Powered By Blogger

Friday, November 18, 2011

Bunge lapitisha Muswada wa katiba Mpya.

Mh. Makinda
BUNGE limeupitisha kwa hoihoi, nderemo na vifijo, Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, huku Serikali ikisisitiza kuwa mchakato wa Muswada huo ulifuata taratibu zote bila kukiuka Katiba.

Pia Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, amesisitiza kuwa mtu atakayekwamisha utekelezaji wake, atakabiliwa na adhabu kali na kubainisha kuwa adhabu katika Muswada huo imeongezwa kutokana na hali halisi ya matukio ya kisiasa yanayoendelea.


Wakati akihitimisha jana hoja ya Muswada huo bungeni, Spika Anne Makinda, alisema hajui sababu halisi ya wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi, kususa mjadala wa Muswada huo, na hata alipomwuliza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, kuhusu suala hilo hakuwa na majibu.


Jana katika mkutano wa tano, kikao cha tisa saa saba mchana, wabunge wa CCM na wa CUF kwa pamoja waliboresha vifungu vya Muswada huo kwa kuongeza vingine vitatu na kuupitisha.


Awali wakati akijibu hoja za michango ya wabunge iliyotolewa wakati wa mjadala kuhusu Muswada huo, Kombani alisema kuwasilishwa kwa Muswada huo bungeni ni halali na kwamba haukupaswa kusomwa kwa mara ya kwanza kama inavyodaiwa.


Alisema Muswada huo hauna tofauti na wa awali na ushahidi uko kwenye kipengele cha maudhui ambacho hakijabadilishwa na katika Muswada wa sasa kilichofanyika ni kuuboresha kutokana na maoni ya wadau.


Aidha, alisisitiza kuwa madai ya Kambi ya Upinzani kutaka Rais asiteue Tume hayawezekani kubadilishwa, kwa kuwa ukweli unabaki kwamba Rais ni Mkuu wa Nchi na ndiye mwenye mamlaka ya masuala yote makubwa yanayotokea nchini.


Kuhusu hoja ya vyama vya siasa kushiriki kuteua Tume, alisema haiwezekani kwa kuwa kila chama kina ilani yake, hivyo iwapo itatokea kutofautiana, hakuna kitakachofanyika zaidi ya vurugu na kutukanana.


Tundu Lissu apotosha “Naomba hapa nihadharishe Kambi Rasmi ya Upinzani iwe makini na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na kupitia matamko yake, kabla ya kuwasilishwa kwani, maoni aliyotoa katika mjadala huu sina uhakika kama amehusisha chama, mengi ni yake,” alisema Kombani.


Aidha, alisema mambo mengi yamepotoshwa na Msemaji huyo, kutokana na ukweli kuwa amekuwa hauhudhurii vikao vya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambamo ni mjumbe, matokeo yake amekuwa akipotosha kuhusu utendaji wa Kamati.


Alisema asilimia kubwa ya maoni yaliyotolewa dhidi ya Muswada huo yamepotoshwa na kuwataka Watanzania wasikubali kuchonganishwa na kuvunjiwa amani na umoja wao.


Mwanasheria Mkuu Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema anashangazwa na hoja ya Muswada huo kusomwa mara ya kwanza wakati ulishasomwa mara ya kwanza, na kilichofanyika ni kuuboresha kutokana na maoni ya wadau.


“Inashangaza Muswada huu ndio umeng’ang’aniwa usomwe eti kwa mara ya kwanza, mbona Muswada wa Ununuzi wa Umma uliletwa hapa mwaka jana, juzi ukasomwa kwa mara ya pili na haukulalamikiwa, hata Muswada wa Uchaguzi vivyo hivyo,” alisema.


Alisisitiza kuwa kutokana na hali halisi ilivyo, adhabu iliyokuwapo kwenye kifungu cha adhabu kwa atakayekwamisha utekelezaji wa Muswada huo, imeongezwa kutoka kifungo cha miaka mitatu hadi saba na faini ya Sh milioni tano hadi Sh milioni 15.


Akihitimisha mjadala huo, Makinda alisema Muswada huo ulipita kihalali kwa kufuata taratibu zote na kanuni za Bunge ikiwamo Katiba pamoja na wananchi kushirikishwa kupitia mikutano ya hadhara.


Alisema kitendo cha Chadema na NCCR-Mageuzi kutoshiriki kimewanyima wananchi wao haki ya kusikiliza michango yao iwe ya kukosoa au kuboresha ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kuzingatiwa na kusikilizwa.


“Jana (juzi) nilikutana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani (Mbowe) nilimwuliza sababu za kutoka ili nijue kama nimekosea sehemu basi nijisahihishe, ingawa tayari nilishajichunguza na kuuliza wataalamu wangu na kukuta sijakosea chochote.


“Kusema ukweli Mbowe hakuniambia chochote kuhusu sababu halisi za wao kutoka, ndiyo maana nasema hawa wamewakosesha haki wananchi wao, kama wanapinga wangebaki ndani wawasilishe mawazo yao na kwa uchache wao yangesikilizwa,” alisisitiza. Chanzo Habari leo.

No comments: