Hoteli ya Sea Cliff.


Shahidi adai Muro alinunua pingu duka la JWTZ

Januria 25 mwaka huu,  shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, Inspekta wa Polisi Anthony Mwita (45), aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa Muro aliwahi kumkabidhi stakabadhi ya pingu aliyoinunua katika duka la JWTZ, Upanga, jijini Dar es Salaam.

Mwita alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe alipokuwa akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Pingu za Muro zawasilishwa kortini   
 Siku ya Januari 26 mwaka huu, pingu alizokutwa nazo Muro ziliwasilishwa katika Mahakamani ya Kisutu kama sehemu ya ushahidi.Ilidaiwa kuwa pingu hizo zilikutwa ndani ya gari la Muro wakati akikaguliwa na Inspekta wa Polisi.

Madai hayo yalitolewa na Mrakibu  Mwandamizi wa Polisi, Duwan Nyanda (49), mbele ya Hakimu Mkazi Mirumbe, wakati akitoa ushahidi wake.


“Wage aliniambia kuwa pingu hizi zilitumiwa  na Muro kumfunga  wakati anamtishia na kumuomba rushwa,”alidai shahidi huyo wa sita wa upande wa mashtaka.

Muro na wenzake wana kesi ya kujibu
Machi 8 mwaka huu, Muro na wenzake walipatikana na kesi ya kujibu katika  mashtaka matatu yaliyokuwa yakiwakabili likiwamo la kuomba rushwa ya Sh 10 milioni kutoka kwa Kalori.

Mashtaka mengine ni ya kula njama  na kujitambulisha kuwa ni maofisa wa serikali.

Uamuzi huo, ulitolewa na Hakimu Mkazi Mirumbe baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Boniface Stanslaus kufunga ushahidi wa upande wa mashtaka.


Muro amlipua Masha
Agosti 18 mwaka huu, Muro aieleza mahakama kuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alimtambia kuwa hatochomoka katika sakata hilo.

Muro alieleza hayo alipoanza kujitetea kwa mara ya kwanza dhidi ya tuhuma ziizokua zikimkabili.

Katika utetezi wake uliodumu kwa saa tatu akiongozwa na mawakili wake, Majura Magafu na Richard Rweyongeza, Muro alidai kwamba Masha  alisema mwisho wa kesi hiyo unampeleka (Muro) kaburini. Chanzo gazeti la Mwananchi.

1 comment:

JigambeAds said...

Pole sana Bro Jerry Muro na wenzako, na tunamshukuru Mungu kwa kuachiwa huru, tuendelee kujenga taifa!