Powered By Blogger

Wednesday, November 23, 2011

Mahakama Kuu yatupilia Mbali kesi ya Ubunge, Mwibala.

Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi ya pingamizi uchaguzi wa ubunge Jimbo la Mwibara mkoani Mara, iliyofunguliwa na mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mahakama hiyo imemtangaza rasmi mgombea wa CCM, kwamba alishinda kihalali katika uchaguzi huo.

Aliyekua mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mwibara Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Chiriko Aron David, amepinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, juu ya kesi yake ya kupinga matokeo dhidi ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Kangi Lugola (CCM), na anatarajia kukata Rufaa katika Mahakama Kuu ya Rufaa.

Katika madai yake mgombea wa Chadema, alidai kuwa taratibu za uchaguzi zilikiukwa, ikiwa ni pamoja na mgombea wa CCM, kuanza kampeni mapema, vitendo vya rushwa, kutumia gari la ubalozi, kutishia wananchi kwa kuwafyatulia risasi na msimamizi wa uchaguzi hakufuata taratibu za uchaguzi huo.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa nne, Jaji Chocha alisema hakuna ushahidi wowote unaojitosheleza wa kutengua matokeo ya uchaguzi jimbo hilo, kwani mgombea wa CCM alishinda kihalali.

Alisema katika hoja zote zilizotolewa na upande wa mashitaka, ikiwemo hoja ya rushwa, mashahidi wote walioletwa hawakuziunga mkono moja kwa moja hoja hizo, na pia ushahidi wao ulipingana, ikiwa ni pamoja na wengine kutokujiamini, hali iliyoashilia kuwa huenda ulikuwa wa kupangwa.

Alisema kwa jinsi hiyo anaamini kuwa wananchi wa Jimbo la Mwibara, walitumia demokrasia yao vizuri kwa kuchagua mbunge waliyemuona kwamba anawafaa kuwaletea maendeleo na hivyo kuifungua kesi mahakamani ni kuwacheleweshea maendeleo yao.

Alisema katika maelezo ya mashahidi wote akiwemo shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji, hakuona kama gari la ubalozi lilikuwa na makosa kwani picha zilizopigwa kama kielelezo zilionesha gari hilo likiwa limesimama, hivyo haamini kama gari hilo lilikuwa kwenye kampeni ya mgombea wa CCM, kama ilivyodaiwa.

Kuhusu rushwa, Jaji Chocha wakati wa kesi inaendelea, hakuna shahidi ye yote aliyethibitisha moja kwa moja rushwa hiyo, aliipokea nani na hata waliopewa hawakufika mahakamani kuthibitisha hilo.
 
Hatima pekee iliyobaki kwa mgombea huyo wa Chadema ni kukuata rufaa Mahakama ya rufaa  au kuomba marejeo ya kesi hio.

No comments: